
Picha mpya za satalaiti zilizochambuliwa zimefichua uharibifu na hasara kubwa iliyotokea katika vituo vingi vya kijeshi vya Israel kufuatia mashambulizi na operesheni za kujihami za Iran na harakati ya Lebanon Hizbullah na hivyo kuzusha maswali kuhusu ukubwa wa uharibifu ambao Tel Aviv inauficha mbele ya umma.
Uchambuzi uliofanywa wa picha za satalaiti na kuchapishwa na kampuni ya usafiri wa anga (Soar) unaonyesha athari za mashambulizi yaliyofanywa katika vituo kadhaa vya kijeshi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za palestina (Israel) katika operesheni za kujihami za Iran kwa jina Oparesheni ya Ahadi ya Kweli-4 yaliyofanywa kulipiza kisasi mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel yalianza kwa kuwaua shahidi maafisa wa ngazi ya juu wa Iran akiwemo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Iran ilijibu hujuma hiyo kwa mashambulizi makubwa na angamizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani na Israel na maslahi mengi ya pande hizo katika Mashariki ya Kati.
Ripoti ya Yedioth Ahronoth, iliyotolewa leo Ijumaa kwa idhini ya udhibiti wa kijeshi, imetumia picha zenye viwango vya chini, na hivyo kutilia shaka pakubwa uwazi wa serikali kuhusu kiwango halisi cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Iran.
Wakati huo huo, picha kutoka satalaiti ya Sentinel-2 zinaonyesha kuwa kambi ya jeshi la anga ya Ramat David ilipigwa katika maeneo mawili tofauti katika mashambulizi ya Iran.
Kwa mujibu wa uchambuzi huo, eneo moja lililoharibiwa ndani ya kambi hiyo ya jeshi la anga lilikuwa na magari na vifaa vya kilojistiki, na eneo la pili lilikuwa likitumika kama kituo cha kuongeza mafuta na kutoa huduma kwa ndege za kivita, kuhifadhi miundombinu muhimu na kwa ajili ya operesheni za anga za Israel.
