Dar es Salaam. Wakati idadi ya wanawake wanaoshika nafasi za juu za uongozi nchini ikiendelea kuongezeka katika sekta binafsi na taasisi za umma, wanawake viongozi wametakiwa kuimarisha mshikamano kwa kuwa sehemu ya jukwaa litakalowawezesha kushirikishana uzoefu, changamoto na mbinu za kukabiliana na mazingira magumu ya kiuongozi.
Wito huo umetolewa leo Mei 22, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Women CEO Roundtable, Emma Kawawa, wakati wa mkutano uliowakutanisha wanawake viongozi kutoka sekta mbalimbali wakiwemo wakurugenzi wakuu, mameneja na watendaji wa taasisi za umma na binafsi.
Kawawa amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za maamuzi, bado wanawake wengi wanaokabidhiwa majukumu ya juu hukutana na changamoto zinazohitaji msaada wa kitaaluma, ushauri na hata faraja ya kisaikolojia kutoka kwa wanawake wengine waliopitia mazingira kama hayo.
Amesema wanawake wengi wanapofikia nafasi za juu za uongozi hujikuta wakibeba changamoto nyingi peke yao kutokana na ushindani uliopo sehemu za kazi au hofu ya kuonekana dhaifu wanapozungumzia changamoto wanazopitia.
Baadhi ya wanawake viongozi walioshiriki kwenye mkutano uliowakutanisha wanawake viongozi kutoka sekta mbalimbali.
“Ni muhimu wanawake viongozi kuwa na jukwaa la pamoja litakalowezesha kushirikishana uzoefu, changamoto na hata mbinu za namna ya kuhimili presha za kiuongozi. Hii itasaidia kujenga kujiamini na kuongeza ufanisi katika kazi,” amesema Kawawa.
Kwa mujibu wa Kawawa, majukwaa hayo yanaweza kuwa sehemu salama kwa wanawake viongozi kujifunza kutoka kwa uzoefu wa wenzao, kujenga mitandao ya kitaaluma na kusaidiana katika safari ya uongozi.
“Wapo wanawake wanaobeba changamoto nyingi kimya kimya kwa sababu hawana sehemu ya kuzungumza na wengine waliopo kwenye nafasi kama zao. Haya majukwaa yanaweza kuwa sehemu ya kujengana na kutiana moyo,” amesema Kawawa.
Aidha, amesema uwepo wa wanawake waliopata mafanikio kwenye nafasi mbalimbali za uongozi unaweza kuwa chachu ya kuwahamasisha wanawake wengine kuthubutu kuwania nafasi za juu zaidi katika taasisi na kampuni.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa jukwaa hilo, Dk Salha Mohamed Kassim amesema majukwaa ya wanawake viongozi yana mchango mkubwa katika kuwajengea wanawake uwezo wa kuhimili changamoto za kiuongozi na kuongeza ushirikiano baina yao.
“Hili ni jukwaa linalowawezesha wanawake viongozi kukutana, kubadilishana mawazo na kupeana nguvu katika safari ya uongozi. Kupitia jukwaa hili tunaweza kujifunza kutoka kwa uzoefu wa wengine na kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazotukabili,” amesema Dk Salha.
Ameongeza kuwa jukwaa hilo pia linalenga kuhakikisha wanawake viongozi wanaendana na kasi ya mabadiliko ya dunia ya sasa kwa kuhamasishana kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na kujiendeleza kitaaluma.
Amesema Tanzania imeendelea kutoa nafasi kubwa kwa wanawake kushiriki katika nafasi za maamuzi na wanawake wengi wameonyesha uwezo mkubwa wanapopewa nafasi hizo.
Amefafanua kuwa hatua hiyo ni ishara ya mabadiliko chanya katika usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake, huku akisisitiza umuhimu wa wanawake kutumia nafasi hizo kuleta matokeo yenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, amewataka wanawake viongozi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo.
“Mwanamke akipewa nafasi anaweza. Tunataka tuungane pamoja kupitia jukwaa hili ili tuendelee kusonga mbele na kuacha alama nzuri katika taasisi tunazoziongoza,” amesema.
