Dar es Salaam. Ndani ya Bongofleva kumewahi kujitokeza makundi mengi ya marapa na baadaye kupotea, mojawapo ni OMG ambao walisifika kwa mtindo wao wa kisasa katika uchanaji.
Hata hivyo, kundi hili halikufika mbali baada ya lebo iliyokuwa ikiwasimamia kusitisha mikataba yao. Je OMG ni kina nani hasa? Fahamu zaidi.
1. Kundi la OMG linaundwa na rapa watatu, Young Lunya, Salmin Swaggz na Conboi Cannabino ambaye alikuja kuvuma zaidi kupitia ngoma yake, Till I Die (2020) huku remix yake akisikika Khaligraph Jones kutokea Kenya.
2. Rapa Quick Rocka aliyetoka na ngoma yake, Bullet (2010), ndiye aliwapa OMG (Ooh My God) jina hilo baada ya kuona uwezo wao ni mkubwa upande wa kuchana hasa miondoko ya trap.
3. Awali, Quick Rocka alimpa Young Lunya jina hilo la OMG ila rapa huyo hakuwa tayari kulitumia ndipo likageuka kuwa la kundi lao. Young Lunya alijiunga na OMG baada ya kuondoka katika kituo cha Mkubwa na Wanawe kilichowatoa wakali kibao Bongo kama Aslay na Mbosso.
4. Boss wao, Quick Rocka naye aliwahi kuwa ndani ya kundi kama OMG, kundi lake lilifahamika kama Rockaz ambapo alikuwepo yeye na wenzake watatu – Chief Rocka, Dau Rocka na Mo Rocka.
5. Na OMG ndio wasanii wa kwanza kusainiwa katika lebo ya Quick Rocka, Switch Music Group (SMG), ambapo walisaini kama kundi, kisha mmoja mmoja kama msanii wa kujitengenezea.
6. Studio kwa Quick Rocka, OMG walimkuta mtayarishaji muziki Luffa ambaye alitengeneza wimbo wao uliotambulisha kwa mara ya kwanza, Fit (2016). Vilevile Luffa ndiye aliyemtambulisha Young Lunya kwa Quck Rocka hadi kuja kuanzishwa kwa kundi la OMG.
7. OMG walikuja kufanya vizuri zaidi kupitia ngoma yao, Uongo na Umbea (2017) wakimshirikisha Barakah The Prince, mwimbaji aliyetoka chini ya Tetemesha Records.
8. Ngoma yao, Uongo na Umbea (2017) ilifanya vizuri hadi kuvunja rekodi ya mauzo kupitia mtandao wa Wasafi.com kufuatia kupata wasikilizaji (downloads & streams) wengi zaidi ndani ya kipindi kifupi.
9. Rosa Ree ndiye msanii wa kwanza wa kike kushirikishwa na OMG, ambapo alisikika katika wimbo wao, Wanangu na Wanao (2018) uliotengenezwa na S2kizzy kipindi akiwa Switch.
10. Ndani ya Switch, OMG walifanya kazi na watayarishaji muziki mbalimbali akiwemo Nahreel, ingawa alikuja kuondoka na kwenda kuanzisha studio yake, The Industry, ambayo pia ilikuwa na lebo ndani yake. Wengine ni Luffa ambaye alikuja kuhamia Wanene Studio ingawa baadaye alirejea Switch na pia S2kizzy aliyekuja kufungua studio yake, Pluto Republic, inayofanya vizuri kwa sasa.
