
Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepanga mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, baina ya Yanga na Azam FC kuchezwa Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba, Juni 21, 2026.
Taarifa iliyotolewa na TFF leo, Jumatatu, Mei 18, 2026 imefafanua kwamba mechi nyingine ya nusu fainali baina ya Simba na Coastal Union itachezwa Arusha, Juni 20, 2026 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Yanga imetinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo baada ya kuitupa nje JKT Tanzania kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 juzi.
Azam imeingia hatua ya nusu fainali baada ya jana kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Coastal Union yenyewe imeingia hatua ya nusu fainali baada ya kuitoa Singida Black Stars kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Simba imetinga hatua ya nusu fainali baada ya jana kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya TRA United.
Mara ya mwisho kwa Yanga kucheza katika Uwanja wa CCM Kirumba ilikuwa ni Aprili 8, 2026 ilipopata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji.
Azam FC yenyewe ilipoenda hapo mara ya mwisho ilikuwa ni Machi 2, 2026 kucheza na Pamba Jiji ambapo ililazimishwa sare ya mabao 2-2.
Coastal Union mara ya mwisho ilipocheza katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha ilipoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Fountain Gate.
Simba yenyewe ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate ilipocheza hapo mara ya mwisho.
