
Dar es Salaam. Matangazo ya bidhaa hasa zinazouzwa kupitia mtandaoni hivi sasa yamekuwa yakitangazwa kimkakati ukilimganisha na zamani, kwa kuchomekewa katikati ya maudhui mengine, kama video za vichekesho, simulizi na habari mbalimbali.
Ni kawaida kukuta video yenye maudhui ya kichekesho au tamthilia ndani ikiwa na tangazo la bidhaa ambalo linachomekwa kana kambwa ni sehemu ya video hiyo.
Zile zama za kuona bango kubwa barabarani lenye picha ya bidhaa na neno “NUNUA SASA KWA BEI NAFUU.” au kusikia tangazo la redio likipiga kelele kuhusu sifa za bidhaa fulani, zinaonekana zinabadilika.
Haya ni mapinduzi makubwa ya ubunifu katika sekta ya matangazo nchini, ambapo wafanyabiashara kuanzia wajasiriamali wadogo hadi kampuni kubwa sasa wanatumia mbinu ya kusimulia (storytelling), vichekesho vifupi na maudhui ya uhalisia ili kushika soko.
Mfano, mtengeneza maudhui anaweza akaandaa video ambayo ndani yake anazungumzia bidhaa fulani kama sehemu ya kichekesho, lakini ujumbe ndio unakua umefika bila ya kumkera mtazamaji.
Mabadiliko haya yanakuja huku kukiwa na ushindani mkubwa wa kibiashara mtandaoni, unaochochewa na mabadiliko ya tabia za walaji ambao sasa hawana uvumilivu wa kuangalia matangazo ya kulazimisha.
Lakini ubunifu huu ndio unahitajika na walaji kwa maana tangazo la moja kwa moja mara nyingi watu huwa hawaliangalii, kama anavyosema mchumi aliyejikita kwenye uchumi wa kidijitali, Freancis Nyonzo aalipozungumza na Mwananchi digital kwa njia ya simu leo Jumanne Mei 20, 2026
“Kiufupi digitali imebadili namna ya kufanya marketing. Hivyo watu wa masoko wamekuwa na ubunifu ili kwenda sawa na mabadiliko yanayoletwa. Matangazo kuwepo kwenye filamu ilikuwa zamani. Hii ni namna nyingine ya kutangaza bila mtu kuona hili ni tangazo. Kwetu hatutumii movie (sinema), bali watengeneza maudhui wenye views nyingi (watazamaji wengi),” anasema.
Nyonzo anasema unaweza kukuta muhusika anaenda kwenye friji au dukani anachukua kinywaji fulani ambacho ni biashara, anakuwa tayari kashatangaza bidhaa, jambo ambalo hata wachekeshaji wa sasa Tanzania ndicho wanachokifanya.
Mfanyabiashara wa Sinza, Eddie Michael anasema sikio na jicho la mtumiaji wa simu janja hivi sasa lina mambo mengi yanayochuana kuwania usikivu wake. Ukianza tangazo kwa kusema ‘Kampuni yetu inauza.., mtu anasogeza mbele (swipe).
“Lakini ukianza na drama, ucheshi au swali linalomgusa, umemkamata. Ndio maana matangazo ya sasa yanajificha ndani ya burudani,” amesema Michael.
Mjasiriamali anayejishughulisha na uuzaji wa bidhaa za urembo kutoka Soko la Kariakoo, Neema Festo anasema mabadiliko haya yameokoa biashara iliyoanza kukosa wateja lakini baada ya kushtuka na kuanza kutangazwa kwa watengeneza maudhui imemsaidia.
“Zamani nilikuwa nikipiga picha sabuni, mafuta naweka mtandaoni lakini nimeamua kuanza kurekodi video fupi nikiwa katika mazingira tofauti na hapo mtu anaweza kuhisi ni tangazo, au namtumia kichekesho mtengeneza maudhui inanisaidia,” ameiambia Mwananchi.
Mtindo huu wa matangazo hauishii kwa wafanyabiashara wadogo tu bali hata kampuni kubwa, benki sasa zinawatumia zaidi wachekeshaji wa mitandaoni (Digital Influencers/Content Creators) kutengeneza maudhui, ambayo mwanzoni yanaonekana kama vichekesho vya kawaida, lakini mwishoni yanabeba ujumbe mzito wa kibiashara.
Inaelezwa baadaye biashara zitakazofanikiwa si zile zenye mitaji mikubwa ya kulipia mabango ya barabarani, bali ni zile zenye uwezo wa kugusa hisia za walaji kupitia simu zao za mkononi kwa kutumia sanaa, ucheshi na uhalisia wa maisha ya Kitanzania.
