Dk Mwigulu: Sheria ya Kutaifisha kufutwaDk Mwigulu: Sheria ya Kutaifisha kufutwa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema Sheria ya Kutaifisha inakwenda kufutwa kwa kuwa, imeshaanza kutumiwa kama kichaka.

Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Mei 17, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, eneo la Kambi ya Nyasa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi.

Msingi wa kuyasema hayo unatokana na kitendo cha kukamata na kutaifishwa kwa mali na vitendea kazi vya wananachi hali inayokwamisha uzaishaji na utendaji kazi kwa watu waliojiajiri.

“Niwape taarifa njema, Rais ameshaelekeza hiyo Sheria ya Kutaifisha tunakwenda kuifuta, imeshaanza kuwa kichaka na ameshatoa barua nimeipokea inayoelekeza hiyo sheria kufutwa,” amesema.

Wakati anasema hayo, alikuwa ameshikilia nakala za kero za watu zinazoelezea migogoro ya ardhi, watu kunyang’anywa mashamba na mali zao, huku akiendelea kusikiliza migogoro hiyo kutoka kwa wananchi moja kwa moja.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, akizungumza na  Mursali Mustafa Issa ambaye ni mlemavu wa viungo katika Uwanja wa shule ya msingiKambi ya Nyasa, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma leo Mei 17, 2026 alipokuwa akifanya Mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya hiyo. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Dk Mwigulu amesema mambo ya kukamata kamata, kushikilia mali na vitendea kazi vya watu, yanapaswa kuachwa  kwasababu yanakwamisha juhudi za maendeleo ya kiuchumi.

“Si tu kamata kamata ya wananchi wenyewe hata kukamata vitendea kazi, unakuta jambo linahitaji tu faini nyie mnakamata kitendea kazi. Unakuta kijana anafanya shughuli yake ya bodaboda, baiskeli au gari ndio amefanya kosa, unashikiliaje bodaboda! Imekuwa ya kwenu? Si mnadai faini kama sheria inavyosema?

“Andikisheni kitambulisho chake, andikeni faini yake mwachieni akaendelee na shughuli yake,’’ amesema.

Amesema kwa watu waliopo serikalini, wanaweza kuwa na uhakika kwa kuwa Serikali haifilisiki, lakini kwa waliojiajiri asipofanya kazi familia nzima inasimama na ukichukua kitendea kazi chake, umeua mtaji na maisha ya familia nzima.

“Unakuta anadaiwa na marejesho, hapa unakuwa umeua na nyumba yake. Niliwahi kwenda Mvumi nikakuta wameshilikia gari ya thamani ya Sh25 milioni kwa deni la Sh700,000 kwa miaka saba.

“Haya mambo ya kukamata kamata na kushikilia vitendea kazi vya watu tuachane nayo. Kama unataka mtu azalishe wewe unakamata kitendea kazi atalipaje?” amehoji.

“Jana nilipita Kondoa nikakuta wamemtuhumu mwizi wamechukua mashine yake ya kusaga hadi kitanda na godoro, sasa wamezoea mimi nimekuja nitawashikisha adabu wote wasio nadabu,” amesema.

Amesema kamata kamata isiyo na msingi ni mambo ya zamani huku akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kuhakikisha anasimamia kulikomesha hilo ili watu waishi wakiwa huru.

Amesema ili kupiga hatua kwa kasi kila mmoja anapaswa kuwajibika kuanzia serikalini hadi sekta binafsi ili kila mmoja apate haki yake.

Mradi wa maji ukamamilike

Awali, alipotembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Chemba unaotekelezwa kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Chemba, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

“Wilaya ya Chemba ni moja ya wilaya zenye shida ya ukame na maji, lakini pia ni wilaya za uzalishaji, kwa hiyo tunahitaji sana mradi huu ukamilike haraka,” alisema.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, akizungumza na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kondoa Mjini, Jimbo la Kondoa, Dayosisi ya Dodoma leo Mei 17, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji kutoka Wizara ya Maji, Charles Mafie amesema mradi huo wenye thamani ya Sh11 bilioni unatarajiwa kuhudumia wananchi 18,141 wa Mji wa Chemba pamoja na vijiji vya Chemba, Chambalo, Kambi ya Nyasa, Gwandi, Paranga na Makamaka.

Amesema mradi huo umefikia asilimia 76 ya utekelezaji na unahusisha ujenzi wa visima vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita 207,000 kwa saa, matenki ya kuhifadhi maji, kituo cha kusukuma maji pamoja na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji yenye urefu wa kilomita 60.

Aidha, amesema mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 37 ya sasa hadi asilimia 100 na kuongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita 170,000 kwa siku hadi kufikia zaidi ya lita milioni tatu kwa siku.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi M/s Megha Engineering and Infrastructure Limited (MEIL) chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri WAPCOS Limited.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka makandarasi wanaotekeleza mradi huo kuhakikisha wanawalipa kwa wakati vijana, mafundi na vibarua wanaoshiriki katika utekelezaji wa kazi kupitia mikataba ya ushirikiano (subcontracting).

“Muendelee na kazi, lakini kila mnapopata fedha za mradi hakikisheni mnawalipa wanaofanya kazi pamoja nanyi. Vijana wetu waliopata subcontracting, mafundi na vibarua wote wapate malipo yao kwa wakati,” amesema.

Pia, amesema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko katika baadhi ya maeneo kuhusu miradi kukamilika huku baadhi ya watu waliohusika katika utekelezaji wake wakibaki wanadai malipo yao jambo ambalo halikubaliki.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema ana imani kubwa na usimamizi wa viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo akieleza kuwa, usimamizi madhubuti una mchango mkubwa katika kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo chanya kwa wananchi.

Akizungumzia hilo, Wakili wa kujitegemea, Dk Khamis Masoud kutoka Everlasting Legal Aid Foundation jijini Dar es Salaam, amesema mambo yote ya utaifishwaji yalikuwa katika Azimio la Arusha.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, akizungumza na wananchi waliojitokeza katika mkutano wake wa hadhara alioufanya katika Uwanja wa shule ya msingiKambi ya Nyasa, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma leo  Mei 17, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Amesema tatizo sio sheria kufutwa, kwa kuwa Tanzania kuna sheria nyingi nzuri, shida inaanzia kwa wasimamizi kuitumia kama fimbo ya kuwachapa wenye haki na wanyonge kwa masilahi yao binafsi.

“Kufuta sheria bado tunaweza kutengeneza tatizo kwa jamii, Serikali inatakiwa kuangalia maadili ya viongozi wake, je inatumika sawa sawa. Mfano mtu ameiba ili kuthibitisha lazima mali zikamatwe zioneshwe; huo ni mchakato wa kisheria na hauna tatizo.

“Inatakiwa tuiboreshe kuhakikisha haitoi mwanya kwa maofisa wenye visa vyao, binafsi wasiitumie vibaya sheria hiyo kuonea watu. Sheria imenyooka ila watu wanavyoitumia ni tatizo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *