Dar es Salaam. Nchi imeendelea kutafakari njia za kujinasua kutoka katika madhara ya vurugu zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Vurugu hizo zilisababisha zaidi ya watu 518 kuuawa na wengine mamia walijeruhiwa, baadhi wakibaki na ulemavu wa kudumu.
Katika kutafakari, wadau wa siasa katika makongamano mawili tofauti, wametaja njia za kulikwamua taifa kutokana na madhara ya vurugu hizo za kisiasa.
Makongamano hayo ni lile lililoandaliwa na Chama cha ACT-Wazalendo, lililokuwa na mada ya “Mjadala wa kitaifa kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi yetu.” Lingine ni liliandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso). Lilikuwa na kaulimbiu ya “Never Again” yenye ujumbe wa “Tuipende, tuitunze na tuiheshimu nchi yetu.”
Wadau hao wamependekeza mbinu mbalimbali za kulitoa taifa katika mtanziko wa kisiasa, uliohusisha matumizi ya nguvu za silaha, uharibifu wa mali za umma na binafsi. Wengine walifunguliwa mashitaka mahakamani.
Kongamano la ACT-Wazalendo lilihusisha wadau mbalimbali wakiwamo wanadiplomasia, viongozi wa vyama vya siasa na wahariri.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman maarufu kama OMO, ndiye aliyewasilisha mada kwenye kongamano lililofanyika leo Mei 16, 2026 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, akitoa mapendekezo ya namna ya kuliondoa taifa katika hali ya sasa ya kisiasa.
Alisisitiza umuhimu wa haki, uwazi na uwajibikaji kama msingi muhimu wa kufikia maridhiano ya kweli nchini.
Miongoni mwa hoja alizotoa OMO kuhusu kulikwamua taifa, ni kuanza kwa kutafuta ukweli, haki na uwajibikaji kuhusu madhara ya uchaguzi wa 2025 ili kurejesha imani ya wananchi.
Pia, amepemdekeza ufanyike uchunguzi huru, wahusika wawajibishwe na waathirika wapate haki zao.
Ametaka iundwe Tume ya Kudumu ya Maridhiano, Haki na Utengamano wa Taifa kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
OMO amesisitiza mfumo wa uongozi, usalama na utumishi wa umma ufanyiwe mageuzi makubwa kwa kuandikwa Katiba mpya kupitia mchakato shirikishi unaojumuisha wananchi wote.
Amependekeza sheria kandamizi zifutwe au zirekebishwe, huku vyombo vya dola na utumishi wa umma vikiondolewa katika ushawishi wa kisiasa.
Pia, Tume Huru ya Uchaguzi iundwe ili kuhakikisha kuna uchaguzi huru na wa haki unaorejesha thamani ya kura ya mwananchi.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la wadau wa demokrasia nchini lililofanyika leo jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
“Wanaoweza kuifurahia hali hii ni mafisadi wachache wanaonufaika na mpasuko wa kitaifa unaozalisha kutokuwepo kwa uwajibikaji.
Katika kukabiliana na hali hiyo, amesema huwezi kuwa na maridhiano bila ukweli, haki na uwajibikaji.
“Kwa pande zote mbili za Muungano kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar, marais wamenyoosha kile kinachoitwa “mkono wa maridhiano,” Hata hivyo, ACT Wazalendo tumetafakari kwa kina na tumejiuliza swali moja muhimu; tunaridhianaje katika hali tuliyo nayo?
“Maridhiano yanaanzaje katika hali ambayo makumi ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati wapo magerezani na mamia hawajulikani walipo?
Amesema kwa Wazanzibari, watawaeleza vipi lugha ya maridhiano bila kwanza kuonyesha nia ya dhati ya utekelezaji wa hoja ambazo Wazanzibari wamekuwa wakizidai miaka nenda miaka rudi.
Pia, OMO ametaka vyombo vya habari vya umma vitende haki kwa vyama vyote vya siasa, huku elimu ya uraia ikitolewa ili kujenga demokrasia ya kweli na mwafaka endelevu wa kitaifa.
Wakati OMO akisema hayo, kada wa CCM, Ezekiah Wenje, kwa upande wake kwenye kongamano la Tahliso lililofanyika Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, amesema mazungumzo ndiyo njia pekee itakayoliwezesha taifa kutoka katika mikwamo ya kisiasa iliyopo nchini.
Kwa mujibu wa Wenje ambaye kabla ya kuhamia CCM alikuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, amesema kiongozi yeyote wa kisiasa anayepinga maridhiano anaonyesha kutokuwa na mapenzi ya dhati kwa taifa na mustakabali wa wananchi wake.
Amesema ni vigumu kupata suluhu ya mikwamo yote ya kisiasa pasi na watu kukaa meza moja kuzungumza.
Mbali na Wenje, Mwanazuoni mkongwe Profesa Issa Shivji, akizungumza kwenye kongamano la ACT-Wazalendo amesema upo umuhimu wa kurejeshwa kwa utamaduni wa uwajibikaji nchini, akieleza kuwa ndio msingi unaounganisha amani na haki katika jamii.
Profesa Shivji amesema amani bila haki ni ya muda mfupi na mara nyingi huzaa migogoro ya baadaye.
Nguli huyo wa sheria amesema kuwa bila uwajibikaji wa kweli, ni vigumu kupata amani ya kudumu inayotokana na haki.
Profesa Shivji amesema kwa sasa uwajibikaji unaonekana kupungua au kutotekelezwa kwa kiwango kilichokuwa kikishuhudiwa awali, hali inayoleta changamoto katika kujenga imani ya wananchi.
“Kiungo kati ya amani na haki ni uwajibikaji, bila uwajibikaji huwezi kuwa na haki na bila haki huwezi kuwa na amani. Hatuwezi kupiga hatua yoyote ile bila uwajibikaji, nchi hii kuna utamaduni wa watu kuwajibisha yanapotokea matukio makubwa,” amesema.
Akirejea baadhi ya matukio ya kihistoria nchini, amesema katika awamu nne zilizopita Serikali ilikuwa ikichukua hatua za uwajibikaji pale makosa au ukatili ulipotokea katika vipindi tofauti.
Mwanazuoni huyo ametaja miongoni mwa matukio hayo ni mauji ya vikongwe yaliyotokea wakati wa utawala wa awamu ya kwanza iliyoongozwa na Mwalimu Julius Nyerere ambapo viongozi waliwajibika kwa ukati uliofanyika wakati wa kufuatilia mauaji hayo.
Amesema katika Awamu ya Pili chini ya Ali Hassan Mwinyi, amekumbusha tukio la mauaji ya wafanyakazi katika shamba la sukari la Kilombero yaliyohusishwa na kikosi cha FFU, ambapo tume ya uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Chipeta iliundwa na ripoti yake kutolewa, kisha hatua kuchukuliwa.
Kwenye Awamu ya Tatu ya iliyoongozwa na Benjamin Mkapa, amegusia ghasia za Pemba wakati wa uchaguzi wa mwaka 2000, ambapo Tume ya Hashim Mbita iliundwa kuchunguza matukio hayo.
Amesema wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Jakaya Kikwete, matukio ya mauaji ya wafanyabiashara wa Morogoro yaliyofanywa na Polisi pamoja na matukio ya ukatili katika hifadhi za taifa, alibainisha baadhi ya hatua zilichukuliwa ikiwemo kujiuzulu kwa waziri wa wakati huo.
Kuhusu mapendekezo ya kuiponya nchi, Profesa Shivji amesema hayapaswi kubaki kwa wataalamu pekee walioko maofisini, bali yanapaswa kutoka katika mijadala ya wananchi wenyewe.
“Ninachotaka mimi mapendekezo yatokane na mijadala… wananchi si wajinga, wakipata nafasi wataongea.
“Othman amesema nchi yetu iko njiapanda, labda niongeze inateleza na hatujui itaangukia wapi, ndiyo maana kuna umuhmu wa kuwa na mijadala ya aina hii, tusipuuze umuhimu wa watu kutoa mawazo yao, kukosa nafasi ya kutoa mawazo ni kitu hatari sana,” amesisitiza.
Kufuatia hilo Profesa Shivji amewahimiza vijana kujenga utamaduni wa kusoma ripoti mbalimbali za uchunguzi na hukumu za mahakama ili kuelewa kwa kina masuala ya haki na uwajibikaji.
Amesema kupitia uelewa huo, vijana wataweza kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kitaifa inayolenga kuimarisha uwajibikaji na haki.
“Suluhu ya kudumu kwa changamoto za kijamii na kisiasa itapatikana kupitia mijadala ya wazi na shirikishi, si maamuzi ya juu pekee,” amesema Profesa Shivji.
Akizungumza kwenye mjadala huo Mwenyekiti wa Kamati maalumu ya Maaskofu na Masheikh ya Haki, Amani na Maadili Tanzania Askofu William Mwamalanga ametoa wito kwa viongozi wa kitaifa na wananchi kurejea katika misingi ya haki, maadili na hofu ya Mungu ili kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili na umwagaji damu nchini.
Amesema taifa haliwezi kuwa na amani ya kweli bila kusimamia haki kwa vitendo, akisisitiza kuwa haki ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya jamii yoyote.
“Jamii haiwezi kujenga uwajibikaji wa kweli ikiwa haina hofu ya Mungu na uelewa wa mema na mabaya. Bila haki na hofu ya Mungu, juhudi za Serikali, kamati au tume mbalimbali za kushughulikia matatizo ya kijamii zinaweza kushindwa kufikia malengo, kwani uovu utaendelea kushika kasi ndani ya jamii,” amesema.
Kwa upande wake Kada wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Catherine Ruge akizungumza kwenye kongamano la ACT-Wazalendo amesema yaliyotokea Oktoba 29, 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu yamerudisha nyuma jitihada za wanawake kushiriki katika siasa, uongozi, uchumi na maendeleo ya Taifa.
Amesema hakuna mama anayeweza kutoa sadaka maisha yake au ya watoto wake kwa jambo lolote, hivyo wanawake waliokuwa na ndoto ya kuwa viongozi wamerudi nyuma kutokana na woga na hofu kwa yaliyotokea Oktoba 29.
“Ukiangalia matukio ya Oktoba 29, 2025 unaona vijana, hii maana yake ni nini …? vijana wanataka sauti zao zisikike ndio maana wamejitokeza, lakini wale wanawake wachache tuliowaona wanataka nafasi salama za kufanya siasa,” amesema.
Amesema kilichotokea ilikuwa kuonyesha Serikali ishara kwamba wanawake wanataka nafasi salama ya kufanya siasa.
Kwa upande wake Kiongozi Mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameungana na wazungumzaji wengine kuhusu uwajibikaji kwamba bila uwajibikaji hakuna ambacho kitaweza kwenda mbele nchini.
“Kama hatutaondoa vyombo vya usalama kwenye siasa zetu tutaendelea kuwa hapa tulipo, lazima tuwe na vita ya kupambana bila ya kuchoka kutenganisha vyombo vya ulinzi na siasa tukifanikiwa hilo hatutakuwa na shida,” amesema.
Kwa upande Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu aliyekuwa mgeni mwalikwa kwenye kongamano la ACT-Wazalendo amesema changamoto kubwa iliyopo sasa ni kushindana kwa maneno, kubadilishana majukwaa na kuonyeshana ukweli wa kusema kuliko utoaji wa majawabu.
Amesema watu wameshindwa kugusa kiini cha namna ya kutoka katika mkwamo uliopo nchini.
“Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman amesema kitu hapa, pengine tukiacha jambo hilo hapa tukaendeleza umahiri wa kuandika kupitia mtandao wa X kwenye makundi ya WhatsApp bado hatutatoka hapa tulipo,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amesema hakuna wanaopingana ni namna gani yametokea matukio ya Oktoba 29 wakati wa Uchaguzi Mkuu, akidokeza uwepo wa uonevu, uvunjaji wa haki, dharau kiburi, umasikini na ajira kwa vijana.
Ametaja pia suala la uwepo wa sheria kandamizi, Katiba mpya, haki, ukweli, uwajibikaji na maridhiano na yote hayo yamekuwa ndio mjadala mkubwa.
“Hakuna mtu ambaye hakiri uwepo wa mauaji nchini, uwepo wa tatizo la ajira kwa vijana na umasikini wa kipato kwa Watanzania na uonevu, hayupo, tunashindana kwenye mchakato, sasa kwenye mchakato wapo wanaotaka kubaki na vinyongo vyao na malengo yao,” amesema.
Mwalimu amemwomba OMO kwenda kuanzisha kamati ya kukwamua Taifa hapa lilipo na alifanye jukumu hilo kama kiongozi mwandamizi na wote watakuwa tayari kumuunga mkono.
“Tunazungumza upande wa pili wa uwajibikaji ni sawa, je sisi tunawajibikaje kwa roho za watu, hasara za watu, ulemavu wa watu…tunautaka ukweli tutaupata wapi?” amehoji.
Wakati wazungumzaji kwenye kongamano la ACT-Wazalendo wakisema hayo, mzungumzaji mwingine kwenye kongamano la Tahliso, Profesa Palamagamba Kabudi, waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, amesema yaliyotokea Oktoba 29, 2025 hayakuwa mambo ya kawaida na hayafanani na Taifa la Tanzania.
Profesa Kabudi, amesema ni vema kama Taifa kukubaliana kwamba yasitokee tena, kauli ambayo imetumika na mataifa mbalimbali yalipokumbwa na mambo yasiyo ya kawaida.
“Zipo nchi, zilikumbwa na misukosuko, tufani na baadaye zikasema never again what happened yesterday. Mmechukua kaulimbiu inayoashiria kwamba kuna lililotokea si la kawaida, halifanani na nchi yetu na limetutikisa,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa nasaha kwa vijana kwamba wasiharibu maisha yao kwa siasa na propaganda za chuki, badala yake wajikite katika jitihada za kujiendeleza kwa kuwa ndio siri pekee ya mafanikio katika maisha yao.
“Pamoja na kupata elimu mnayoipata leo, mchawi wa kweli ni kujimudu kimaisha na namna pekee ya kujimudu kimaisha ni kuyatafsiri maisha kwa namna ya kipekee,” amesema.
Imeandikwa na Elizabeth Edrwad, Aurea Simtowe, Juma Issihaka na Baraka Loshilaa.
