Maajabu ya mabao 11 ya Fei TotoMaajabu ya mabao 11 ya Fei Toto

KIUNGO mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji hatari zaidi kwa sasa Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025/26, huku akionekana kubadilika kiuchezaji kutoka mchezaji wa pasi na mashuti ya mbali hadi kuwa tishio ndani ya eneo la hatari.

Licha ya kujulikana kwa uwezo wake wa kupiga mashuti na pasi za mbali zinazovunja safu za ulinzi, Feisal msimu huu ameonyesha uwezo mkubwa zaidi kwenye kumalizia nafasi karibu na goli, jambo lililomfanya aonekane tofauti zaidi katika mfumo wa Azam.

Takwimu zinaonyesha kuwa mabao yake yote 11 ya ligi ambayo yamemfanya kuwa kinara kwa wafungaji, ameyafunga akiwa ndani ya boxi, akionyesha uelewa wa kukaa katika nafasi na uwezo wa kusoma mwelekeo wa mpira.

Katika mfumo wa sasa chini kocha Florent Ibenge ambaye anaonekana kubebeshwa zigo la mabao, Feisal hucheza kati ya viungo lakini huingia kwenye eneo la hatari kama mshambuliaji wa pili, hali inayompa nafasi ya kupokea mipira ya mwisho na kumalizia.

Utofauti wake mkubwa msimu huu unaonekana kwenye aina ya mabao aliyofunga, ambapo amefunga kwa kichwa (4), mguu wa kulia (sita) na mguu wa kushoto (1), akionyesha kuwa ni mchezaji asiye na mguu dhaifu katika kumalizia nafasi.

Aidha, uwezo wake wa kutumia mipira ya juu umeonekana wazi baada ya kufunga mabao manne kwa kichwa kwa mguu wa kulia, Feisal amefunga jumla ya mabao  sita kati ya hayo mawili ni kwa penalti.

Kwa mguu wa kushoto pia ameonesha uwezo wa kumalizia nafasi, akifunga bao muhimu dhidi ya Singida Black Stars ikiwa ni bao la ushindi wakati Azam ikiwatandika wenyeji wao mabao 2-1.

Miongoni mwa mabao yake ya kukumbukwa ni lile la dakika ya 90 dhidi ya Pamba Mei 14, alipofunga kwa kichwa akimalizia kona ya Iddi Seleman ‘Nado’ ulikuwa ni wakati ambao Azam ilihitaji bao kabla ya Japhet Kitambala kufunga la pili katika dakika ya  90+4’.

Dhidi ya Namungo, alifunga kwa penalti dakika ya 42, akionesha utulivu mkubwa katika mchezo huo na bao lake ndio liliamua matokeo.

Katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, alifunga mabao mawili, moja kwa kichwa na lingine kwa mguu wa kulia.

Bao pekee la mguu wa kushoto, Feisal alifunga Aprili Mosi, 2026 dhidi ya Singida Black Stars, akimalizia asisti ya Nado.

Kwa upande wa Dodoma Jiji, Mei 11, 2026 alifunga mapema dakika ya 12 kwa mguu wa kulia, akimalizia pasi ya Zidane Sereri.

Kwa ujumla, msimu huu Feisal ameonesha mabadiliko ya kimkakati kutoka mchezaji anayejulikana zaidi kwa mashuti ya mbali, hadi kiungo mshambuliaji hatari zaidi ndani ya boxi na ikumbukwe kuwa msimu uliopita ndiye aliyekuwa kinara wa asisti akitoa 13 huku akifunga mabao manne tu, hali hii inamfanya kuwa mchezaji wa kipekee Azam huku mchango wake ukiendelea kuwa muhimu katika vita ya timu hiyo kusaka nafasi ya kimataifa msimu ujao.

Katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara ambazo Feisal amefunga msimu wa 2025/26, Azam imekuwa na matokeo chanya zaidi kwani imeshinda mechi nane na kutoka sare mbili huku ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja katika mechi alizopachika mabao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *