
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP, nchini Tanzania limefanya utafiti wa kubainisha vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya Bonde la Ziwa Victoria kwa upande wa Tanzania ili kufanya uchechemuzi wa kuhifadhi mazingira na kufungua fursa za uchumi wa kijani au usioharibu mazingira na ule wa buluu utokanao na shughuli za baharini na ziwani kupitia utalii wa ziwa hilo hususan kwa wanawake na vijana.
Vivutio 40 vyabainishwa katika utafiti
Utafiti huo uliofanyika katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu na Geita kwa ushirikiano na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), tawi la Mwanza, umebainisha takribani vivutio vya utalii 40 zikiwemo fukwe, hifadhi za wanyamapori, migodi ya madini, historia za kale, uvuvi na safari za majini.
UNDP: Utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa maendeleo
Mkurugenzi wa Miradi ya UNDP nchini Tanzania, Amon Manyama, amesema kuna uhusiano mkubwa kati ya utunzaji wa mazingira ya Ziwa Victoria na maendeleo ya watu zaidi ya milioni 45 wanaonufaika na ziwa hilo.
“Kutunza mazingira kwa mfano, fukwe zote za ziwa zitunzwe vizuri zisiharibiwe. Pia visiwa vilivyopo katika wilaya mbalimbali vina haja ya kulindwa ili viendelee kutoa manufaa kwa wananchi kupitia chakula, biashara na mazingira bora,” amesema.
Ripoti yabaini uchafuzi mkubwa wa maji
Ripoti mpya ya hali ya Ziwa Victoria iliyowasilishwa katika jukwaa hilo imeonesha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha uchafuzi wa maji katika maeneo mbalimbali ya ziwa na fukwe zake.
Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni uwepo wa kemikali hatarishi kama zebaki, taka ngumu, plastiki pamoja na maji taka yanayotiririka kutoka kwenye makazi ya watu na viwandani.
Wito wa kudhibiti taka za plastiki
Kuhusu tatizo la plastiki, Bw. Manyama amesema kuna haja ya kuwa na mifumo madhubuti ya ukusanyaji na urejelezaji wa taka.
Amesema teknolojia zilizopo sasa zinaweza kusaidia kuzalisha mbolea na bidhaa nyingine kutokana na taka huku akisisitiza umuhimu wa kuchakata maji taka kutoka majumbani na viwandani kabla hayajaingia ziwani.
Mkakati wa kuendeleza utalii waendelea
UNDP kwa sasa inashirikiana na viongozi wa serikali za mikoa, wilaya pamoja na wadau wengine kukusanya maoni ya wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki katika shughuli za utalii na changamoto zinazowakabili.
“Tuko katika hatua ya kutengeneza mkakati na tunashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii Kanda ya Ziwa pamoja na wadau wengine,” amesema Bw. Manyama.
Jukwaa la wadau
Jukwaa hilo la wadau wa maendeleo limeratibiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria kuelekea uzinduzi na maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria yaliyofanyika Mei 21 jijini Mwanza, yakihudhuriwa na viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.