Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya kwa hatua yao ya haraka ya kufika katika eneo la barabara ya Tabata Bima–Kimanga mara baada ya changamoto ya ubovu wa barabara hiyo kuripotiwa bungeni na Mbunge wa Segerea, Agnesta Lambert Kaiza.
Kufuatia changamoto hiyo kuwasilishwa bungeni hivi karibuni na mbunge wa Segerea, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na timu ya TARURA walifika eneo hilo kufanya tathmini ambapo mkuu wa wilaya alisema kuwa tayari Serikali imetenga zaidi ya Tsh. Bilioni 1.7 kwa ajili ya kuboresha barabara hiyo ya Tabata Bima – Kimanga ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo leo Mei 15, 2026 bungeni Jijini Dodoma, Dkt. Dugange amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, ni serikali sikivu inayoweka mbele mahitaji ya wananchi kwa kuhakikisha viongozi wanachukua hatua za haraka pale changamoto zinapojitokeza.
Amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu katika mazingira bora, ikiwemo miundombinu ya barabara inayorahisisha usafiri, biashara pamoja na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Katika hatua nyingine, Dkt. Dugange ameahidi kuwa serikali ina mpango wa kuikarabati barabara ya Segerea kwa Bibi – Zahanati ya Segerea, baada ya Mbunge wa Segerea Agnesta Lambert Kaiza kuiomba serikali kutoa majibu kuhusu lini ukarabati wa barabara hiyo utaanza.
(Feed generated with FetchRSS)