Tirdo kuanzisha maabara ya Nishati na Madini NjombeTirdo kuanzisha maabara ya Nishati na Madini Njombe

Dodoma. Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) linatarajia kuanzisha Maabara ya Nishati na Madini katika Mkoa wa Njombe, hatua inayolenga kusogeza huduma karibu na maeneo yenye shughuli kubwa za uzalishaji na rasilimali za madini.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 22, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Waziri Kapinga amesema maabara hiyo itahudumia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Ruvuma, Mbeya na Rukwa. Aidha, maabara hiyo itafanya vipimo vya ubora wa makaa ya mawe, kemikali, madini pamoja na nishati mbadala ikiwemo biomasi na mkaa mbadala.

“Hadi Aprili 2026, Shirika limefanikiwa kumpata mzabuni wa kusambaza na kusimika vifaa vya kisasa pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalam watakaoendesha maabara hiyo,” amesema Kapinga.

Amesema kukamilika kwa maabara hiyo kutachochea uchumi wa viwanda unaozingatia matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema TIRDO inaendelea na mchakato wa kupata ithibati kwa maabara zake za mazingira, kemia, makaa ya mawe, mafuta na gesi ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.

Akizungumzia ubunifu na teknolojia, Kapinga amesema Wizara kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) imefanikiwa kuhawilisha teknolojia nane za uchakataji wa mazao na uzalishaji.

Teknolojia hizo ni pamoja na mashine za kutengeneza mkaa mbadala, kusafisha mafuta ya alizeti, kuzalisha chakula cha samaki, kubangua korosho, kukamua mafuta ya nazi pamoja na mashine za kusaga mawe yenye madini.

Pia amesema SIDO kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) imetengeneza mashine tatu za kuzalisha mkaa mbadala na kuanzisha teknolojia mpya kutoka Japan katika maeneo ya Ifakara, Kahama na Mwanjelwa.

Aidha, TIRDO imeendelea kutekeleza tathmini ya viwanda na kubaini fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Waziri Kapinga, tathmini hiyo inalenga kubaini idadi ya viwanda, ajira, uwezo wa uzalishaji, teknolojia zinazotumika pamoja na maeneo yenye fursa za uwekezaji ili kuchochea maendeleo ya viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.

Amesema shughuli hiyo imefanyika katika mikoa miwili mipya na kufanya jumla ya mikoa iliyofikiwa kufikia tisa ambayo ni Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Manyara, Mwanza na Shinyanga.

Kapinga amesema taarifa zote zilizokusanywa zimeingizwa katika mfumo wa kanzidata za viwanda ambapo hadi Aprili 2026 kulikuwa na viwanda 25,650 vilivyosajiliwa nchini.

Kati ya viwanda hivyo, 482 ni vikubwa, 625 vya kati, 8,980 vidogo na 15,563 ni viwanda vidogo sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *