Mbunge wa Musoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mgore Miraj, ameishinikiza Serikali kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi zinatumika moja kwa moja kwenye shughuli za ujenzi na matengenezo ya barabara nchini.
Akizungumza bungeni, mbunge huyo alipinga vikali pendekezo la kukata asilimia tano ya fedha za Mfuko wa Barabara na kuzipeleka kwenye matumizi mengine.
Amesema hatua hiyo itaathiri maendeleo ya sekta ya miundombinu kwani tayari wizara hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa bajeti ya kutosha.
Mgore alitolea mfano hali ya barabara kutoka Dodoma hadi Musoma, akieleza kuwa safari kwenye eneo hilo imekuwa ngumu kutokana na ubovu wa miundombinu unaosababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri na watumiaji wa barabara hizo kila siku.
Aidha, amesema uhaba wa fedha za matengenezo ndio chanzo cha kuchelewa kukarabatiwa kwa barabara nyingi nchini, hali inayowaathiri wananchi pamoja na shughuli za kiuchumi.
Ameitaka Serikali kutafuta vyanzo vingine vya mapato kwa ajili ya miradi mingine badala ya kupunguza fedha za Mfuko wa Barabara, akisisitiza kuwa uwekezaji kwenye miundombinu ya usafiri ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.
(Feed generated with FetchRSS)
