Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa gawio la Sh8.38 bilioni kwa Serikali, huku faida, mizania na kiwango cha mikopo vikiongezeka.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ishara ya kuimarika kwa benki hiyo ya maendeleo, wakati sekta ya kilimo ikiendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa taifa na chanzo kikuu cha ajira kwa Watanzania wengi vijijini.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema Serikali, ambayo ni mwanahisa mkuu na mwanahisa pekee wa TADB, imepata gawio hilo ambalo ni ongezeko la asilimia takribani 50 kulinganisha na gawio la mwaka uliopita la Sh5 bilioni.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa wa benki hiyo uliojadili taarifa ya mwaka wa fedha pamoja na mahesabu yaliyokaguliwa, uliofanyika leo Mei 15, 2026, jijini Dar es Salaam, Mchechu amesema, “Kiwango cha faida kimekuwa kizuri kulinganisha na mwaka jana.

“TADB ni benki ambayo inakua kwa kasi zaidi. Nitumie nafasi hii kuzitaka taasisi zote ziige mfano huu kwa kuendelea kuongeza kiwango cha faida kwa mwanahisa.”

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (katikati) kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Frank Nyabundege katika picha ya pamoja mara baada ya mkutano wa mwaka wa wanahisa wa benki hiyo.

Amesema kama kiwango cha faida kitaongezeka kwa asilimia 50 au 100, ni wazi taasisi hizo zitakuwa zikiitendea haki nchi na uwekezaji, akibainisha kuwa Serikali inahitaji kuongeza mapato yasiyo ya kikodi yanayotokana na uwekezaji ilioufanya.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Ishmael Kasekwa, amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa bodi na menejimenti ya benki.

Amesema gawio la mwaka huu limeongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka uliopita, jambo linaloonesha kasi ya ukuaji wa taasisi hiyo ya kifedha.

“Maendeleo haya yametokana na usimamizi mzuri wa benki pamoja na ushirikiano mkubwa kati ya bodi na menejimenti, hivyo basi tutaendelea kuhakikisha benki inaendelea kufanya vizuri zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema ukuaji huo umechangiwa na kuongezeka kwa utoaji wa mikopo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ambazo zinaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi.

Amesema mizania ya benki imeongezeka kutoka Sh917 bilioni hadi zaidi ya Sh1.3 trilioni, huku kiwango cha mikopo kikikua kutoka Sh926 bilioni hadi zaidi ya Sh1.34 trilioni ndani ya kipindi hicho.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) wakiwa katika picha ya pamoja na msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (katikati) kushoto kwake ni Mwenyekiti wa bodi hiyo,  Ishmael Kasekwa na kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Frank Nyabundege mara baada ya mkutano wa mwaka wa wanahisa wa benki hiyo.

Amesema kupitia huduma za mikopo, benki hiyo imeendelea kuchochea shughuli za uzalishaji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi, hasa wanaotegemea kilimo.

“Kupitia mikopo yetu tayari tumegusa maisha ya zaidi ya wananchi milioni 2.6 moja kwa moja au kwa njia nyingine,” amesema, na kufafanua kuwa mbali na shughuli za kifedha, TADB pia imeendelea kushiriki katika utekelezaji wa shughuli za kijamii kwa kusaidia wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *