Chanjo ya Ebola itachelewa, WHO yaonya vifo vitaongezeka zaidiChanjo ya Ebola itachelewa, WHO yaonya vifo vitaongezeka zaidi

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya huenda ikachukua kati ya miezi sita hadi tisa kabla ya chanjo dhidi ya aina ya Ebola ya Bundibugyo kuwa tayari kutumika, huku idadi ya vifo na maambukizi ikiendelea kuongezeka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hadi sasa kuna zaidi ya wagonjwa 600 waliopata maambukizi ya Ebola na vifo 139 vinavyohusishwa na mlipuko huo, huku visa 51 vikithibitishwa nchini DRC na viwili nchini Uganda.

Akizungumza Geneva, Uswisi jana Jumatano, Mei 20, 2026 Dk Tedros amesema idadi hiyo huenda ikaongezeka zaidi kutokana na kuchelewa kugundulika kwa ugonjwa huo katika maeneo yaliyoathirika.

WHO ilitangaza Jumapili kuwa mlipuko huo ni dharura ya afya ya umma yenye umuhimu wa kimataifa, lakini ikaeleza kuwa bado haujafikia kiwango cha janga la dunia.

“WHO inatathimini hatari ya mlipuko huu kuwa kubwa katika ngazi ya kitaifa na kikanda, lakini ndogo katika ngazi ya dunia,” amesema Tedros.

Aina ya Bundibugyo ndiyo chanzo cha mlipuko wa sasa, ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana tena baada ya zaidi ya muongo mmoja. Aina hiyo ilisimamisha milipuko miwili pekee hapo awali nchini Uganda mwaka 2007 na DRC mwaka 2012 ambapo takribani theluthi moja ya walioambukizwa walifariki.

Mshauri wa WHO, Dk Vasee Moorthy amesema chanjo mbili za majaribio dhidi ya Bundibugyo zinaendelea kutengenezwa lakini bado hazijafanyiwa majaribio ya kitabibu kwa binadamu.

Amesema chanjo moja inaonekana kuwa na matumaini makubwa zaidi, lakini inaweza kuchukua miezi sita hadi tisa kabla ya kuanza kutumika.

“Chanjo hiyo ndiyo inayopewa kipaumbele kwa sasa kama kinga yenye matumaini zaidi dhidi ya Bundibugyo,” amesema Dk Vesee.

Chanjo nyingine inayotumia teknolojia inayofanana na ile ya AstraZeneca iliyotumika dhidi ya Covid-19 bado iko katika hatua za uzalishaji, huku WHO ikisema huenda dozi zake zikawa tayari kwa majaribio ndani ya miezi miwili hadi mitatu.

Mbali na changamoto ya chanjo, wataalamu wanasema hakuna dawa maalumu inayolenga aina ya Bundibugyo, hali inayofanya matibabu kuwa magumu zaidi.

Mlipuko huo umeathiri zaidi mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC, huku wagonjwa wa Uganda wakihusishwa na wasafiri waliotoka DRC. Mgonjwa mmoja nchini Uganda amefariki dunia.

Wahudumu wa afya waliopo maeneo yaliyoathirika wameeleza hospitali zimeelemewa na wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola, huku baadhi yao wakifanya kazi bila vifaa vya kutosha vya kujikinga.

Meneja wa programu za dharura wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), Trish Newport, amesema baadhi ya vituo vya afya vimejaa wagonjwa wanaoshukiwa kuambukizwa.

“Hatujawahi kuona hali kama hii kwa sasa. Vituo vingi havina nafasi tena,” amesema.

Serikali ya Uingereza imetangaza kutoa hadi pauni milioni 20 kusaidia kukabiliana na mlipuko huo, ikiwamo kugharamia wahudumu wa mstari wa mbele, kuimarisha udhibiti wa maambukizi na ufuatiliaji wa ugonjwa.

Ebola husambazwa kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa aliyeambukizwa au ngozi yenye michubuko. Ugonjwa huo unaweza kusababisha kutokwa damu nyingi na viungo vya mwili kushindwa kufanya kazi.

Mgonjwa wa kwanza anayejulikana katika mlipuko huu ni muuguzi aliyefariki Aprili 24 mwaka huu katika mji wa Bunia, mkoani Ituri.

WHO imesema changamoto nyingine kubwa ni kwamba dalili za awali za Ebola zinafanana na magonjwa ya kawaida katika eneo hilo kama malaria na homa ya matumbo, hali inayochelewesha utambuzi wa ugonjwa.

Mashariki mwa DRC pia imekumbwa na migogoro ya muda mrefu ya makundi yenye silaha, jambo linaloendelea kuathiri juhudi za kudhibiti maambukizi hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *