Dk Possi: Mawakili wa Serikali wana nafasi muhimu kufanikisha Dira 2050Dk Possi: Mawakili wa Serikali wana nafasi muhimu kufanikisha Dira 2050

Arusha. Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi amesema mawakili wa Serikali wana nafasi muhimu katika kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inafikiwa kwa kusimamia kitaalamu uwekezaji, mikataba na kulinda rasilimali za Taifa.

Dk Possi amesema hayo leo Mei 22, 2026 jijini Arusha katika mkutano mkuu wa watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, akieleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo hivyo kuna umuhimu wa kuwashirikisha mawakili wa Serikali katika hatua zote za utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema mawakili wa Serikali siyo tu wana jukumu la kuendesha mashauri mahakamani, bali pia kuzuia migogoro isitokee kwa kutoa ushauri wa kisheria mapema katika hatua za maandalizi ya mikataba na utekelezaji wa miradi.

“Nafahamu Serikali inawekeza sana katika uwekezaji na mawakili wa Serikali tuna nafasi kubwa sana kuhakikisha dhima na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inafikiwa,” amesema Dk Possi.

Amesema katika uwekezaji kuna eneo muhimu la usimamizi wa mikataba (contract management) ambalo linahitaji ushiriki mkubwa wa mawakili wa Serikali ili kuhakikisha masilahi ya Taifa yanalindwa kitaalamu.

“Masuala ya contract management ni muhimu sana. Ni vizuri Wizara ya Katiba na Sheria ikaangalia namna mawakili wa Serikali watakavyoweza kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unasimamiwa kitaalamu,” amesema.

Dk Possi amesema baadhi ya taasisi na viongozi bado hawawashirikishi wanasheria katika hatua za uundaji wa mikataba, maandalizi ya nyaraka na utekelezaji wa miradi, hali inayosababisha migogoro mingi ya kisheria ambayo ingeweza kuzuilika mapema.

“Kuna wakati wakili hashirikishwi katika hatua za makubaliano, lakini mgogoro ukitokea ndipo wanaambiwa peleka kwa Wakili Mkuu wa Serikali, wakati jambo hilo lingeweza kuzuiwa mapema,” amesema.

Wakili Mkuu huyo amesema ni muhimu viongozi wa taasisi za umma  kutambua kuwa mawakili wa Serikali wanapaswa kushirikishwa katika kila hatua ya miradi mikubwa ya maendeleo na uwekezaji ili kupunguza migogoro na hasara kwa Serikali.

“Hii yote ni kwa sababu Rais alituambia sisi mawakili wa Serikali ni askari wa kalamu, tuna jukumu la kulinda rasilimali za nchi yetu,” amesema

Aidha, Dk Possi alisema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itaendelea kuwekeza katika kukuza weledi, ujuzi na utaalamu wa watumishi wake ili kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa.

“Sisi tumeona hatuwezi kuacha kukuza weledi, ujuzi na utaalamu katika kila nyanja. Jukumu letu ni kubwa, siyo tu uendeshaji wa mashauri bali pia usimamizi na uratibu wa masuala mbalimbali ya Serikali,” amesema

Amesema tayari ofisi hiyo imeanza mafunzo ya kisheria kwa watumishi wake tangu mwanzoni mwa wiki kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kuomba Wizara ya Katiba na Sheria kuangalia uwezekano wa kupanua Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutokana na ongezeko la mahakama na huduma za kisheria nchini.

Kuhusu maendeleo ya teknolojia, Dk Possi amesema ofisi hiyo imeendelea kuwekeza katika Tehama na matumizi ya akili bandia (AI) ili kuwawezesha mawakili wa Serikali kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia.

“Tehama ndiyo dunia ya sasa na AI ni jambo ambalo lazima tutaishi nalo kama nchi. Hatuna budi kuangalia maendeleo ya teknolojia ili mawakili wetu waweze kuendana na mwenendo wa dunia,” amesema

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Franklin Rwezimula, aliwataka watumishi wa Ofisi hiyo kuendelea kuzingatia weledi, maadili na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi wa huduma za kisheria na kulinda maslahi ya taifa.

Amesema kupitia mkutano huo, washiriki watapata mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku pamoja na kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ushindani wa kiuchumi na mahitaji ya sasa ya utumishi wa umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *