Yusuf Chippo arejeshwa Mtibwa SugarYusuf Chippo arejeshwa Mtibwa Sugar

UONGOZI wa Mtibwa Sugar umemrejesha kikosini kocha mkuu wa timu hiyo, Mkenya, Yusuf Chippo baada ya kumweka pembeni tangu Mei 6, 2026, kutokana na mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-2026.

Chippo aliwekwa pembeni muda mfupi timu hiyo ilipochapwa bao 1-0 na Dodoma Jiji, Mei 6, 2026, baada ya kufikisha mechi tisa mfululizo za Ligi Kuu bila ushindi, tangu mara ya mwisho Februari 2, 2026 ilipoifunga Tanzania Prisons 2-1.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chippo amesema kwa sasa amerejea kazini kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake na anashukuru uongozi kwa imani kubwa waliyompa tena, licha ya hivi karibuni kupitia kipindi kigumu cha mwenendo mbaya kikosini humo.

“Ni kweli baada ya mechi yetu na Dodoma Jiji niliwekwa pembeni na sikuwa sehemu ya msafara wa timu iliyoenda Singida kwa ajili ya kucheza dhidi ya Singida Black Stars, kwa sasa kila kitu kinaendelea vizuri na nimerudi upya,” amesema Chippo.

Chippo aliyeachana na Murang’a SEAL ya kwao Kenya tangu Agosti 21, 2025, alijiunga na Mtibwa Novemba 17, 2025, ili kuiongoza akishirikiana na Kocha Msaidizi, Awadh Juma ‘Maniche’ aliyeipandisha Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025.

Tangu Chippo alipojiunga na timu hiyo Novemba 17, 2025, amekiongoza kikosi hicho katika mechi 16, za Ligi Kuu Bara hadi sasa, akishinda nne, sare sita na kupoteza sita huku kati ya hizo Mtibwa imefunga mabao 14 na kuruhusu 22.

Hadi sasa Mtibwa imecheza mechi 23 za Ligi Kuu Bara, ikishinda sita, sare nane na kupoteza tisa, ikifunga mabao 20 na kuruhusu 32, ikiwa nafasi ya 10 na pointi 26.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *