Wadau wataka uimarishaji wa mfumo wa uanagenzi kuongeza ajira kwa vijanaWadau wataka uimarishaji wa mfumo wa uanagenzi kuongeza ajira kwa vijana

Morogoro. Wadau wa maendeleo ya ujuzi nchini wameitaka serikali na sekta binafsi kuimarisha mfumo wa uanagenzi ili kuongeza ajira kwa vijana, kwa kuzingatia mwongozo wa kimataifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 18, 2026 katika kikao kazi kilichoratibiwa na ILO kupitia programu ya Dunia ya Ujuzi kwa ufadhili wa Norway, kilicholenga kuthibitisha mpango wa utekelezaji wa mafunzo ya uanagenzi kilichofanyika mkoani Morogoro na kuwashirikisha wadau kutoka sekta ya elimu, vyuo vya ufundi, serikali na sekta binafsi.

Mshauri wa ukuzaji ujuzi kutoka ofisi ya ILO Pretoria, Albert Okal.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mshauri wa ukuzaji ujuzi kutoka ofisi ya ILO Pretoria, Albert Okal, amesema tathmini inaonyesha mfumo wa uanagenzi nchini bado haujafikia kiwango kinachotarajiwa na hivyo kuna haja ya maboresho ili kuendana na viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dk Bakari Ali Silima, amesema uanagenzi ni nyenzo muhimu inayowaandaa vijana kupata ajira kutokana na mafunzo yanayoendana na mahitaji halisi ya soko la kazi na viwanda.

Ameongeza kuwa taasisi za elimu zinapaswa kuimarisha mafunzo ya vitendo ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dk Bakari Ali Silima.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Daudi Simbeye, amesema serikali imejipanga kuimarisha mfumo huo kupitia programu mbalimbali za ukuzaji ujuzi, ikiwemo mpango wa Samia unaolenga kutambua na kuthibitisha ujuzi wa vijana waliopata maarifa katika sekta isiyo rasmi.

Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Daudi Simbeye.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Dennis Assey, amesema kupitia warsha hiyo ILO iliwasilisha ripoti ya tathmini ya mfumo wa uanagenzi nchini inayozingatia mapendekezo ya kimataifa ya ILO.

Amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuimarisha programu ya taifa ya ukuzaji ujuzi, ambapo zaidi ya vijana 5,000 tayari wananufaika na mafunzo ya uanagenzi katika vyuo 46 nchini.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Dennis Assey.

Assey ameongeza kuwa programu hiyo ni fursa muhimu kwa vijana nchini kujiandaa na soko la ajira na kujiajiri, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kuendelea kuchangamkia mafunzo hayo yanayotangazwa kila mwaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *