Sheria vyeti vya taaluma kutumika kama dhamana yajaSheria vyeti vya taaluma kutumika kama dhamana yaja

Dar es Salaam. Serikali imeanza kuandaa sheria maalumu itakayoruhusu matumizi ya mali zinazohamishika, ikiwemo vyeti vya taaluma kama dhamana ya kupata mikopo kwa lengo la kuwasaidia wahitimu wa vyuo kuanzisha miradi ya uwekezaji na shughuli za kiuchumi.

Hatua hiyo imeelezwa bungeni leo Alhamisi Mei 21, 2026 na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Neema Majule, aliyehoji mkakati wa Serikali kuwasaidia wahitimu kutumia vyeti vyao kupata mikopo ya kuanzisha miradi ya maendeleo.

Mbali na swali hilo la mbunge Neema, akiuliza swali la nyongeza Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko alitaka kujua utayari wa Serikali kuweka mfumo maalumu utakaowawezesha wahitimu kutumia taaluma na vyeti vyao kama dhamana ya kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha, ili waanzishe biashara na viwanda vidogovidogo.

Matiko ameuliza: “Nataka kujua Serikali ipo tayari sasa kuanzisha Graduate Credit Guarantee Scheme ambao utawezesha wahitimu hawa kutumia taaluma zao na vyeti vyao kama dhamana ili waweze kupata mitaji.

Pendekezo hilo limekuja wakati tafiti mbalimbali zikionyesha zaidi ya asilimia 60 ya wahitimu wa vyuo nchini hukosa ajira rasmi, hali inayowaacha vijana wengi wenye elimu na ujuzi kukaa bila kazi kwa muda mrefu.

Matiko amesema changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi ni kukosekana kwa dhamana zinazotambulika na benki pamoja na taasisi za fedha, jambo linalowafanya washindwe kupata mikopo hata wanapokuwa na mawazo ya biashara na ubunifu wa miradi ya uzalishaji.

Amesema mfumo huo unaweza kuwa suluhisho la muda mrefu kwa kuwa utaondoa utegemezi wa dhamana za mali zisizohamishika kama ardhi na nyumba ambazo wahitimu wengi hawana.

Akitoa ufafanuzi kuhusu hilo Naibu Waziri ameeleza kwa sasa benki na taasisi nyingi za fedha hutegemea zaidi dhamana za mali zisizohamishika kama ardhi na majengo katika utoaji wa mikopo, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Sura ya 113.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuandaa sheria ya dhamana kwa mali zinazohamishika, ambayo inalenga kutambua rasmi mali hizo katika mfumo wa utoaji wa mikopo.

Amesema chini ya sheria hiyo, mali zinazohamishika zitakuwa zinasajiliwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuimarisha usimamizi, uwazi na ufuatiliaji wa dhamana hizo.

“Miongoni mwa mali zinazopendekezwa kufanyiwa tathimini ni vyeti vya taaluma vya wahitimu wa vyuo, kwa lengo la kuchunguza uwezekano wa kuvifanya vitumike kama dhamana katika upatikanaji wa mikopo,” amesema Naibu Waziri huyo.

Pamoja na mpango huo, Serikali imeendelea kuwahamasisha vijana kutumia mifuko na programu mbalimbali zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Baadhi ya mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Vijana, unaotoa mikopo kwa riba nafuu kwa lengo la kuwawezesha vijana kujiajiri na kuendeleza biashara zao.

Aidha, mpango huo umewahi kuelezwa ndani na nje ya Bunge na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kwamba unakwenda kuwa msaada hasa kwa vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *