
Dodoma. Katika mwaka wa fedha 2026/27, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umepanga kujenga barabara kuu zenye urefu wa kilomita 260.5 kwa kiwango cha lami, Bunge limeelezwa.
Katika bajeti yake ya takribani Sh2.6 trilioni, Wizara ya Ujenzi imetangaza kufanya ukarabati wa kilomita 87.5 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa madaraja 16, ukarabati wa daraja moja (1) na kuendelea na maandalizi ya ujenzi wa madaraja 11.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa takwimu hizo leo Jumatano Mei 20,2026 wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambapo amesema kazi nyingine ni kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara zenye urefu wa kilomita 7,020.79.
Waziri ametaja pia ujenzi wa madaraja matatu, ambayo ni Bujonde (Mbeya), Kilambo (Mtwara) na Sanga (Simiyu) ambayo ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara zenye urefu wa kilomita 135.51 na kati hizo, kilomita 59 zitajengwa kwa kutumia fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali na kilomita 76.51 zitajengwa kwa fedha za Mfuko wa Barabara.
“Vilevile, wakala umepanga kufanya ukarabati kwa kiwango cha changarawe wa barabara zenye urefu wa kilomita 693.21,kati ya hizo, kilomita 421.62 zitakarabatiwa kwa kutumia fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali na kilomita 271.59 zitakarabatiwa kwa kutumia fedha za mfuko wa Barabara,” amesema Waziri Ulega.
Amesema Wakala umepanga kujenga na kufanya ukarabati wa madaraja/ makalavati 73, ambapo kati ya hayo, madaraja/ makalavati 51,129 yatatumia fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali na 22 yatatumia fedha za Mfuko wa Barabara.
Waziri amesema Wakala umepanga kufanya matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa ambayo yatahusisha matengenezo ya kawaida (routine and recurrent maintenance) kwa kilomita 35,356.36 matengenezo ya muda maalumu kilomita 3,390.92.
Nyingine ni matengenezo ya sehemu korofi kilomita 382.47 na matengenezo ya madaraja 3,863 ambapo mpango huo utahusisha shughuli za udhibiti wa uzito wa magari na hifadhi za barabara, kazi za dharura na mradi wa matengenezo ya barabara kwa mikataba ya muda mrefu.
Kingine ni kusimamia miradi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vilivyokasimiwa Wizara ya Ujenzi.
