
Dar es Salaam. Marekani imemwekea vikwazo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Tanzania, Faustine Mafwele kwa tuhuma za kuhusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje, iliyonukuliwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.
Si mara ya kwanza kwa Marekani kuwawekea vikwazo maofisa au viongozi wa Tanzania, mwaka 2020 ilimwekea vikwazo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na mkewe kuingia nchini humo kwa madai ya kuhusika katika matukio mengi ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa Mei 21, 2026, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema hatua hiyo imechukuliwa chini ya kifungu cha 7031(c) baada ya kuwepo kwa “taarifa zinazoaminika” zinazomhusisha Mafwele na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Marekani imedai kuwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi Tanzania waliwakamata, kuwatesa na kuwafanyia ukatili wa kingono mwanaharakati wa Uganda, Agather Atuhaire pamoja na mwanaharakati wa Kenya, Boniface Mwangi, walipokuwa jijini Dar es Salaam kufuatilia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu.
Tukio hilo lilizua wasiwasi mkubwa kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu ya kikanda na kimataifa, yaliyotaka kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu madai ya ukiukwaji huo yaliyodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama vya Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikwazo hivyo vinamzuia Mafwele kuingia nchini Marekani na vinalenga kuhimiza uwajibikaji kwa wanaohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Juhudi za Mwananchi kumapata Mafwele kupitia simu yake ili aweze kuzungumzia hatua hiyo dhidi yake bado zinaendelea.
Mei 22, 2025, Mwangi na Agather, waliokamatwa na kudaiwa kuwekwa kizuizini nchini Tanzania, baadaye walipatikana mpakani kwenye nchi zao wakiwa na maumivu makali, kisha wakapata msaada wa kuwasafirisha hadi sehemu wanazotokea.
Wanaharakati hao walidai kuteswa na vyombo vya dola vya Tanzania ikiwamo unyanyasaji wa kingono na kupigwa, kabla ya kusafirishwa na kutelekezwa wakiwa na hali mbaya.
Awali, Mwangi, Agatha pamoja na wanaharakati wengine akiwemo Martha Karua, waliwasili nchini Tanzania kuhudhuria usikilizwaji wa kesi ya Uhaini ya Lissu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, lengo hilo liligonga mwamba baada ya kuzuiwa Uwanja wa Julius Nyerere (JNIA) na Martha na wenzake kurejeshwa makwao, huku huku Mwangi na Agatha wakidaiwa kuchukuliwa na kuwekwa kizuizini.
Baadaye Mwangi alisema aliondolewa nchini Tanzania na kusafirishwa kwa barabara hadi nchini Kenya ambako aliachwa eneo la Ukunda nchini humo.
Kwa upande wake, Agather alipatikana akiwa eneo la Mutukula lililopo katika mpaka wa Tanzania na Uganda usiku wa Alhamisi Mei 22, 2025.
Hata hivyo, akizungumza na kituo kimoja cha redio cha Kenya, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuhusu madai kuwa Mwangi na Agather waliteswa, alisema kama wamefanyiwa hivyo waende kushtaki katika mamlaka husika.
Muliro aliongeza kuwa madai yao ya kuteswa ni ya kiuanaharakati na ni maoni yao.
Kabla wanaharakati hao hawajapatikana, Mei 19, 2025, wakati wa uzinduzi wa Sera mpya ya mambo ya nje (Toleo la mwaka 2024) jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan alisema hataruhusu watu kutoka mataifa mengine kuvuruga amani ya nchi.
Alisema: “Tumeanza kuona mwenendo ambapo baadhi ya wanaharakati kutoka nchi jirani wanajaribu kuingilia mambo yetu. Kama wamekomeshwa kwao, basi wasije kuvuruga amani yetu hapa.”
Haina tija
Akizungumzia hatua ya Marekani kumwekea vikwazo Mafwele, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Denis Konga amesema haoni kama hatua hiyo ina uwajibikaji ndani yake kwa mhusika.
Amesema Mafwele ni mtu mdogo kwa sababu anapokea maelekezo kutoka kwa wakubwa zake ambao ni wanasiasa, hivyo kumwekea vikwazo yeye hakujagusa mzizi wa tatizo kwani vikwazo hivyo havitambadilisha tabia au kumwondoa kwenye nafasi yake.
“Sioni kama ina tija kwa sababu kama amezuiwa kwenda Marekani, utasikia ‘kwani Marekani ni wapi?’ lakini kama kungekuwa na hati ya mashitaka inayotaka kuwajibika kwa nchi wanachama waliosaini Rome Stature (mkataba wa Roma) ulioanzisha ICC, hiyo ingekuwa suala tofauti,” amesema Konga.
Hata hivyo, amesema kwenye uwanja wa diplomasia, vikwazo vinatumika kuona kama Serikali inaweza kuchukua hatua dhidi ya watu wanaotajwa kuhusika katika uvunjaji wa haki za binadamu, jambo ambalo haoni likitokea nchini.
“Kwa mtazamano wangu, uamuzi huu wa Marekani hauna tija, labda kama kuna hatua zaidi zinakuja kumshinikiza yeye na wengine kuwajibika,” amesema mwanazuoni huyo akisisitiza uwajibikaji katika vikwazo vyenyewe.
