Kigogo Yanga ataja hesabu mpya za ubingwaKigogo Yanga ataja hesabu mpya za ubingwa

MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo amesema kupoteza mechi moja hakuwezi kuiondoa timu hiyo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na  malengo yao makubwa bado ni kutwaa taji hilo msimu huu huku kukiwa na hesabu mpya za kufanikisha hilo.

Ikumbukwe kuwa, Yanga ilifungwa mabao 3-2 na Dodoma Jiji ugenini, ikiwa ni mechi ya kwanza kwa kikosi hicho kupoteza msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara na ni mara kwanza Dodoma Jiji kushinda dhidi yao.

Matokeo hayo yakapunguza gepu la pointi kutoka tano hadi mbili na kufanya mbio za ubingwa baina ya Yanga inayoongoza msimamo na Simba iliyopo nafasi ya pili kushika kasi zaidi huku zikibaki mechi saba kumaliza msimu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gumbo aliweka wazi kuwa, ndani ya klabu hiyo hakuna hofu wala presha ya kukata tamaa kutokana na uzoefu mkubwa walionao kwenye mbio za ubingwa misimu ya hivi karibuni.

Gumbo amesema, Yanga imepitia nyakati nyingi ngumu kwenye ligi lakini imekuwa ikipewa nguvu na uwezo wa kupambana hadi dakika za mwisho, jambo ambalo linaifanya timu hiyo kuendelea kuamini inaweza kufikia malengo yake msimu huu.

“Sio kitu kipya kwetu kupoteza mchezo, mpira una matokeo ya aina yoyote, lakini hayo hayawezi kututoa kwenye malengo yetu ya kuchukua ubingwa msimu huu,” amesema Gumbo.

Amesema kilichobaki kwa sasa ni uongozi kukaa pamoja na benchi la ufundi sambamba na wachezaji ili kufanya tathmini ya haraka kuelekea michezo saba iliyosalia ambayo anaamini ndiyo itaamua hatma ya ubingwa wa msimu huu.

“Tutakaa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi kuweka sawa mikakati yetu kwenye hizi mechi saba zilizobaki. Tunajua ushindani ni mkubwa lakini Yanga ni timu yenye uzoefu wa kupambana kwenye mazingira kama haya,” amesema.

Kiongozi huyo amesema ndani ya Yanga hakuna anayefikiria kitu kingine zaidi ya ubingwa kwani hilo ndiyo jambo pekee ambalo mashabiki, viongozi pamoja na wadhamini wanahitaji kuona mwishoni mwa msimu.

“Hakuna kitu mfadhili wetu anataka kusikia zaidi ya ubingwa, hata sisi viongozi ndio jambo letu kubwa kwa sasa kuhakikisha tunamaliza ligi tukiwa mabingwa,” amesema Gumbo.

Katika misimu ya karibuni, Yanga imejijengea rekodi ya kuwa timu ya mafanikio makubwa ndani ya soka la Tanzania baada ya kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB kwa misimu minne mfululizo.

Tayari timu hiyo imefuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ikibakisha hatua chache kwenda kutetea taji lake, huku pia ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 54 ikishuka dimbani mara 23, imebakiwa na mechi saba katika hesabu za kuwa bingwa tena kwa mara ya tano mfululizo.

Katika mechi saba zilizobaki, Yanga ina kazi kubwa ya kufanya kwani inakutana na Azam inayoshika nafasi ya tatu, Singida Black Stars (nafasi ya nne) na JKT Tanzania (nafasi ya tano) na TRA United (nafasi ya sita), ambapo zote hizo zinapambana kumaliza ndani ya nne bora ili kuingia kwenye uwezekano wa kushiriki kimataifa msimu ujao.

Mechi zingine ni dhidi ya timu zinazopambana zisikae kwenye hatari ya kushuka daraja ambazo ni Namungo, Mashujaa, Fountain Gate.

Mechi hizo saba zilizobaki, Yanga itacheza nne nyumbani dhidi ya Singida Black Stars, Namungo, Azam na TRA United, huku za ugenini ni dhidi ya Mashujaa, Fountain Gate na JKT Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *