Unguja. Wizara ya Afya imeomba kuhidhinishiwa Sh405.89 bilioni kutekeleza vipaumbele sita ambayo vitajikita katika, kuimarisha utoaji huduma, ujenzi wa miundombinu ya afya, vifaa tiba, kuimarisha mifumo ya kidijitali na kuimarisha nguvu kazi ya wizara kwa kuajiri.
Akisoma hotuba ya bajeti hiyo leo Mei 19, 2026, Kaimu Waziri wa Wizara hiyo, Dk Saada Mkuya amesema bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh368.15 bilioni hadi Sh405.89 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 10.23 kwa mwaka 2026/2027 kwa kuzingatia kuimarisha maeneo muhimu ya sekta hiyo.
Ameyataja maeneo hayo ni pamoja na miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali maalumu ya huduma ya saratani Binguni, kuendelea na ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja eneo la Mahonda, ujenzi na utanuzi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja na kuimarisha huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo katika Hospitali ya Lumumba.
“Ujenzi wa hospitali tatu za mikoa; Kusini Makunduchi, Kaskazini Wete na Kusini Chake Chake Pemba. Ujenzi wa hospitali maalumu ya matibabu ya macho Mazizini Unguja, ujenzi wa ofisi ya maabara ya chakula, dawa na vipodozi Chamanagwe Pemba, vituo vya afya ya msingi na kuimarisha nguvu kazi kwa sekta ya afya,” amesema Dk Saada.
Mjumbe wa kamati ya Ustawi wa Jamii, Shaame Ali Ali akisoma hotuba ya maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Afya mwaka 2026/27 Barazani Chukwani Unguja Zanzibar.
Dk Saada amesema wanatarajia kusomesha wataalamu bingwa na bobezi, kuimarisha huduma za kidijitali, ununuzi wa mashine za kisasa za kimaabara na kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Kuanzisha na kutekeleza, Mfuko wa maendeleo ya sekta ya afya, ambao pamoja na shughuli nyinginezo, itasaidia katika kuimarisha utolewaji wa huduma za afya kwa kuimarisha ujuzi wa wataalamu wa afya, ununuzi wa vifaa tiba pamoja na miundombinu mengine ya afya.
Pia, katika mkakati wa wizara, Dk Mkuya amesema inapanga kuanzisha Taasisi ya huduma na wataalamu Zanzibar ikiwa ni pamoja na (Baraza la Madaktari, Baraza la Wauguzi na Wakunga, Baraza la Maofisa Afya Jamii na Mazingira, Baraza la Wataalamu wa Uchunguzi wa Maabara, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi.
Katika kuimarisha huduma za kinga na elimu ya afya dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza Dk Mkuya amesema Sh141.11 bilioni sawa na asilimia 34.8 ya bajeti zimetengwa huku huduma za utibabu wa maradhi umetengewa Sh184.89 bilioni sawa na asilimia 45.6 ya bajeti.
Amesema Wakala wa Bohari Kuu ya Dawa ilinunua dawa, vitendanishi vya maabara na vifaa tiba kutoka kwa wazalishaji na wazabuni yenye thamani ya Sh9.07 bilioni na kusambazwa katika vituo vya afya Unguja na Pemba.
Changamoto
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2024/2025, amesema wizara imepitia changamoto ikiwa ni pamoja na msongamano mkubwa wa wagonjwa kutokana na uhaba wa watumishi na wananchi kutofuata mfumo wa rufaa.
Pia, kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) na ajali za barabarani na uhaba wa madaktari na wauguzi bingwa na bobezi na huduma nyingine za kitaalamu.
Changamoto nyingine ni upatikanaji wa fedha usioridhisha kwa ajili ya uendeshaji wa wizara na miradi ya maendeleo. Hadi kufikia Machi 2026, fedha zilizotolewa ni Sh185.42 bilioni, sawa na asilimia 67 ya makadirio ya miezi tisa zilipatikana.
Mama na mtoto
Waziri Mkuya amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika eneo la huduma za mama na mtoto na kuendelea kuimarisha utekelezaji wa afua mbalimbali zilizopelekea kupungua vifo vya mama vinavyotokana na ujauzito kutoka vifo 145 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2023 hadi vifo 121 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2025.
Kaimu Waziri wa Afya, Dk Saada Mkuya akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo mwaka 2026/27 katika mkutano wa baraza la bajeti Chukwani Unguja Zanzibar.
“Kwa upande wa vifo vya watoto wachanga ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa vimepungua kutoka 13.2 katika kila vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2023 hadi kufika 11 katika kila vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2025,” amesema Dk Saada.
Katika kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga, wizara inaendelea kutekeleza mfumo wa huduma za rufaa kwa mama wajawazito na watoto wachanga (M-mama).
Akisoma maoni ya kamati ya ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi, Mjumbe wa kamati hiyo Shaame Ali Ali, amesema licha ya Serikali kujenga hospitali, huduma zinazotolewa zinasuasua katika hospitali hizo jambo linalorudisha nyuma kasi ya Serikali kuwaleta wananchi wake maendeleo.
“Kamati inaishauri Serikali kufutilia kwa ukaribu hospitali hizo utoaji wa huduma ili kufikia malengo,” amesema
Pia, kamati imeishauri Serikali kuharakisha ujenzi ghala la kuhifadhi dawa na vifaa tiba ili wakala wa dawa aondokane na changamoto ya kukosa sehemu ya kuhifadhi dawa wanapopata mzigo mkubwa.
