
BODI ya Ligi Zanzibar (ZLB), imefuta matokeo ya mechi ya Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) kati ya Kipanga na Chipukizi United na kuzipiga faini ya Sh5 milioni baada ya kuibuka tuhuma za upangaji wa matokeo.
Taarifa iliyotolewa Mei 20, 2026 na ZLB kwa vyombo vya habari, ilieleza Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Bodi hiyo imebaini na kujiridhisha katika mechi hiyo kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni ya mashindano ya kuchafua, kuvuraga na upangaji wa matokeo uliofanywa na timu hizo.
Taarifa hiyo iliyotumwa na Ofisa Habari wa ZLB, Issa Chiwile, ilisema Kamati hiyo imetoa uamuzi huo kwa mujibu wa sura ya 23 (1)a,b,c,d na h ya kanuni ya mashindano ya mwaka 2025-2026. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi huo umetolewa baada ya kikao chake cha Mei 18, 2026 na mechi hiyo iliyochezwa Mei 15, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, ilimalizika kwa Chipukizi kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
“Kamati imepitia ripoti ya wasimamizi wa mchezo huo, imebaini na kujiridhisha kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni ya kuchafua, kuvuruga na upangaji matokeo uliofanywa na timu zote mbili, kitendo ambacho ni kosa,” ilisema taarifa hiyo.
Pia, ilieleza timu hizo zimetozwa faini kwa kosa la kupanga matokeo kwenye mchezo huo.
Vilevile, Kiongozi Mwandamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Kassim Moh’d Abdulla, shauri lake limepelekwa kwenye kamati ya maadili kwa kosa la kujihusisha na ukiukwaji wa kanuni.
Taarifa hiyo ilisema kitendo hicho ni kinyume na utaratibu wa kiongozi wa ZFF na kanuni ya mashindano na uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa sura 32(2).
Pia, Kamati hiyo ilisema inaendelea na uchunguzi zaidi wa shauri hilo na kila atakayehusika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni ya mashindano ya 2025-2026.
