
Dar/Mara. Kwanini alikamatwa? Ndilo swali linalogonga vichwa vya mawakili nchini, baada ya mwenzao, Leonard Magwayega, kukamatwa na polisi mjini Tarime mkoani Mara, muda mfupi baada ya washitakiwa aliokuwa akiwatetea kuachiwa huru.
Taarifa za kukamatwa kwa wakili huyo zilitolewa kupitia akaunti ya X (zamani Twitter) leo na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, akinukuu ujumbe aliotumiwa na Magwayega baada ya kukamatwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tarime, Mark Njera amesema hajapata taarifa kamili kuhusu tukio hilo, lakini ameahidi kufuatilia na kutoa taarifa kwa umma.
“Kwa kweli sina taarifa hiyo kwa sasa, kwanza nipo safari. Ngoja nifuatilie kwa mtu aliyekuwepo ofisini ili kujua ukweli,” amesema Kamanda Njera, lakini alipotafutwa tena hakupatikana hadi habari hii inaandikwa.
Akitoa taarifa kwa Rais wa TLS, wakili Magwayega amedai alikamatwa na polisi mjini Tarime wakati akitekeleza majukumu yake ya uwakili kwa watuhumiwa waliokuwa wakikabiliwa na Shauri la Jinai namba 1812/2026 lililohusiana na matukio ya Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa aliyomwandikia Rais wa TLS, wakili huyo amedai alikamatwa Ijumaa Mei 22, 2026 baada ya watuhumiwa 17 aliokuwa akiwatetea kuachiwa huru huku polisi wakimtuhumu kuwasaidia kutoroka wakiwa bado wanakabiliwa na kesi nyingine ya jinai.
“Katika utekelezaji wa jukumu langu la uwakili kwa watuhumiwa wa matukio ya Oktoba 29, 2025, leo Mei 22, 2026 nimekamatwa na Jeshi la polisi mjini Tarime baada ya watuhumiwa 17 kuachiwa huru katika Shauri la Jinai namba 1812/2026.”
Wakili huyo ameeleza kuwa, polisi wanadai aliwasaidia watuhumiwa hao kutoroka huku wakiwa bado wana kesi ya uhaini inayowakabili, wakati shauri lililokuwa likiwakabili washitakiwa likisikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime.
Wakili huyo amesema hakuhusika kwa namna yoyote katika tukio hilo, akidai kuwa Jeshi la Polisi lilikuwepo wakati watuhumiwa hao walipoondoka, lakini bado likaamua kumuweka chini ya ulinzi kwa kumtuhumu kuwatorosha.
“Sikufanya jambo hilo. Hata hivyo, kwa sababu zinazojulikana zaidi na Jeshi la Polisi, ambalo lilikuwepo wakati watuhumiwa hao walipoondoka, waliamua kuniweka chini ya ulinzi wa polisi.”
Wakili Magwayega amedai alizuiwa katika Kituo cha Polisi Tarime kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni kabla ya kuachiwa kwa dhamana ya polisi, akitakiwa kuripoti katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Tarime siku ya Jumatatu Mei 25, 2026 saa 2:00 asubuhi.
“Nimewasilisha taarifa hii mheshimiwa Rais Mwabukusi,” amesema wakili huyo mwenye namba ya uwakili (Roll number 2897) ambapo kupitia ukurasa huo, Rais wa TLS ambaye pia ni wakili aliandika “Tutachukua hatua.”
Wadau walaani
Akieleza msimamo wake baada ya kuipokea taarifa hiyo, Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi amesema chama hicho hakitakubali kuona mawakili nchini wakinyanyaswa wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria na Kikatiba.
Amesema hatua stahiki zitachukuliwa baada ya viongozi wa chama hicho kukubaliana hatua za kuchukua kutokana na tukio hilo huku akitoa wito kwa Jeshi la Polisi kujiepusha na unyanyasaji wa mawakili wawapo katika majukumu yao.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kuachana na unyanyasaji huu na zaidi TLS itakaa kutathmini jambo hili na kuchukua hatua stahiki,” amesema katika taarifa yake.
Akizungumza na Mwananchi, wakili ambaye pia ni mwanachama wa TLS (akiomba jina lake lisitajwe) aliyehusika kusimamia kupatikana dhamana kwa Wakili Magwayega, ameeleza kushitushwa na uamuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi, kumkamata wakili mwenzao akiwa anatekeleza majukumu yake.
Amesema jukumu la ulinzi wa washtakiwa wanapokuwa mahakamani ni la askari polisi na si la wakili, hivyo kitendo cha kumkamata wakili na kudai anahusika na watuhumiwa kutoroka ni kinyume cha sheria na taratibu.
“Mawakili wa Serikali walitakiwa kuwasiliana na askari polisi ili kuimarisha ulinzi kwani wao walijua dhahiri kuwa watuhumiwa wale licha ya kufutiwa shitaka moja bado walikuwa na mashtaka mengine,” ameeleza.
Amesema askari polisi waliokuwepo mahakamani hapo ndio wanaostahili kuchukuliwa hatua kwa kushindwa kutimiza wajibu wao na si vinginevyo.
“Baada ya kukamatwa tulishughulikia suala la dhamana na kufanikiwa kumtoa; anatakiwa kuripoti tena polisi Jumatatu Mei 25, 2026 lakini hii sio sawa. Wakili jukumu lake lilikuwa kuwatetea wateja wake, jukumu alilolitekeleza vizuri,” ameongeza wakili huyo ambaye amesema yeye sio msemaji.
Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa amelaani kitendo hicho akitoa wito kwa Mahakama kukemea na kukataza matukio ya namna hiyo kwa mawakili.
“Tunalaani kabisa matukio hayo ya mawakili kukamatwa wakiwa katika majukumu yao. Tunataka polisi waache mara moja kusumbua mawakili, wakili ni mtumishi wa Mahakama anaisaidia Mahakama kufanya kazi zake. Tunategemea Mahakama pia itasema na kukemea matendo ya mawakili kusumbuliwa wakiwa katika kazi zao,” amesema.
Ameonya kuwa, kuendelea kujirudia kwa matukio hayo kunaichafua Mahakama ambayo ndiyo sehemu ya ulinzi na utetezi wa haki za binadamu, akisema kuwa kitendo cha polisi kuwashambulia watumishi wa Mahakama wakiwa katika majukumu yao hakuleti picha nzuri.
Katika siku za hivi karibuni, hili limekuwa tukio la pili kwa mawakili kukumbana na sintofahamu na Jeshi la Polisi. Tukio jingine lilitokea Septemba 15, 2025 Wakili Deogratias Mahinyila, alijikuta katika mvutano na maofisa wa Jeshi la Polisi akiwa anatekeleza majukumu yake katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Katika kadhia hiyo, wakili Mahinyila alikamatwa na polisi kisha kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, kabla ya kuachiwa kwa dhamana baadaye siku hiyo hiyo, huku akitakiwa kuripoti kituoni hapo.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Denis Konga amesema kuwa mwendelezo wa vitendo vya polisi kuvutana na mawakili mahakamani kunajenga picha mbaya ya kutoheshimiwa kwa mhimili wa Mahakama.
“Matendo haya yanaashiria kutoheshimiana kwa mihimili ya Serikali, mbaya zaidi ni kwamba mhimili wa Mahakama ndio hutoa haki, ikiwa mhimili huo unadharauliwa hadi mawakili wanaweza kukamatwa wakiwa kwenye majukumu yao, inaweza kuondoa imani ya jamii kuhusu utetezi wa haki zao.
“Mawakili hawawajibiki kulinda watu mahakamani, hakuwafungulia mlango wala pingu, unamkamate kwamba amehusika kuwatorosha wakati wapo mahakamani,” amehoji Konga.
Amesema tatizo hilo linahitaji kuangaliwa upya sheria inayoruhusu askari kukamata mawakili wakiwa katika majukumu yao ili kuondoa sintofahamu inayochafua mhimili wa Mahakama kwa kuingiliwa na mamlaka zingine.
