
Nairobi. Maelfu ya wananchi nchini Kenya wamejikuta wakikwama katika vituo mbalimbali vya usafiri baada ya madereva wa daladala, maarufu matatu kuanza mgomo kupinga kupanda kwa bei ya mafuta, hatua iliyosababisha miji mikuu na maeneo ya pembezoni kutatizika kwa usafiri.
Mgomo huo umeanza leo Jumatatu Mei 18, 2026 umeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kawaida katika maeneo mengi ikiwamo jijini Nairobi, Kitengela, Kisii na maeneo jirani, ambapo wananchi wengi walilazimika kutembea kwa miguu baada ya kukosa magari ya kuwafikisha kazini na kwenye shughuli zao za kila siku.
Waendesha matatu wamesema wamechukua hatua hiyo baada ya serikali kutangaza ongezeko jipya la bei ya mafuta, wakidai kuwa gharama za uendeshaji zimepanda na kupunguza faida yao kwa kiasi kikubwa.
Viwango vipya vya mafuta nchini Kenya vinaonyesha petroli ikiuzwa kwa KSh214.25 (takriban Sh4,307), dizeli KSh242.92 (takriban Sh4,883) na mafuta ya taa KSh152.78 (takriban Sh3,071) kwa lita.
Kutokana na hali hiyo, madereva binafsi pamoja na waendesha bodaboda wameongeza nauli kwa viwango vikubwa, hali iliyowaongezea mzigo wananchi ambao baadhi yao walilazimika kufunga barabara na kuchoma matairi katika maeneo mbalimbali ya mijini.
Katika baadhi ya maeneo ya Nairobi, abiria walionekana wakitembea umbali mrefu huku wengine wakisubiri kwa saa kadhaa kupata usafiri mbadala, hali iliyoathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aidha, baadhi ya shule jijini Nairobi na vitongoji vyake zimeahirisha masomo kwa siku moja kutokana na usumbufu wa usafiri, zikisema usalama wa wanafunzi ndio sababu kuu ya hatua hiyo.
Shule hizo zimewataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanasalia nyumbani wakiangalia hali itakavyokuwa.
Wakati huohuo, ujumbe unaosambaa mitandaoni kuhusu mgomo huo umeongeza hofu kwa wazazi, wengi wakihofia usalama wa watoto wao wanaotegemea usafiri wa umma.
