Wadau wafunguka Nigeria kupiga marufuku matumizi ya ‘Dk’ wenye udaktari wa heshimaWadau wafunguka Nigeria kupiga marufuku matumizi ya ‘Dk’ wenye udaktari wa heshima

Wakati Serikali ya Shirikisho la Nigeria ikipiga marufuku watu waliotunukiwa shahada za udaktari wa heshima kutumia kiambishi cha “Dk” mbele ya mwanzo wa majina yao katika matumizi rasmi, kitaaluma au ya kikazi, wadau wamelipokea kwa maoni tofauti kuhusu jambo hilo.

Serikali ya Nigeria imesema matumizi ya cheo hicho kwa wahusika yanachukuliwa kuwa ni upotoshaji wa sifa za kitaaluma, na kuanzia sasa hatua hiyo itahesabika kama udanganyifu wa kitaaluma wenye madhara ya kisheria na kijamii.

Waziri wa Elimu wa Nigeria, Tunji Alausa, alitangaza uamuzi huo Mei 11, 2026 Ikulu ya Nigeria wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi ulioidhinishwa na Baraza la Mawaziri ambao haukuwa umetangazwa katika kikao kilichotangulia.

Alausa, aliyekuwa ameambatana na Naibu Waziri wa Elimu, Suwaiba Ahmad, alisema Baraza la Mawaziri limeidhinisha sera ya pamoja kuhusu utoaji na matumizi ya shahada za heshima katika vyuo vikuu vya Nigeria.

Alisema sera hiyo inalenga kukomesha kile alichokitaja kuwa ni miongo ya utoaji holela wa shahada hizo kwa ajili ya maslahi ya kisiasa na kifedha, pamoja na kurejesha imani ya umma katika uhalali wa hadhi za kitaaluma.

“Mtindo wa hivi karibuni wa utoaji wa shahada za heshima umeonyesha kuongezeka kwa matumizi mabaya na siasa katika fursa hii ya kitaaluma,” alisema Alausa.

“Tumeona shahada hizo zikitumika kwa upendeleo wa kisiasa, maslahi ya kifedha, pamoja na kutolewa kwa viongozi waliopo madarakani, jambo ambalo kimaadili halipaswi kutokea,” aliongeza.

Kwa mujibu wa sera hiyo mpya, waliotunukiwa shahada za heshima hawataruhusiwa tena kutumia kiambishi cha “Dk” kabla ya majina yao.

Badala yake, wanatakiwa kuandika hadhi kamili ya shahada hiyo baada ya jina lao.

Akitoa mfano, Alausa alisema mtu anaweza kuandika “Bw Louis Clark, D.Lit. (Doctor of Literature, Honoris Causa)” au “Bi Miriam Adamu, LL.D. Hons.”

Alisema mfumo huo utaonyesha wazi kuwa shahada hiyo ni ya heshima na si ya kitaaluma iliyopatikana kupitia masomo rasmi.

“Waliotunukiwa shahada za heshima hawapaswi kutumia kiambishi cha ‘Dk’ mbele ya majina yao katika matumizi rasmi, kitaaluma au ya kikazi,” alisema Waziri huyo.

Aliongeza kuwa, “Kuonyesha shahada za heshima kana kwamba ni sifa halali za kitaaluma kutachukuliwa kama udanganyifu wa kitaaluma na kutakuwa na madhara ya kisheria pamoja na kuharibu sifa za mhusika.”

Mjadala bungeni

Hapa nchini, Februari 2023, suala la shahada za udaktari wa heshima liliibuka bungeni ambapo Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi alitaka kufahamu ni kwa kiasi gani vyuo vinavyotoa shahada hizo vinatambulika katika mamlaka za Tanzania zinazosimamia elimu katika nchi hii.

Spika wa Bunge wakati huo, Dk Tulia Ackson alisisitiza hoja hiyo akisema taifa linahitaji kufahamu utaratibu wa kwenda nao huku akiwataka viongozi hao (wabunge) kuwa mfano kwa watoto wao.

Akifafanua kuhusu shahada za heshima, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali huwa inafuatilia uhalali wa chuo kilichomtunuku mtu shahada ya heshima kama imepokea maombi maalumu.

“Kwa watu ambao wanatunukiwa, mahitaji yanapotokea, Serikali kupitia TCU ifanye uhakiki, tuko tayari kufanya uhakiki na kutambua kwamba nani amepata lakini yasipokuja sisi huwa hatuingilii.

“Kwa hiyo sisi mahitaji yakija, kwamba huyu mtu anahitaji kuhakiki kile alichokipata kama PhD na amepewa na chuo ambacho kinatambulika duniani, likija hilo hitaji kwetu, kazi hiyo tuna uwezo wa kuifanya vizuri sana.

“Lakini tukisikia mtu yuko mahali tu labda amesema ameipata na hatujaulizwa sisi, hatuwezi kwenda kujiridhisha kwa kila mtu mahali popote alipo kwa sababu amesema amepata PhD,” alisema Profesa Mkenda.

Maoni mseto ya wadau

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Luisulie amesema Tanzania ilipaswa kuchukua hatua hiyo muda mrefu kabla ya Nigeria ili kupunguza uholela wa ugawaji wa shahada hizo.

“Hii inafanya elimu kuwa holela na kudharauliwa, ikishakuwa holela inakuwa inadharauliwa. Kwa hiyo, kuendelea kuchelewa tunaumiza nchi kwa sababu tutaua jitihada za kupigania heshima hiyo,” amesema Dk Louisulie.

Amewataka watu watofautishe kutunukiwa na kupewa, kwamba wanaosomea wanatunukiwa na wale wa heshima wanapewa.

“Kwa utaratibu wa kawaida, wale wanaopata udaktari wa heshima, hawapaswi kabisa kuitwa ‘Dk’, bali wanatakiwa kujitambulisha kama Honoris Causa, lakini watu wameamua kufanya hivyo, ikazoeleka na sasa imekuwa ni mtindo wa maisha,” amesema.

Akiwa na mtazamo tofauti, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana amesema kila nchi ina mamlaka zake zinazodhibiti vyuo vikuu au zinazodhibiti ubora, kwa hiyo uamuzi wa Nigeria ni wao lakini nchi nyingi zinatoa shahada za udaktari wa heshima.

“Hii ni title inayoheshimika, inayotambulika popote dunia, Marekani wanafanya hivyo, Japan wanafanya hivyo, India wanafanya hivyo, kwa hiyo huo ni utaratibu wa nchi.

“Mimi sioni tatizo, sisi tuendelee tu, mtu akikidhi vigezo vilivyowekwa na Mamlaka ya chuo kwamba anaweza kutunukiwa shahada ya udaktari wa heshima, atunukiwe tu. Mwalimu (Julius Nyerere) alikuwa nazo zaidi ya 20, Benjamin Mkapa zaidi ya nane. Kwa hiyo mtu anayefanya kitu kinachotambulika, tumtunuku tu,” amesema Dk Bana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *