
Mbeya. Halmashauri ya Jiji la Mbeya imetumia zaidi ya Sh11.743 bilioni kutekeleza na kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo sekta ya elimu, afya, kilimo na uwekezaji.
Imeelezwa kuwa kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh9.744 bilioni ni mapato ya ndani ya halmashauri, huku Sh1.999 bilioni ni fedha kutoka Serikali Kuu.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Mei 15, 2026, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justine Kijazi, amesema lengo la Serikali ni kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya elimu, afya, biashara, kilimo na uwekezaji.
“Utekelezaji wa miradi umezingatia usawa wa kisekta, kata na majimbo mawili, likiwemo la Mbeya Mjini na Uyole, ili kufikisha huduma muhimu kwa wananchi kupitia sekta husika,” amesema.
Kuhusu sekta ya afya, amesema zaidi ya Sh2.465 bilioni zimetumika kutekeleza ujenzi wa miundombinu, huku Sh801.8 milioni zikiwa mapato ya ndani na Sh1.663 bilioni kutoka Serikali Kuu.
Amesema miongoni mwa fedha hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa shule mbili mpya za msingi za Utulivu, Kata ya Iwambi na Ilembo, Kata ya Iyela, huku Sh282.1 milioni zikitumika kukarabati Shule ya Msingi Itezi.
Kuhusu shule kongwe
Kijazi amesema halmashauri imetumia zaidi ya Sh116.964 milioni kukarabati Shule ya Msingi Chemchem, kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanajifunza na kujifunzia katika mazingira mazuri.
Amesema hadi kufikia Aprili 2026, halmashauri imetumia Sh801.819 milioni kutekeleza miradi ya sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa matundu 77 ya vyoo, ukarabati, ujenzi wa vyumba 33 vya madarasa, uzio na uchongaji wa madawati 2,222 kwa elimu ya msingi.
Amesema kwa elimu ya sekondari, jumla ya Sh58.4 milioni zimetolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu manne ya vyoo katika Shule za Sekondari Old Airport na Ilomba, huku mapato ya ndani Sh100.7 milioni yakitumika kukarabati Shule ya Msingi Halinji.
Kuhusu sekta ya afya
Amesema halmashauri imetumia Sh827.9 milioni kutekeleza miradi ya sekta ya afya, kati ya hizo Sh550.3 milioni zikiwa mapato ya ndani.
Ametaja miradi iliyotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati katika Kata za Nonde, Nsoho, Isanga na Itezi, pamoja na ukarabati wa kituo cha afya Mwakibete, Isyesye, Itagano na Hospitali ya Wilaya ya Igawilo.
“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta Sh227.6 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji katika zahanati ya Itensa, Kata ya Nsalaga, sambamba na huduma ya mama na mtoto,” amesema.
Amesema manufaa ya miradi hiyo ni kusogeza huduma muhimu kwa jamii na kuchangia kukua kwa shughuli za kiuchumi na kuongeza mapato ya halmashauri.
Katika hatua nyingine, amesema halmashauri imetenga Sh400 milioni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya masoko ya Igawilo, Ukuti, Nsalaga na Iganjo jijini hapa.
“Tutaboresha vyanzo vya mapato na usimamizi wa shughuli za uwekezaji, ukarabati wa ukumbi wa Mkapa na kutenga Sh322.9 milioni kununua mashine ya PoS,” amesema.
Kauli za wananchi, wadau
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wananchi wamesema katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan wameona mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali, hususan afya, elimu na barabara za mitaa.
“Mafanikio hayo hayaji peke yake, bali ni matokeo ya usimamizi thabiti wa wateule wake, akiwemo Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya. Kwa kipindi kifupi tumeona mabadiliko makubwa,” amesema Joyce Aidan.
Naye Peter Fredy amependekeza halmashauri kuishauri Serikali kuanzisha mitalaa ya elimu ya ujasiriamali shuleni ili kuandaa vijana kujiajiri baada ya kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu.
“Huku nje hali ya maisha kwa vijana wasomi si nzuri, lakini tumeona uchapa kazi wa uongozi wa halmashauri katika kuboresha miradi ya kimkakati, hususan katika sekta ya elimu na afya,” amesema.