Che Malone ataja siri ubingwa CAFChe Malone ataja siri ubingwa CAF

BEKI wa zamani wa Simba, Che Malone Fondoh ametaja siri iliyowapa ubingwa USM Alger baada ya kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika kwa mikwaju ya penalti 8-7 dhidi ya Zamalek katika fainali iliyopigwa Mei 16, 2026 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo nchini Misri.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Mcameroon huyo kucheza fainali ya michuano hiyo, msimu uliopita alipoteza akiwa na Simba kufuatia kufungwa kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane.

CHE 01

Katika mechi ya kwanza ambayo ilipigwa Morocco, Simba ilifungwa mabao 2-0 kabla ya kutoa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambapo ilipigwa fainali hiyo ya pili.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya fainali hiyo ya pili mfululizo, Che Malone aliyetua USM Alger msimu huu akitokea Simba, amesema msingi mkubwa wa mafanikio yao ulikuwa nidhamu na maandalizi ya muda mrefu, hasa kuelekea mchezo mgumu wa fainali.

CHE 02

“Siri kubwa ya ubingwa huu ni maandalizi yetu. Tulijua kabisa mechi itakuwa ngumu na inaweza kuamuliwa kwa penalti,” amesema beki huyo aliyecheza mechi zote 14 za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Katika mechi hiyo ya fainali, Zamalek ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la mapema dakika ya tano kupitia penalti ya Oday Al-Dabbagh, baada ya Adam Kayed kufanyiwa madhambi ndani ya boksi na Che Malone. Bao hilo lilifanya mzani kuwa sawa kutokana na mechi ya kwanza USM Alger kushinda 1-0 nyumbani kwao Algeria.

CHE 03

Baada ya dakika 90 za mchezo huo Zamalek ikitoka na ushindi wa 1-0 ikifanya matokeo ya jumla kuwa 1-1, hatima ya ubingwa iliamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Che  Malone amesema walikuwa tayari kiakili kwa changamoto hiyo.

Katika mikwaju hiyo, timu zote zilifunga penalti saba za mwanzo, kabla ya Mohamed Shehata wa Zamalek kukosa huku USM Alger ikitumia vizuri nafasi hiyo kupitia kwa Glody Likonza  na kufunga penalti ya ushindi ikiwapa Waalgeria hao taji la pili la Kombe la Shirikisho baada ya lile la mwaka 2023 ilipoifunga Yanga.

CHE 04

Ushindi huo pia umeihakikishia USM Alger nafasi ya kucheza Super Cup ya CAF dhidi ya mshindi kati ya Mamelodi Sundowns au FAR Rabat, sambamba na zawadi ya rekodi ya dola 4 milioni ambazo ni zaidi ya Sh10.7 bilioni za Kitanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *