
Dar es Salaam. Serikali ya Marekani imeanza maandalizi ya kuwahamisha baadhi ya raia wake walioguswa na mlipuko wa Ebola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wakati juhudi za kimataifa zikiongezwa kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
Kutokana na hali hiyo, Marekani tayari imetoa tahadhari mpya ya safari dhidi ya kusafiri kwenda DRC, huku ubalozi wake mjini Kampala ukisitisha kwa muda huduma za viza kutokana na hofu ya kuenea kwa ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la CNN leo Jumatatu, Mei 18, 2026 hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza rasmi mlipuko huo kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa, kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi katika DRC na Uganda.
Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa cha Marekani (CDC) kimesema kinaunga mkono juhudi za kuwahamisha Wamarekani walioathiriwa moja kwa moja na mlipuko huo, huku ripoti zikieleza kuwa baadhi yao walikuwa katika hatari kubwa ya maambukizi.
Hata hivyo, mamlaka za afya Marekani hazijathibitisha iwapo kuna raia wake waliothibitika kuambukizwa Ebola. Mkuu wa operesheni ya mwitikio wa Ebola wa CDC, Dk Satish Pillai amesema taasisi hiyo inaendelea kutathmini hali halisi ilivyo ardhini kabla ya kutoa taarifa zaidi kuhusu waathirika.
WHO imesema mlipuko huo unaendelea katika Jimbo la Ituri mashariki mwa DRC ambako hadi sasa vifo 10 vimethibitishwa rasmi huku vifo vingine vikihusishwa pamoja na wagonjwa wapya 336. Uganda nayo imeripoti visa viwili vilivyothibitishwa maabara, ikiwamo kifo kimoja mjini Kampala.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa CDC Afrika, Jean Kaseya, zaidi ya watu 100 wanaoshukiwa kufariki dunia wamehusishwa na mlipuko huo nchini DRC.
WHO imesema mlipuko hunasababishwa na aina ya virusi vya Ebola vinavyojulikana kama Bundibugyo, aina ambayo kwa sasa haina chanjo wala tiba maalumu zilizoidhinishwa.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya misuli, vipele na wakati mwingine kutokwa damu. Ugonjwa huo huambukizwa kwa kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au vifaa vilivyochafuliwa.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, Médecins Sans Frontières, limesema kiwango cha vifo kwa aina ya Bundibugyo kinakadiriwa kuwa kati ya asilimia 25 hadi 40.
Wakati huo huo, WHO imesema tani saba za vifaa vya dharura vya matibabu pamoja na wataalamu 35 wa afya tayari wamewasili katika mji wa Bunia kusaidia juhudi za kudhibiti mlipuko huo.
Serikali ya DRC nayo imesema imefungua vituo vitatu vya matibabu katika maeneo yaliyoathirika ili kuongeza uwezo wa kuwahudumia wagonjwa.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wameonya kuwa juhudi za kukabiliana na Ebola zinakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na migogoro ya kivita mashariki mwa DRC ambayo imedhoofisha mifumo ya afya na kusababisha mamilioni ya wananchi kuyahama makazi yao.
Mlipuko huu ni wa 17 wa Ebola kutokea DRC tangu virusi hivyo vilipogunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976.
