
Kuanzia mifumo ya usafiri inayotumia akili mnemba (AI), nakala za kidijitali za miji hadi bustani zinazozuia mafuriko, miji duniani inakumbatia teknolojia kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa ushirikishwaji, uaminifu na usalama vitaamua nani atanufaika kweli na maendeleo hayo.
Katika maonesho makubwa ya miji yanayofanyika Baku, mji mkuu wa Azerbajian ambako kunaendelea Mkutano wa 13 wa Miji duniani, #WUF13, wageni wamevutiwa na skrini kubwa za kidijitali zilizoonesha mifano ya mafuriko, mifumo ya udhibiti wa reli za chini ya ardhi na nakala pepe za maeneo ya makazi.
Miji mbalimbali imewasilisha maono ya maisha ya mijini yanayoendeshwa na akili mnemba, miundombinu ya kidijitali na matumizi ya taarifa za muda halisi — taswira ya kile serikali nyingi zinachokiita “mji wa baadaye.”
Mfano wa Shanghai
Miongoni mwa miji inayoongoza katika ndoto ya miji ya kisasa au miji janja ni Shanghai nchini China. Katika banda la China maafisa wameeleza jinsi jiji hilo linavyotumia data kubwa na akili mnemba kujenga mfumo unaoitwa “Usimamizi wa Pamoja kwa Mtandao Mmoja.”
Mfumo huo unaunganisha usafiri, miundombinu, huduma za dharura na huduma za umma katika mtandao mmoja mkubwa wa kidijitali.
Shanghai pia imepunguza pengo la kidijitali kupitia mfumo wake wa “Huduma za Serikali Mahali Pamoja,” unaowezesha wakazi kupata zaidi ya huduma 3,500 za umma mtandaoni.
Mfumo wa usafiri wa jiji hilo ni mfano mwingine wa teknolojia ya kisasa. Reli ya chini ya ardhi ya Shanghai, ambayo ni miongoni mwa mitandao mikubwa duniani ikiwa na zaidi ya kilomita 800 na vituo zaidi ya 400, hutumia AI, mawasiliano ya kasi ya mtandao ya 5G na teknolojia za kutabiri hali ya hewa ili kuboresha usalama na kupunguza usumbufu.
Treni zinajiendesha bila dereva, mifumo ya AI hufuatilia nyufa
Baadhi ya njia tayari zina treni zinazojiendesha bila dereva. Mifumo ya AI hufuatilia nyufa, uvujaji wa maji na udhaifu wa miundombinu kwenye vichuguu vya reli huku data za abiria zikichambuliwa kwa wakati halisi ili kuzuia hitilafu.
Mfano mwingine ni Hifadhi ya Lingang Starry Sky Sponge Park yenye ukubwa wa hekta 54. Hifadhi hiyo imejengwa kwa teknolojia ya kudhibiti mafuriko kupitia barabara zinazopenyeza maji, mifumo ya uchujaji chini ya ardhi na mifereji janja inayoweza kuhifadhi, kusafisha na kutumia tena hadi mita za ujazo 15,000 za maji ya mvua kila siku.
Kipaumbele katika miji ya kisasa kiwe watu
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat), Anacláudia Rossbach amesema miji duniani inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa makazi, makazi holela, athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa pengo la kiuchumi.
Amesema teknolojia ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hizo lakini akasisitiza kuwa miji janja lazima iweke watu katikati ya maendeleo yake.
Kwa mujibu wake, haki za binadamu, ushirikishwaji na usawa lazima viwe msingi wa mageuzi ya kidijitali.
Pia alionya kuhusu hatari ya baadhi ya jamii kutengwa kidijitali. Wakati wa janga la coronavirus“>COVID-19, wakazi wengi wa makazi holela walikosa elimu, huduma na kazi za mtandaoni kutokana na ukosefu wa mtandao na vifaa vya kidijitali.
Nani mnufaika wa kweli?
Watafiti wengine wanaonya kuwa si kila matumizi ya teknolojia yana manufaa kwa wananchi. Mbunifu na mtafiti wa mijini kutoka Colombia, Gynna Millan, amesema teknolojia inaweza kuwa chombo cha kuwawezesha wananchi au njia ya kudhibiti watu, kutegemea namna inavyotumika.
Kwa miji mingi iliyo kusini mwa dunia, hasa maeneo yenye makazi yasiyo rasmi ambayo mara nyingi hayana miundombinu ya msingi au intaneti ya uhakika, swali muhimu si uwepo wa teknolojia bali kama kweli inaboresha maisha ya kila siku ya wananchi.
AI yafika katika usimamizi wa miji
Akili mnemba sasa inaingia kwa kasi katika mifumo ya usimamizi wa miji. Mshauri wa serikali ya jiji la Moscow, Dmitri Atov, amesema AI si neno la kisasa tu bali ni nyenzo inayobadili namna miji inavyoendeshwa.
Afisa wa Umoja wa Mataifa wa Mawasiliano (ITU), Yining Zhao, ametaja mwelekeo muhimu wa teknolojia unaobadilisha maisha ya mijini, ukiwemo matumizi ya mifumo inayoweza kuiga mwenendo wa miji, mawakala wa AI wanaoweza kufanya maamuzi kwa kujitegemea, roboti na droni, mazingira pepe ya kazi na nakala pepe za miji zinazotumika kupima mipango mbalimbali kwa wakati halisi.
Jiji la Moscow tayari lina moja ya mifumo mikubwa duniani ya nakala pepe za kidijitali inayosasishwa mara mbili kwa mwaka kwa kutumia picha za angani.
Hatari za usalama wa kidijitali
Kadiri miji inavyozidi kuunganishwa kidijitali, ndivyo inavyokuwa katika hatari zaidi ya mashambulizi ya mtandao.
Mwakilishi wa wakala wa usalama wa mtandao wa Azerbaijan, Aytaj Khalafli, amesema usalama wa mtandao sasa ni sehemu muhimu ya maendeleo ya miji janja.
Ameonya kuwa mashambulizi ya mtandao yanaweza kusababisha machafuko makubwa, hasa katika mifumo ya usafiri na huduma muhimu za umma.
Miji ya kisasa au miji janja ni kwa ajili ya nani hasa?
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasisitiza kuwa mafanikio ya miji hii hayatategemea ukubwa wa vituo vya data au kasi ya AI pekee, bali namna miji hiyo inavyowahudumia wananchi wake.
Wametaja miradi ya kuongeza maeneo ya kijani, kubadilisha barabara kuu kuwa maeneo ya umma na kuhamasisha matumizi ya kutembea kwa miguu na baiskeli kama mifano ya maendeleo endelevu ya mijini.
