Hivi ndivyo maziwa ya nyuki yatakavyokuchelewesha kuzeekaHivi ndivyo maziwa ya nyuki yatakavyokuchelewesha kuzeeka

Dar es Salaam. Umewahi kusikia umuhimu wa maziwa ya nyuki? Hii ni bidhaa adimu na muhimu ya wadudu hao maarufu kwa kung’ata na kutengeneza asali, inayoweza kupunguza dalili za kuzeeka kwa binadamu (anti-aging).

Mbali na maziwa, kimsingi nyuki ana mazao saba ambayo ni asali, nta, chavua (ungaunga unaotokana na maua au Bee Pollen), sumu ya nyuki, gundi ya nyuki (utomvu wa mimea mbalimbali nyuki anaotumia kuzuia vimelea kuingia kwenye mzinga) na majana.

Kitaalamu maziwa ya nyuki yana vitamini mbalimbali zinazoweza kulainisha ngozi, kupunguza ukavu, kusaidia uzalishaji wa collagen na kulinda seli dhidi ya uharibifu.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanaeleza bado tafiti zaidi zinaendelea ili kuthibitisha kiwango chake halisi cha uwezo wa kupunguza dalili za uzee kwa binadamu.

Akifanya mahojiano na Mwananchi jana Jumatano Mei 20, 2026 siku ya maadhimisho ya nyuki duniani, Igunda Selele, Ofisa Ufugaji Nyuki Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Shamba la Nyuki Manyoni anasema yana protini nyingi inayomfanya hata malkia wa nyuki kuishi muda mrefu wa miaka miwili hadi mitano.

“Mtu anakuwa na mwonekano usio wa kizee ingawa anakuwa na umri mkubwa (kuna ile hali unakutana na mtu ana umri mkubwa lakini hazeeki). Badala ya seli kutumika kuzeeka haraka, maziwa ya nyuki yana uwezo wa kupunguza kutumika kwa seli hizo,” anasema.

Anasema ndiyo maana hata malkia wa nyuki ambaye anatumia hayo maziwa anaishi kwa muda mrefu ukilinganisha na nyuki wa kawaida anayeishi miezi kadhaa.

Akieleza yanavyotengenezwa anasema nyuki wanapokuwa wadogo wakishaanguliwa wanakuwa na uwezo wa kutengeneza maziwa kwa kiasi kidogo, ikiwa ni chakula maalumu cha kulishia malkia na watoto wadogo wa nyuki.

“Ili kuyapata unaandaa mazingira ya nyuki kumkuza malkia ambapo kiwavi aliyeandaliwa kuwa malkia analishwa maziwa hayo. Hivyo nyuki wanaandaliwa, wakishakuwa tayari kumlisha maziwa unaenda kukatisha kitendo hicho na badala yake maziwa hayo yanavunwa,” anasema.

Anasema gharama ya maziwa hayo ni kubwa ambapo gramu moja inauzwa hadi Sh20,000. Akifafanua zaidi anasema maziwa hayo hunywewa kama asali au kuwekwa kwenye vidonge.

Unga wa nyuki

Mtaalamu na mtoa tiba za bidhaa za nyuki kutoka Mpunguzi Dodoma, Festo Mugongo anasema unga wa nyuki au chavua unatokana na maua yenye asili tofauti tofauti huku kijiko chake kimoja kinakuwa na maelfu ya mimea ya maua ikiwemo yenye dawa na virutubisho muhimu.

“Unga huo unaweza kutumiwa kama vitamini. Kama mtu ana shida kwenye mfumo wa chakula anaweza kutumia unga huo kumletea hamu ya kula, inakuza kinga ya mwili, ni chakula cha asili kilichojitosheleza chenyewe.” “Unga huo pia unasaidia katika afya ya uzazi.

Anasema mazao ya nyuki yana uwezo wa kunyonya kemikali zilizopo kwenye mwili wa binadamu ambazo zinaua seli. Pia yana uwezo wa kuzuia uvimbe na kutibu kilichosababisha uvimbe huo kuingia mwilini, iwe ni bakteria, kujigonga au fangasi.

“Mazao ya nyuki yana muundo wa kikemikali unaotokana na vitamini, protini na madini mbalimbali, ndiyo maana yanaweza kutumika kama tiba kwa sababu yanaweza kupambana na bakteria mbalimbali,” anasema Mugongo ambaye ni Mkurugenzi wa API-Care International.

Nyuki anaweza kutumika kama tiba na kuimarisha afya ya binadamu. Pia husaidia kuchavusha mimea, kilimo na kutunza mazingira. Kutokana na umuhimu huu ndiyo maana Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeanzisha siku hiyo ya kukumbushana umuhimu wa nyuki pamoja na kuwatunza.

Mbali na hayo, uchavushaji, uhifadhi wa mazingira na kuhusika katika uzalishaji wa chakula ni miongoni mwa faida zake katika maisha ya mwanadamu pamoja na uchumi.

Kwa mujibu wa tafiti za kisayansi za nyuki na asali za Taasisi ya Kimarekani (NCBI), sehemu kubwa ya mazao ya chakula duniani hutegemea uchavushaji unaofanywa na nyuki na wachavushaji wengine. Hivyo, uwepo wao husaidia kuongeza uzalishaji wa matunda, mboga, karanga na mazao mengine muhimu kwa lishe ya binadamu.

Nyuki husaidia kuzalisha chakula kupitia maua ya mimea mbalimbali, jambo linalosaidia mazao kuzaa vizuri na kuongeza mavuno. Bila nyuki, uzalishaji wa baadhi ya vyakula ungepungua kwa kiwango kikubwa.

FAO inaeleza zaidi ya asilimia 75 ya mazao ya chakula duniani hutegemea uchavushaji unaofanywa na nyuki na wadudu wengine wachavushaji. Hii ina maana mazao mengi ya matunda, mboga na karanga yasingepatikana kwa wingi bila uwepo wa nyuki.

Wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa kupungua kwa nyuki kunaweza kusababisha baadhi ya mimea kutoweka na kuvuruga mfumo mzima wa ikolojia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *