NI wikiendi spesho katika ulimwengu wa soka kuanzia ndani ya Tanzania, nje ya mipaka ya nchi hii lakini hapahapa Afrika, pia kule Ulaya napo hapatoshi. Siku hizi mbili kwa maana ya Jumamosi na Jumapili, kuna mechi za moto sana.
Robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB inapigwa leo Jumamosi mechi mbili, Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Singida Black Stars kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, kisha saa 12:30 pale Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, JKT Tanzania itaikaribisha Yanga.
Kesho Jumapili saa 10:00 jioni, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Mashujaa itaikaribisha Azam, halafu robo fainali ya mwisho ni Simba dhidi ya TRA United saa 12:30 jioni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Pia kuna fainali mbili za mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Leo Jumamosi ni marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Zamalek ikiikaribisha US Alger pale jijini Cairo, halafu kesho ni fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Mamelodi Sundowns ikiwa nyumbani nchini Afrika Kusini, itakuwa mwenyeji wa AS FAA Rabat kutoka Morocco, hakika hii ni Wikiendi Spesho.
Kule Ulaya, leo Jumamosi ni fainali ya Kombe la FA, Chelsea itapambana na Manchester City kwenye Uwanja wa Wembley katika mchezo mkali unaosubiriwa kwa hamu.
COASTAL UNION VS SINGIDA BLCK STARS
Robo fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la CRDB inachezwa jioni ya leo saa 10:00 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Wenyeji Coastal Union wanaikaribisha Singida Black Stars, mechi ambayo imebeba kumbukumbu ya mara ya mwisho kukutana hapo wenyeji kushinda 2-1, Mei 2, mwaka huu.
Kwa Coastal Union, mechi hii ni sehemu ya kuendelea kudhihirisha kwamba haikubahatisha katika ushindi wa kwanza, huku ikipata nguvu zaidi ya kutoka ugenini kuifunga Mbeya City mabao 2-0 katika Ligi Kuu Bara.
Ni mechi inayowakutanisha wanafainali wawili ambao wote walikutana na Yanga kwa nyakati tofauti na kupoteza. Coastal Union walicheza fainali ya michuano hii msimu wa 2021-2022 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na kumaliza muda wa kawaida kwa sare ya 3-3, wakaenda kupoteza kwa penalti 4-1.
Singida Black Stars walicheza fainali msimu uliopita 2024-2025 dhidi ya Yanga na kufungwa 2-0 pale kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Coastal wanajua wazi kuwa kucheza nyumbani ni faida ambayo lazima itumike ipasavyo kwa sababu mechi za mtoano mara nyingi huamuliwa kwa makosa madogo sana.
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias, tayari ameonyesha kujiamini akisisitiza kuwa kikosi chake kimejiandaa vizuri tangu walipowasili Tanga.
“Tumefanya mazoezi kuanzia jana (juzi) baada ya kufika Tanga, tunategemea kuwa na mchezo mzuri kulingana na maandalizi tuliyofanya. Tunataka kuvuka hatua hii na kuingia nusu fainali ya CRDB, tunafahamu ni mchezo mgumu na Singida ni timu yenye ubora mkubwa ila tutaingia uwanjani kucheza mchezo wa mtoano na kutafuta matokeo bora,” alisema kocha huyo.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wa Coastal, Abdallah Denis, ameweka wazi kuwa morali ya kikosi ipo juu huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa timu nguvu.
“Wachezaji tuko tayari kukabiliana na Singida na tunautaka mchezo ili tuvuke kwenda nusu fainali. Kocha amefanya kazi yake na wachezaji tutaingia uwanjani kufuata maelekezo ya mwalimu ili tushinde mchezo. Mashabiki wetu waje kwa wingi, tunaahidi kuwapa furaha tena pale CCM Mkwakwani,” alisema nyota huyo.
Kwa upande wa Singida Black Stars, imeonesha kiwango kizuri katika kipindi cha karibuni na imekuwa moja ya timu zinazocheza kwa nidhamu kubwa ya kiufundi.
Kocha Muhibu Kanu ameweka wazi kuwa mafanikio ya mechi zilizopita yamewekwa pembeni na akili zote sasa zimehamia kwenye pambano hili la mtoano.
“Ni kweli tumepata matokeo mazuri nyumbani lakini akili imeshatoka huko na sasa tunawaza namna ya kuwakabili Coastal Union ili kwenda hatua ya nusu fainali na baadae ikiwezekana tuingie tena fainali,” alisema Kanu.
Singida wanaingia wakiwa na nguvu kubwa ya uzoefu wa mechi za ushindani pamoja na uwezo wa kucheza kwa utulivu hata katika mazingira magumu ya ugenini.
Mchezaji wa kikosi hicho, Miraji Abdallah, alisema kikosi kipo tayari na kwamba kila mchezaji amejipanga kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
“Tunafahamu ugumu wa mchezo hapo kesho (leo) dhidi ya Coastal Union, lakini hata sisi tupo hapa kuhakikisha tunavuka hatua inayofuata. Sisi kama wachezaji tutahakikisha tunafuata maelekezo ya walimu wetu ili kufanya vizuri mchezo wa kesho (leo).”
Kiufundi, mchezo huu unaweza kuwa wa tahadhari kubwa. Coastal huenda wakaanza kwa kasi wakitaka kutumia presha ya nyumbani kupata bao la mapema, lakini hilo linaweza kuacha nafasi kwa Singida kutumia mashambulizi ya kushtukiza. Timu itakayodhibiti eneo la kiungo na kutumia nafasi zake vizuri ndiyo inaweza kubeba tiketi ya nusu fainali.
JKT TANZANIA VS YANGA
Nusu fainali ya msimu uliopita katika mashindano haya, ni kama tunakwenda kushuhudia marudiano yake msimu huu ambapo timu hizo zinakutana hatua ya robo fainali, mechi ikipangwa kuanza saa 12:30 jioni.
Msimu uliopita, ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Yanga dhidi ya JKT Tanzania, uliwapeleka fainali na kwenda kutetea ubingwa wao. Safari hii ni robo fainali, kila upande unataka kudhihirisha ubora wake.
Yanga inayoongoza kwa kubeba taji la michuano hii tangu kuanzishwa kwake msimu wa 1967 enzi za FAT Cup, imefanya hivyo mara tisa huku nne mfululizo ikiwa kuanzia 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na msimu uliopita 2024-2025.
JKT Tanzania inaisaka fainali yake ya kwanza ya michuano hii kwani rekodi zinaonyesha wakati inaitwa JKT Ruvu iliwahi kubeba mwaka 2002, ambapo ilikuwa mara ya mwisho kwa michuano hiyo kufanyika ikifahamika kama Kombe la FAT, kisha kurejea mwaka 2015 na kuitwa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na sasa ni Kombe la Shirikisho la CRDB.
Yanga chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Abdihamid Moallin, wana kazi ya kujiuliza mbele ya maafande hao kwani Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo haujawa rahisi kwa mpinzani kwenda na kuondoka na ushindi.
Kwa Yanga, huu ni mtego wanaopaswa kuutegua baada ya kuvunjwa rekodi yao ya mechi 42 mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza kuja kukwama mbele ya Dodoma Jiji ilipofungwa 3-2, hivi karibuni.
MASHUJAA VS AZAM
Saa 10:00 jioni kesho Jumapili, vijana wa Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ Mashujaa watakuwa nyumbani kuikaribisha Azam, ambayo msimu huu zilipokutana uwanjani hapo katika mechi ya Ligi Kuu Bara, hakukuwa na mbabe, matokeo yakiwa 0-0.
Mashujaa iliyokuwa na rekodi ya kutopoteza nyumbani msimu huu, imejikuta ikikwama mbele ya Simba ilipofungwa 3-0, juzi Alhamisi katika Ligi Kuu Bara.
Azam chini ya Kocha Florent Ibenge, inahitaji kufanya vizuri katika mashindano haya msimu huu ili kufika fainali nyingine baada ya kupoteza 2023-2024 kwa penalty 6-5 dhidi ya Yanga.
Mabingwa hao wa msimu wa 2018-2019 ukiwa ni ubingwa wao pekee wa michuano hii, wanahitaji kurudia tena makali yao, hivyo ushindi mbele ya Mashujaa ni muhimu kwao ili msimu huu wasitoke patupu kwani mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara zinaonekana kuwa ngumu kwao.
SIMBA VS TRA UNITED
Timu hizi tayari msimu huu zimekutana mara mbili katika ligi, ambapo Wekundu wa Msimbazi waliifunga mara moja huku mechi ya mwisho zikitoka suluhu ugenini mjini Arusha.
Simba inakumbuka mara ya mwisho ilipoikaribisha TRA United pale Meja Jenerali Isamuhyo iliondoka na ushindi mzuri wa mabao 3-0, hata hivyo hii haitakuwa rahisi huku macho ya wengi yakiwa kwa winga wa TRA United, Ramadhan Salum Chobwedo, vita yake na beki wa kushoto wa Simba, Nickson Kibabage inaweza kuamuliwa hapa.
Mara ya mwisho wawili hao kukutana, kulikuwa na vita kubwa ambapo mara kadhaa Chobwedo alimtesa Kibabage, lakini wakati mwingine winga huyo alikwama.
Simba inahitaji ushindi ili kuingia nusu fainali, kisha fainali kwenda kubeba ubingwa wa michuano hii ilioukosa kwa misimu mine.
Mara ya mwisho Simba yenye rekodi ya kubeba ubingwa wa michuano hii mara nne, taji lake la mwisho lilikuwa msimu wa 2020-2021 ilipoifunga Yanag 1-0.
ZAMALEK VS USM ALGER
Jiji la Cairo nchini Misri litageuka kuwa sehemu inayotolewa macho zaidi kwa soka la Afrika leo Jumamosi wakati Zamalek itakapoikaribisha USM Alger katika mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, mechi inayobeba rekodi, historia na vita ya kutwaa taji.
USM Alger inaingia kwenye mchezo huu ikiwa mbele kwa ushindi wa bao 1-0 ilioupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa Algiers, wikiendi iliyopita.
Ushindi huo ulikuja kwa namna ya kusisimua baada ya Ahmed Khaldi kufunga penalti dakika ya 90+8 kufuatia uamuzi wa VAR uliyozua taharuki kubwa uwanjani.
Kinachofanya mchezo huu kuwa ya kipekee ni ukweli kwamba timu zote mbili zina historia ya kutopoteza fainali walizowahi kucheza katika mashindano haya.
USM Alger ilitwaa ubingwa mwaka 2023 ilipoifunga Yanga kwa faida ya bao la ugenini, huku Zamalek ikibeba mataji yao mawili ya awali katika fainali mbili ilizoingia.
Kwa Zamalek, mara zote ilipofuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilianza kwa kupoteza ugenini lakini ikaibuka bingwa baada ya kucheza nyumbani Cairo.
Ilitokea mwaka 2019 dhidi ya RS Berkane na tena mwaka 2024 dhidi ya timu hiyo hiyo ya Morocco.
Uwanja wa Kimataifa wa Cairo umekuwa ngome ya Zamalek msimu huu kwani timu hiyo haijapoteza hata mechi moja katika mashindano haya.
Hata hivyo, changamoto yao kubwa imekuwa kwenye eneo la ushambuliaji ambako imekuwa ikishinda kwa tofauti ndogo ya mabao.
Ili kutwaa ubingwa, Zamalek itahitaji ushindi wa angalau mabao mawili dhidi ya USM Alger, jambo linalomaanisha itahitaji kuwa na makali zaidi mbele ya lango.
Kwa upande wa USM Alger, morali ipo juu baada ya ushindi wa kwanza lakini changamoto kubwa ni rekodi yao ya ugenini. Katika mechi sita za ugenini msimu huu, imepata ushindi mara mbili pekee huku ikipoteza mbili. Hii inaonyesha kuwa safari ya Cairo haitakuwa rahisi kwao hasa mbele ya mashabiki wa Zamalek wanaojulikana kwa kutengeneza mazingira magumu kwa wapinzani.
Kiufundi, USM Alger inaweza kuingia kwa tahadhari kubwa ikitaka kulinda faida yao huku ikitegemea mashambulizi ya kushtukiza.
Zamalek kwa upande wao haina budi kushambulia tangu dakika za mwanzo kutafuta bao la mapema litakalorejesha imani ya mashabiki wao.
Hata hivyo, kushambulia kupita kiasi kunaweza kuwa hatari kwa wenyeji kwani bao moja la USM Alger linaweza kubadilisha kabisa hesabu za mchezo.
MAMELODI SUNDOWNS VS AS FAR
Katika upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kesho Jumapili macho yataelekezwa Afrika Kusini, wakati Mamelodi Sundowns na AS FAR zitakapokutana katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayobeba historia ya mabingwa wa zamani wanaotafuta kurejesha heshima zao.
Mamelodi Sundowns inaingia kwenye fainali hii ikisaka taji la pili la Afrika tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 2016. Kwa miaka kadhaa sasa, Sundowns imekuwa moja ya timu bora zaidi Afrika Kusini na imejijengea heshima kubwa kutokana na mfumo wao wa kucheza soka la pasi nyingi na umiliki mkubwa wa mpira.
Mchezo wa kwanza utakaopigwa Pretoria, unaweza kuwa muhimu sana kwa Sundowns kwa sababu wanajua safari ya Morocco si rahisi.
Rekodi yao nyumbani dhidi ya timu kutoka Morocco inawapa matumaini kwani hawajawahi kupoteza. Pia, katika misimu miwili iliyopita ya mashindano haya, hawajafungwa nyumbani.
Silaha kubwa ya Sundowns msimu huu imekuwa mshambuliaji Brayan Léon ambaye yupo kwenye kiwango bora baada ya kufunga mabao matano katika mechi tano alizoanza hivi karibuni.
Kama ataendelea na moto huo, anaweza kuwa tishio kubwa kwa safu ya ulinzi ya AS FAR.
Lakini upande wa AS FAR, wanaingia na silaha tofauti katika uimara wa kujilinda. AS FAR imeonyesha kuwa moja ya timu ngumu zaidi kufungika msimu huu baada ya kuruhusu wastani wa mabao 0.5 pekee kwa kila mchezo.
Takwimu hizo zinaonyesha namna ambavyo safu yao ya ulinzi imekuwa ngumu kupenyeka.
Golikipa Ahmed Tagnaouti ameonekana kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi kutokana na uwezo wake wa kuokoa hatari. Mara nyingi ameisaidia timu kuendelea kubaki kwenye michezo hata ilipokuwa chini ya presha kubwa.
Hata hivyo, rekodi ya AS FAR ugenini inaweza kuwa tatizo kubwa kwao. Katika michezo 12 ya ugenini kwenye mashindano haya, imefanikiwa kushinda mara mbili pekee. Hii inaweka presha kubwa kwao kuhakikisha hairuhusu kufungwa mabao mengi Pretoria kabla ya marudiano nyumbani Rabat.
Kiufundi, Sundowns itataka kumiliki mpira na kucheza kwa kasi kubwa ikitafuta mabao ya mapema. Lakini AS FAR inaonekana kuwa timu inayoweza kusubiri kwa nidhamu na kutumia makosa ya wapinzani kwenye mashambulizi ya kushtukiza.
Kwa ujumla, hii ni fainali ya falsafa mbili tofauti za soka, zinakutana timu inayopenda kushambulia dhidi ya timu inayopenda kujilinda kwanza.
