Imani za kishirikina zinavyokwaza mapambano dhidi ya fistulaImani za kishirikina zinavyokwaza mapambano dhidi ya fistula

Tabora. Imani za kishirikina na hofu ya unyanyapaa zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazoathiri juhudi za kutokomeza Ugonjwa wa Fistula nchini, huku wanawake wengi wakiamini hali hiyo husababishwa na uchawi badala ya matatizo ya uzazi.

Hayo yameelezwa leo, Jumanne Mei 19, 2026, mjini Tabora na Mratibu wa Afua ya Ugonjwa wa Fistula kutoka Wizara ya Afya, Fidea Obimbo.

Amesema wanawake wengi wanaokumbana na changamoto hiyo hushindwa kufika hospitalini mapema kutokana na kuamini hawawezi kutibiwa kitabibu.

“Tatizo kubwa ni kwamba jamii nyingi bado zinaamini fistula ni ugonjwa wa kulogwa, kumbe hali hiyo hutokea kutokana na uzazi pingamizi au uchungu wa muda mrefu wakati wa kujifungua,” amesema.

Amesema kutokana na imani hizo, wanawake wengi hukimbilia kwa waganga wa jadi badala ya hospitali, hali inayochelewesha matibabu na kuongeza mateso kwa wagonjwa.

Obimbo ameeleza kuwa, kati ya wanawake 2,500 hadi 3,000 wanaobainika kuwa na fistula kila mwaka nchini, ni wanawake takribani 1,500 pekee wanaofanikiwa kupata matibabu kutokana na changamoto za uelewa na utayari wa kujitokeza.

Amesema maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani yatafanyika Mei 23 mwaka huu katika Hospitali ya Nkinga wilayani Nzega mkoani Tabora, yakibebwa na kaulimbiu ya: “Afya ni haki ya msingi ya kila mwanamke, wekeza kutokomeza fistula na majeraha yatokanayo na uzazi.

“Hospitali ya Nkinga ni moja ya vituo vinavyotoa huduma za matibabu ya fistula nchini, hivyo tumeweka kambi maalumu ya madaktari kwa ajili ya upasuaji na huduma nyingine za kurejesha matumaini kwa wanawake hawa.”

Amesema hadi sasa wanawake 15 tayari wamejitokeza kupata matibabu katika hospitali hiyo huku akitoa wito kwa wengine kujitokeza mapema.

Mkazi wa Tabora, Johari Mtemvu, amesema wanawake wengi wenye Fistula hupitia maisha magumu kutokana na kutengwa na jamii.

“Mtu anakosa kujiamini kabisa kwa sababu ya harufu na hali anayopitia. Wengine hujikuta wakikosa hata watu wa kuzungumza nao,” amesema.

Saidi Salim, amesema zamani waliamini ugonjwa huo unasababishwa na uchawi, lakini elimu inayotolewa sasa imewasaidia kuelewa kuwa unatibika hospitalini.

“Tulikuwa tunakosea kuwapeleka wanawake kwa waganga wa jadi, kumbe wanahitaji matibabu hospitalini. Serikali iendelee kutoa elimu ili wanawake wengi waokolewe,” amesema.

Takwimu za Hospitali ya Nkinga zinaonesha kuwa tangu mwaka 2017 hadi 2025, wanawake 523 wamepatiwa matibabu ya fistula hospitalini hapo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *