
Zaidi ya watu 2,000 walihudhuria mazishi yaliyofanyika jana Alhamisi ya wahanga watatu wa shambulio dhidi ya msikiti na Kituo cha Kiislamu huko San Diego, California, huku kukiwa na huzuni kubwa zilizoandamana na pongezi kwa kujitolea wahanga hao waliowalinda watoto zaidi ya 140 waliokuwa ndani ya shule ya kituo hicho.
Waislamu watatu waliuawa katika shambulio hilo, akiwemo mlinzi ambaye alifanikiwa kutuma ujumbe wa kuomba msaada kupitia chombo cha mawasiliano (Radio Call) ili kuzindua taratibu za kufungwa njia za kuelekea kwenye Kituo cha Kiislamu cha San Diego kabla ya kukabiliana na washambuliaji waliolenga msikiti mkubwa zaidi wa jiji hilo.
Waombolezaji walijipanga kwenye bustani kwa ajili ya Swala ya Maiti ya wanaume hao watatu, ambao wametajwa kama mashujaa, kwa sababu waliwazuia washambuliaji kumwaga damu zaidi wakati watoto wakikuwa shuleni na msikitini.
Shambulio na mauaji hayo yaliyofanywa na vijana wawili waliojulikana kwa majina ya Caleb Velasquez na Cain Clark, yamewatia wasiwasi mkubwa Waislamu kote nchini Marekani huku chuki dhidi ya Uislamu ikiendelea kuongezeka.
Polisi wamesema mlinzi wa Kituo cha Kiislamu cha San Diego huko California, Amin Abdullah, alipigwa risasi na kuuawa katika mapigano ya risasi na washambuliaji hao vijana.
Wengine waliouawa katika hujuma hiyo dhidi ya msikiti na Kituo cha kiislamu cha San Diego ni Mansour Kaziha, 78, mfanyakazi wa matengenezo na mpishi wa kituo hicho, na dereva wa Uber, Nadir Awad, aliyekuwa na umri wa miaka 57, jirani ambaye mke wake anafanya kazi kama mwalimu shuleni hapo. Alikamatwa na kupigwa risasi hadi kufa katika eneo la kuegesha magari.
Polisi ya Marekani inasema mlinzi, Abdullah aliwazuia washambuliaji kuingia kwenye kituo hicho cha Kiislamu, ambapo wanafunzi 140 walijificha kwenye kabati na sehemu zingine.
Taarifa ya polisi imeongeza kwamba, washambuliaji walikimbia kutoka msikitini hapo kwa kutumia gari lao, na baadaye walipatikana wamekufa ndani ya gari kutokana na majeraha ya kujipiga risasi.
Kituo cha Kiislamu cha San Diego ndicho kikubwa zaidi katika kaunti hiyo na kina msikiti mkubwa zaidi. Kwa mujibu wa tovuti yake, pia kinajumuisha taasisi za elimu, ikiwamo Shule ya Al-Rashid, ambayo hutoa masomo ya Kiislamu na Kiarabu, na kuhifadhi Qur’ani.
