
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume ya uchunguzi wa kijinai wa matukio ya ghasia ya wakati na baada ya uchaguzi wa 2025, huku akimteua Jaji Shaban Lila kuwa Kamishna na Mwenyekiti wake.
Uamuzi wa kuundwa kwa tume hiyo, ni utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya uchunguzi wa matukio hayo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande, iliyotaka uchunguzi wa kijinai ufanywe na tume maalumu ya kijinai.
Katika pendekezo hilo, Jaji Chande alisema tume hiyo itakuwa na jukumu la kupeleleza na kufuatilia masuala mahsusi yanayohitaji upelelezi zaidi ili kushughulikia tuhuma zilizobainishwa katika taarifa ya Tume.
”Masuala hayo ni pamoja na kubaini wahusika wakuu wa ghasia, matukio tatanishi ya vifo na majeruhi, maiti ambazo hazijapatikana, na kupendekeza hatua za uwajibikaji,” alisema Aprili 23, 2026 alipokabidhi ripoti kwa Rais Samia.
Taarifa ya kuundwa kwa Tume hiyo ya kijinai, imetolewa leo Jumatatu Mei 18, 2026 na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.
Uundwaji wa Tume hiyo, taarifa inasema umezingatia mamlaka aliyonayo Rais chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32.
Imewataja walioteuliwa ni Jaji Lila, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na atakuwa kamishna na mwenyekiti wake.
Wengine walioteuliwa kuwa makamishna wa tume hiyo ni Jaji mstaafu Gad Mjemmas, Jaji mstaafu Awadh Bawazir na Jaji mstaafu Aishieli Sumari, wote walikuwa Mahakama Kuu.
