KOCHA Mkuu wa Muembe Makumbi, Sheha Khamis, amesema ushindani wa Ligi Kuu Zanzibar unazidi kupamba moto kutokana na kila mmoja kuwa na uhitaji wa kujiweka sawa kwenye nafasi nzuri, huku wao wakiweka mikakati ya kumaliza salama.

Sheha amesema katika ligi hiyo, zipo baadhi ya timu ambazo zinapambana kusaka ubingwa huku nyingine zikijinusuru kushuka daraja jambo ambalo linafanya kila mechi kuwa ngumu.

Amesema kutokana na ugumu wa mechi hizo, hakuna timu inayoweza kuingia uwanjani ikiwa na uhakika wa ushindi bila maandalizi mazuri.

“Tunaendelea kujipanga kuhakikisha tunaendana na kasi ya ligi licha ya baadhi ya wachezaji wa timu yetu kufungiwa, tuna kikosi kipana kinachoweza kuleta ushindani,” amesema.

Hata hivyo, kocha huyo amewapongeza wachezaji wa kikosi hicho kwa kazi nzuri wanaoifanya kuipambania timu hiyo kwa kila mechi.

Alieleza kuwa, mipango ya timu hiyo ni kufanikisha kwamba wanafanikiwa kutoshuka daraja na nguvu zote ni kupata matokeo mazuri ya kila mechi.

Kwa upande wake, mchezaji wa timu hiyo, Ali Khamis Kibwete, amesema wataendelea kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha timu hiyo inabaki salama.

Aliwasihi mashabiki kuendelea kuwaunga mkono katika kipindi hiki cha mwisho wa msimu huku akiahidi kuwa wachezaji watajituma ili timu ifikie malengo yake.

Muembe Makumbi yenye pointi 34 baada ya mechi 25, inashika nafasi ya tisa ikiendelea kupambana kukimbia zaidi na eneo la hatari ya kushuka daraja zikibaki mechi tano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *