
Arusha. Serikali imesema sekta ya fedha nchini inaendelea kuonesha ukuaji mkubwa na uthabiti, huku ikiitaka benki na taasisi za kifedha kuongeza ubunifu, kupunguza gharama za huduma na kuwafikia Watanzania wengi zaidi ambao bado hawatumii huduma rasmi za benki.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, wakati wa Siku ya Uwekezaji kwa Wanahisa wa benki ya CRDB iliyofanyika leo, Mei 15, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Waziri Omar amesema Serikali inaendelea kujenga sekta ya fedha iliyo imara, jumuishi, shindani na inayochochea mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha pamoja na Mkakati wa Taifa wa Upatikanaji wa Huduma Jumuishi za Fedha.
Amesema mafanikio makubwa yanaendelea kushuhudiwa katika masoko ya mitaji, na thamani ya uwekezaji imeongezeka kutoka Sh47.2 trilioni mwaka 2024 hadi Sh63.1 trilioni mwaka 2025, sawa na ukuaji wa asilimia 33.7, huku mauzo ya hisa na dhamana yakiongezeka kwa asilimia 91.
Kwa mujibu wa waziri huyo, sekta ndogo ya benki ambayo ndiyo mhimili mkuu wa mfumo wa fedha nchini, sasa inachangia zaidi ya asilimia 71 ya mali zote za sekta ya fedha.
Amesema mali za benki zimeongezeka kutoka Sh39.3 trilioni mwaka 2021 hadi Sh77 trilioni mwaka 2025, huku amana zikiongezeka kutoka Sh28.5 trilioni hadi Sh53.5 trilioni na mikopo kufikia Sh46.7 trilioni.
Aidha, kiwango cha mikopo chechefu kimepungua kutoka asilimia 5.8 mwaka 2021 hadi asilimia 2.8 mwaka 2025, jambo alilosema linaonesha uimara wa sekta hiyo pamoja na kuongezeka kwa ubora wa huduma za kifedha nchini.
Hata hivyo, Waziri Omar amesema bado kuna changamoto ya kuwafikia wananchi wengi zaidi, akibainisha kuwa utafiti wa FinScope wa mwaka 2023 unaonesha ni asilimia 22 pekee ya Watanzania wanaotumia huduma za benki.
“Hivyo wito wangu kwa benki zetu nchini ni kuendelea kubuni na kuchukua hatua mahususi ili kuwafikia Watanzania wenzetu waliobakia, yaani asilimia 78,” amesema Waziri Omar.
Amesisitiza umuhimu wa vijana kushiriki katika uwekezaji wa hisa, hati fungani na mifuko ya uwekezaji, akieleza kuwa vijana ni nguvu muhimu katika uchumi kutokana na mchango wao katika uzalishaji mali, ubunifu na maendeleo ya teknolojia.
Katika hafla hiyo, Waziri Omar ameipongeza benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika uchumi wa Taifa, akisema benki hiyo inatoa takribani asilimia 29 ya mikopo yote kwa sekta binafsi nchini.
Amesema mwaka 2025 benki hiyo ilipata faida safi baada ya kodi ya Sh725 bilioni, huku akieleza matumaini kuwa hivi karibuni itaweka rekodi mpya ya kufikia faida ya Sh1 trilioni.
Mbali na hilo, waziri huyo amesifu juhudi za benki hiyo katika kuendeleza bidhaa bunifu za kifedha, ikiwemo Samia Infrastructure Bond, hati fungani za kijani pamoja na bidhaa zinazozingatia misingi ya Sharia kama Sukuk.
Aidha, amesema upanuzi wa huduma za CRDB katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na mipango ya kuingia Kenya na Zambia ni hatua muhimu katika kuipeperusha Tanzania kimataifa.
Pia, Waziri Omar amesisitiza umuhimu wa kulinda wanahisa wadogo pamoja na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu viwango vya riba na gharama za miamala ya benki.
“Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa katika utendaji wetu sote tujielekeze katika kuwapa tabasamu Watanzania,” alisema.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya benki ya CRDB, Profesa Neema Mori, amesema idadi ya wawekezaji wa benki hiyo imeongezeka kutoka 30,000 mwaka 2021 hadi 89,000 hivi sasa, wengi wao wakiwa vijana.
Profesa Mori amesema benki hiyo itaendelea kuimarisha utawala bora, kuongeza uwekezaji katika teknolojia, kupanua huduma za ujumuishi wa kifedha na kuongeza thamani kwa wanahisa wake.
Kwa upande wake, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Jesper Kammersgaard amesema ushirikiano kati ya Denmark kupitia Danida na CRDB ulianza tangu miaka ya 1990 ukiwa na lengo la kuijengea uwezo taasisi hiyo.
Amesema Denmark itaendelea kuiunga mkono CRDB ili iendelee kuwa imara na kukua zaidi, hasa katika kipindi ambacho mamilioni ya wananchi wanategemea mifumo ya benki katika maisha yao ya kila siku.
Balozi huyo pia ameipongeza CRDB kwa uwekezaji na uamuzi wa kuhamia kwenye mfumo mpya wa core banking, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya ukomavu wa taasisi hiyo pamoja na dhamira ya kuendelea kuboresha huduma kwa wateja.