
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, imeondoa amri ya Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, iliyoelekeza Evelyn Chiomba kuondolewa katika nyumba yake ya makazi iliyopo Kitalu namba 317, Regent Estate, Dar es Salaam.
Amri ya kuondolewa kwa amri ya RC Chalamila imetolewa leo Ijumaa, Mei 15, 2026, na Jaji Arnold Kirekiano na kuelekeza hali ibakie kuwa kama ilivyokuwa awali kabla ya amri hiyo ya RC Chalamila na utekelezaji wake.
Mahakama hiyo imetoa amri hiyo kwa muda kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa shauri la maombi alilolifungua Evelyn la kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi na maelekezo hayo ya RC Chalamila.
RC Chalamila alitoa amri na maelekezo hayo ya kumuondoa bibi huyo mwenye umri wa miaka 83 aondoke yeye mwenyewe na familia yake pamoja na mali zao, au aondolewe kwa nguvu katika nyumba hiyo Mei 6, 2026.
Katika maelekezo hayo, RC Chalamila alisema kuwa bibi huyo si mmiliki wa nyumba hiyo, na kwamba wamiliki halali ni Godfrey Japhet Shuma na Callista Godfrey Shuma.
Kutokana na amri na maelekezo hayo ya RC Chalamila, bibi huyo na familia yake aliondolewa ndani ya nyumba hiyo chini ya usimamizi wa askari wa Jeshi la Polisi na kukabidhiwa wanafamilia hao wa Shuma.
Hata hivyo, Evelyn amefungua mahakamani shauri la maombi dhidi ya RC Chalamila kwa jina lake na kwa wadhifa wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) akiwa mjibu maombi wa pili, na Godfrey Japhet Shuma na Callista Godfrey Shuma, wakiwa wajibu maombi muhimu.
Evelyn anayewakilishwa na Wakili Ferdinand Makore, chini ya hati ya dharura sana, inayothibitishwa na Wakili Makore, akibainisha sababu mbalimbali za dharura hiyo, pamoja na mambo mengine akidai kuwa mteja wake huyo, licha ya umri wake mkubwa, pia kwa sasa hana makazi.
Katika shauri hilo anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama ili mahakama itoe amri za kutengua uamuzi na maelekezo ya RC Chalamila, na amri ya mahakama ya kumzuia RC Chalamila kutoa uamuzi, amri au maelekezo mengine ya kiutawala kuhusu nyumba hiyo.
Pia aliomba amri za muda za kudumisha hali iliyokuwepo awali kabla ya uamuzi, amri na maelekezo ya RC Chalamila kuhusiana na nyumba hiyo, hadi maombi hayo ya kibali yatakapoamuliwa pamoja na maombi ya msingi ya mapitio ya mahakama atakayoyafungua baada ya kupata kibali.
Vilevile aliomba mahakama itoe amri ya muda ya kuhifadhi nyumba hiyo na kuwazuia wajibu maombi, mawakala, warithi wao au mtu mwingine yeyote anayefanya kazi chini ya maelekezo au maagizo ya RC Chalamila au wajibu maombi wengine.
Amri hiyo ya zuio inahusu uchukuaji, umiliki, au kufanya aina yoyote ya uhamisho au kuhitimisha makubaliano yoyote ya kibiashara au mpango wowote kuhusiana na uhamisho wa nyumba hiyo hadi kuamuliwa kwa maombi ya msingi ya mapitio ya kimahakama atakayoyafungua baada ya kupata kibali.
Shauri hilo limetajwa leo kwa ajili ya maelekezo muhimu, na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ayoub Sanga, kwa niaba ya mjibu maombi wa kwanza na wa pili (RC Chalamila na AG), ameomba mahakama wapewe siku 14 kuwasilisha majibu.
Wakili Sanga amedai kuwa watu wanaoshughulikia suala hilo katika ofisi ya mkuu huyo wa mkoa wako Morogoro, na watakuwepo Dar es Salaam Jumatatu, na kwamba kuanzia Jumapili mawakili wote wa Serikali watakuwa wanahudhuria mkutano jijini Arusha kwa wiki nzima.
Naye Wakili wa wadaiwa muhimu, Godfrey na Callista, Dickson Mtobeseo, ameomba siku 14 kujibu maombi hayo akidai kuwa amepewa nyaraka za shauri hilo leo asubuhi na kwamba hajakutana na wateja wake ambao nao wana changamoto ya kiafya.
Hata hivyo, kufuatia maombi hayo ya mawakili wa wajibu maombi kuomba siku 14, Wakili Makore (wa mwombaji) ameikumbusha mahakama kuwa shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura, huku akibainisha kuwa kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa mashauri hayo ya maombi ya kibali, yanapaswa kuamuliwa ndani ya siku 14, na kwamba kanuni hizo pia zinaruhusu kutoa kibali hata bila kusikiliza upande mwingine.
Huku akirejea uamuzi wa kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa na mahakama hiyo, Wakili Makore amesema haitakuwa mara ya kwanza kutoa amri kama hizo wakati shauri likisubiri kuamuliwa.
“Kwa kuzingatia mazingira ya shauri hili kama ilivyo kwenye hati ya dharura, ni kwamba mwombaji, kwa kuzingatia umri wake wa utu uzima, kwa sasa hana pa kulala,” amesema Wakili Makore na kuongeza:
“Kwa hiyo wakati tunasubiri kusikilizwa, mahakama yako itoe amri ya ku-maintain status quo ante (kudumisha hali ilivyokuwa kabla) kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa shauri hili.”
Huku akirejea uamuzi wa mashauri mbalimbali ya Mahakama Kuu, Wakili Makore amesema haitakuwa mara ya kwanza kutoa amri kama hizo wakati shauri likisubiri kuamuliwa.
“Hivyo nikualike tu mamlaka uliyo nayo na kwa busara za mahakama yako. Mazingira ya shauri hili, kama utakubaliana na maombi ya Wakili wa Serikali, basi utoe amri hizo,” amesisitiza Wakili Makore.
Jaji Kirekiano baada ya kusikiliza hoja za pande zote amesema kuwa kwa kuwa wajibu maombi wameomba kuwasilisha viapo kinzani ndani ya siku 14 na kwa kuwa mawakili wa Serikali hawatakuwepo kwa juma zima, mahakama inatoa nafasi ya kuwasilisha viapo hivyo ndani ya muda huo.
“Wakati tukisubiri viapo, amri ya muda mfupi ya kudumisha hali iliyokuwepo kabla dhidi ya mjibu maombi wa kwanza (RC Chalamila) na mawakala wake au watu wanaoweza kufanya kazi kwa maelekezo yake imekubaliwa kwa sasa wakati tukisubiri usikilizwaji,” amesema Jaji Kirekiano.
Kwa uamuzi huo, amri na maelekezo ya RC Chalamila yaliyosababisha bibi huyo mjane kuondolewa katika nyumba hiyo yameondolewa, na kwa maana hiyo bibi huyo anarejea katika nyumba yake hiyo wakati shauri linaendelea kusikilizwa mpaka litakapoamuliwa.
Jaji Kirekiano amepanga kuendelea na usikilizaji wa shauri hilo Mei 29, 2026 saa 5:00 asubuhi.
Kwa mujibu wa kiapo chake Evelyn, yeye na mumewe walipata kiwanja mwaka 1976, na kwa pamoja mwaka 1978 walijenga nyumba hiyo ambamo waliendelea kuishi mpaka mumewe alipofariki mwaka 1978, na baada ya kifo chake aliendelea kuishi humo bila usumbufu wowote kutoka mtu yeyote.
Umiliki wa mumewe katika nyumba hiyo haujawahi kupingwa wala kubatilishwa kwa amri au maelekezo yoyote kutoka mahakamani kupitia shauri, rufaa au mapitio yoyote.
Lakini kwa mshangao na masikitiko Mei 6, 2026, RC Chalamila alifika kwake na kutoa maelekezo ya kumtaka aondoke katika nyumba hiyo yeye na familia yake na mali zake ndani ya saa moja, au aondolewe kwa nguvu.
RC Chalamila wakati akitoa amri hiyo alieleza kuwa kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi iliyowasilishwa kwake na kamati iliyoanzishwa na yeye mwenyewe, wamiliki wa nyumba hiyo ni Godfrey Japhet Shuma na Callista Godfrey Shuma, ambao walipaswa kukabidhiwa umiliki wa nyumba hiyo.
Bibi huyo anadai kuwa muundo, mamlaka na uaminifu wa kamati hiyo vina mashaka, na kwamba taarifa yake, kwa ufahamu wake, haikuungwa mkono na taratibu zilizowekwa wazi, kumbukumbu au msingi wowote unaoweza kuthibitishwa.
Pia anadai kuwa ameelezwa na washauri wake wa kisheria kuwa RC hana mamlaka chini ya Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura ya 97, wala chini ya mfumo wa sheria za ardhi kuamua migogoro ya ardhi kati ya raia au watu binafsi.
Anadai kuwa kuna viashiria vya rushwa na ushawishi wa kifisadi katika uamuzi uliosababisha kuondolewa katika nyumba yake, kwani aliombwa na kamati hiyo Sh250 milioni ili asiondolewe, lakini akakataa.