Kongamano la Miji Duniani lafanyika Baku wakati mgogoro wa makazi na athari za tabianchi vikiongezekaKongamano la Miji Duniani lafanyika Baku wakati mgogoro wa makazi na athari za tabianchi vikiongezeka

Wakati Kongamano la  Umoja wa Mstaifa la 13 la Miji Duniani linafunguliwa kesho Jumapili 17 Mei mjini Baku, Azerbaijan, washiriki wanatarajiwa kujadili namna ya kukabiliana na mgogoro unaozidi kuongezeka wa makazi duniani.

Mkutano huo, ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-HABITAT kwa ushirikiano na serikali ya Azerbaijan, utawakutanisha viongozi wa dunia, mameya, wataalamu wa mipango miji pamoja na wawakilishi wa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na taasisi za kimataifa.

Lengo kuu: Kuweka dunia katika makazi salama

Kaulimbiu ya kongamano hilo ni wito wa kuchukua hatua: Makazi kwa Dunia: Miji na Jamii Salama na Imara. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karibu watu bilioni 2.8 wanaishi katika mazingira yasiyofaa ya makazi, huku zaidi ya milioni 300 wakiwa hawana makazi kabisa.

Na kwa kuwa karibu asilimia 70 ya watu duniani wanatarajiwa kuishi mijini ifikapo mwaka 2050, mgogoro huo unatarajiwa kuwa mkubwa zaidi.

Katika mahojiano na UN Video, Mkuu wa UN-Habitat, Anacláudia Rossbach, ameelezea hali hiyo kama “mgogoro wa kimataifa wa makazi.”

Amesema “Kwa muda mrefu mgogoro huu umekuwa mkubwa zaidi katika nchi za Kusini mwa dunia, lakini sasa pia unaanza kuonekana kwa kiwango kikubwa katika nchi za Kaskazini mwa Dunia”.

Kwa mujibu wa Bi. Rossbach, kupanda kwa gharama za maisha limekuwa tatizo kubwa, huku migogoro ya kimataifa ikiwemo vita vya Mashariki ya Kati na hatari zake kwa minyororo ya usambazaji bidhaa duniani zikizidisha hali hiyo.

© UN-Habitat / Alexia Seraiva Timu ya UN-Habitat inafanya ziara ya uwanja katika mji wa Izidora nchini Brazil.

Changamoto ni zaidi ya nyumba pekee

Mgogoro huo hauhusu tu kujenga nyumba. Makazi sasa yanaonekana kuwa msingi wa utu wa binadamu, mnepo wa miji na hata utulivu wa dunia.

Umoja wa Mataifa unaonya kuwa athari zake zinaonekana katika kila nyanja ya maisha kuanzia mifumo ya afya na elimu hadi uchumi na mshikamano wa kijamii.

Francine Pickup, Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP na mkuu wa ujumbe wa UNDP katika kongamano hilo, amesema taasisi hiyo inalenga kutumia mkutano wa Baku kuimarisha ushirikiano katika kutafuta suluhu jumuishi za miji zinazounganisha masuala ya makazi, mnepo dhidi ya tabianchi, utawala bora na ufadhili wa ndani.

“Mgogoro huu wa makazi duniani si tatizo la ujenzi pekee,” amesema Bi. Pickup. “Tunapaswa kwenda zaidi ya kujenga nyumba na kuangalia mazingira ya miji pamoja na suala la makazi kama changamoto changamano.”

Makazi holela: Changamoto na fursa

Moja ya mada kuu zitakazojadiliwa ni ongezeko kubwa la makazi holela au maeneo yasiyopangwa ambako wakazi hawana umiliki rasmi wa ardhi na wanaishi katika mazingira hatarishi.

Kwa sasa, takriban watu bilioni 1.1 wanaishi katika makazi duni, na makadirio yanaonesha kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa watu wengine bilioni mbili katika miongo ijayo.

Watoto ndio walio hatarini zaidi, huku kati ya watoto milioni 350 hadi 500 wakikadiriwa kuishi katika mazingira ya mabanda.

Wakati huo huo, UN-Habitat inataka mabadiliko ya mtazamo kuhusu makazi holela, kwani katika hali nyingi ndiyo njia pekee kwa mamilioni ya watu kupata makazi mijini.

UN News/Thelma Mwadzaya Mtaa wa mabanda wa Kibera, Nairobi Kenya

Kujenga upya baada ya migogoro

Suala jingine litakalopewa uzito ni jinsi miji inavyoweza kujijenga upya baada ya vita na majanga.

Kufikia mwisho wa mwaka 2022, zaidi ya watu milioni 123 duniani walikuwa wamelazimika kuyakimbia makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, huku zaidi ya asilimia 60 wakikimbilia maeneo ya mijini.

Kupoteza makazi si kupoteza paa pekee. Kunamaanisha pia kuvunjika kwa jamii, kupoteza ajira na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa salama.

Hivyo, mjadala wa Baku hautahusu tu kutoa makazi, bali pia namna ya kujenga upya maisha ya watu kuanzia kurejesha mitaa, kuunda ajira hadi kusaidia jamii kurejea katika hali ya kawaida.

Athari za tabianchi

Majadiliano pia yataangazia mabadiliko ya tabianchi. Wataalamu wanaonya kuwa mgogoro wa tabianchi sasa unakuwa chanzo kikuu cha mgogoro wa makazi duniani.

Matukio ya hali mbaya ya hewa kama mafuriko, dhoruba na moto wa nyika yaliwafanya zaidi ya watu milioni 20 kuhama makazi yao mwaka 2023 pekee. Makadirio yanaonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuharibu nyumba milioni 167 duniani ifikapo mwaka 2040.

Wakati huo huo, sekta ya ujenzi ni moja ya vyanzo vikubwa vya uzalishaji wa hewa chafuzi, ikichangia asilimia 34 ya uzalishaji wa hewa ukaa unaotokana na matumizi ya nishati duniani.

Hivyo, kongamano hilo litatafuta majibu ya jinsi ya kujenga makazi zaidi bila kuongeza kasi ya mabadiliko ya tabianchi.

“Kaulimbiu ya kongamano ni makazi. Tutachunguza suala hilo kwa mitazamo tofauti ikiwemo makazi holela, fedha, uendelevu na mnepo,” amesema Bi. Rossbach.

Ameongeza kuwa mjadala pia utahusu ujenzi mpya na uokoaji katika nchi zilizoathiriwa na vita na majanga.

“Kuna haja ya haraka si tu ya kutoa makazi, bali pia kujenga upya jamii kwa njia jumuishi, imara na endelevu,” amesema.

UN News Kwa kikao cha kumi na tatu cha Jukwaa la Miji Duniani (WUF13), ambalo litafanyika huko Baku mnamo Mei 2026, nembo ni zaidi ya ishara au kitambulisho cha kuona. Inawasilisha hadithi ambayo inaunganisha mada ya Jukwaa la kimataifa na utamaduni na utambulisho wa nchi yake mwenyeji, Azerbaijan.

Ushirikiano wa pamoja

Moja ya ujumbe mkuu wa kongamano hilo ni umuhimu wa hatua za pamoja zinazohusisha serikali, mamlaka za mitaa, vyuo vikuu, jamii na sekta binafsi.

“Jukwaa la Miji Duniani ndiyo jukwaa letu kubwa zaidi la kuwakutanisha wadau,” amesema Bi. Rossbach. “Tunatarajia kuona jamii pana na yenye uwakilishi mkubwa ikikusanyika Baku na kutoka WUF13 ikiwa na muungano imara zaidi wa kukabiliana na mgogoro wa makazi duniani.”

Miaka 10 ya Ajenda Mpya ya Miji

Kongamano la Baku pia linaadhimisha miaka kumi tangu kupitishwa kwa Ajenda Mpya ya Miji mwaka 2016.

Aidha, mwezi Julai mwaka huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani litafanya tathmini ya katikati ya utekelezaji wa ajenda hiyo, huku majadiliano ya Baku yakitarajiwa kusaidia kupima hatua iliyofikiwa katika kujenga miji salama, endelevu na nafuu kwa wote.

Kuhusu Kongamano la Miji Duniani

Kongamano la Miji la Dunia lilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2001 na huandaliwa na UN-Habitat kila baada ya miaka miwili. Linachukuliwa kuwa mkutano mkubwa zaidi wa kimataifa unaojadili maendeleo endelevu ya miji na mustakabali wa miji duniani.

Tangu kikao cha kwanza kilichofanyika mjini Nairobi mwaka 2002, kongamano hilo limekuwa likifanyika katika miji mbalimbali duniani.

Washiriki 40,000 wamejiandikisha kutoka nchi 182 ili kushiriki mkutano wa mwaka huu mjini Baku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *