“Tutawafanya maadui wajute”: Qalibaf aonya dhidi ya njama za Marekani kuanzisha vita vipya“Tutawafanya maadui wajute”: Qalibaf aonya dhidi ya njama za Marekani kuanzisha vita vipya

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ametoa onyo kali akisema kuwa mienendo ya wazi na ya siri ya adui inaashiria wazi kuwa wanapanga kuanzisha duru nyingine ya vita.

Amesisitiza kuwa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yako tayari kikamilifu na yatamfanya adui yeyote ajute iwapo atathubutu kufanya uchokozi mpya dhidi ya nchi hiyo.

Katika ujumbe wake wa tatu wa sauti kwa wananchi wa Iran uliotolewa Jumatano, Qalibaf amesema ingawa mapigano yamesimama kufuatia makubaliano ya kusitisha vita, adui bado hajaacha malengo yake ya kijeshi.

Qalibaf amesema: “Mienendo ya adui ya wazi na ya siri inaonyesha kuwa, sambamba na shinikizo za kiuchumi na kisiasa, bado hajakata tamaa kuhusu malengo yake ya kijeshi na anatafuta njia ya kuanzisha duru mpya ya vita na uadui mwingine.”

Spika wa Bunge la ameongeza kuwa Marekani kwa sasa imetumbukia katika mkwamo mkubwa wa kimkakati. Akifafanua amesema: “Ukweli ni kwamba adui, kinyume na majigambo yake ya mara kwa mara, amekwama katika changamoto kuu ya kimkakati”, huku akitolea mfano kupanda kwa bei ya mafuta, machafuko katika soko la dhamana, viwango vya juu vya riba, na mfumuko wa bei nchini Marekani.

Qalibaf amesema Trump kwa sasa anasita kati ya machaguo mawili: “Chaguo la kwanza ni kutanguliza kumaliza vita, kwa kukubali kushindwa. Chaguo la pili ni kuanzisha tena vita au kuendeleza mzingiro wa majini ili kuishinikiza Iran ikubali kusalimu amri.”

Ameongeza kuwa tathmini makini ya hali ya Marekani inaonyesha kuwa Washington bado inang’ang’ania tumaini potofu kwamba Iran itasalimu amri.

Qalibaf ametoa wito kwa taifa la Iran kuimarisha utayari wa kijeshi na ustahimilivu wa kiuchumi. Amewahakikishia wananchi kuwa majeshi ya Iran yametumia kipindi hiki cha kusitisha vita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi.

“Kwa taufiki na nusra ya Mola, na kwa kuungwa mkono na wananchi, leo hii jeshi letu lina utayari ambao utamshangaza adui na bila shaka litamfanya ajute kwa uchokozi wowote mpya dhidi ya Iran,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *