UNDP Kutumia utalii wa Ziwa Victoria kuhifadhi mazingira na kukuza uchumi UNDP Kutumia utalii wa Ziwa Victoria kuhifadhi mazingira na kukuza uchumi 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP, nchini Tanzania limefanya utafiti wa kubainisha vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya Bonde la Ziwa Victoria kwa upande wa Tanzania ili kufanya uchechemuzi wa kuhifadhi mazingira na kufungua fursa za uchumi wa kijani au usioharibu mazingira na ule wa buluu utokanao na shughuli za baharini na ziwani kupitia utalii wa ziwa hilo hususan kwa wanawake na vijana.

© UNDP Tanzania UNDP Tanzania wanazindua mafunzo kwa wananchi kwa ajili ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya Ziwa Victoria kwa utalii ili kukuza ustawi wa mazingira.

Vivutio 40 vyabainishwa katika utafiti

Utafiti huo uliofanyika katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu na Geita kwa ushirikiano na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), tawi la Mwanza, umebainisha takribani vivutio vya utalii 40 zikiwemo fukwe, hifadhi za wanyamapori, migodi ya madini, historia za kale, uvuvi na safari za majini.

UNDP: Utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa maendeleo

Mkurugenzi wa Miradi ya UNDP nchini Tanzania, Amon Manyama, amesema kuna uhusiano mkubwa kati ya utunzaji wa mazingira ya Ziwa Victoria na maendeleo ya watu zaidi ya milioni 45 wanaonufaika na ziwa hilo.

“Kutunza mazingira kwa mfano, fukwe zote za ziwa zitunzwe vizuri zisiharibiwe. Pia visiwa vilivyopo katika wilaya mbalimbali vina haja ya kulindwa ili viendelee kutoa manufaa kwa wananchi kupitia chakula, biashara na mazingira bora,” amesema.

Ripoti yabaini uchafuzi mkubwa wa maji

Ripoti mpya ya hali ya Ziwa Victoria iliyowasilishwa katika jukwaa hilo imeonesha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha uchafuzi wa maji katika maeneo mbalimbali ya ziwa na fukwe zake.

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni uwepo wa kemikali hatarishi kama zebaki, taka ngumu, plastiki pamoja na maji taka yanayotiririka kutoka kwenye makazi ya watu na viwandani.

© UNDP Tanzania UNDP Tanzania wanazindua mafunzo kwa wananchi kwa ajili ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya Ziwa Victoria kwa utalii ili kukuza ustawi wa mazingira.

Wito wa kudhibiti taka za plastiki

Kuhusu tatizo la plastiki, Bw. Manyama amesema kuna haja ya kuwa na mifumo madhubuti ya ukusanyaji na urejelezaji wa taka.

Amesema teknolojia zilizopo sasa zinaweza kusaidia kuzalisha mbolea na bidhaa nyingine kutokana na taka huku akisisitiza umuhimu wa kuchakata maji taka kutoka majumbani na viwandani kabla hayajaingia ziwani.

Mkakati wa kuendeleza utalii waendelea

UNDP kwa sasa inashirikiana na viongozi wa serikali za mikoa, wilaya pamoja na wadau wengine kukusanya maoni ya wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki katika shughuli za utalii na changamoto zinazowakabili.

“Tuko katika hatua ya kutengeneza mkakati na tunashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii Kanda ya Ziwa pamoja na wadau wengine,” amesema Bw. Manyama.

Jukwaa la wadau 

Jukwaa hilo la wadau wa maendeleo limeratibiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria kuelekea uzinduzi na maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria yaliyofanyika Mei 21 jijini Mwanza, yakihudhuriwa na viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *