Wakulima Simiyu wataka mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabianchiWakulima Simiyu wataka mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabianchi

Simiyu. Wakulima wa mahindi mkoani Simiyu wamewataka wadau wa kilimo, kampuni za mbegu na taasisi za utafiti kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zinazostahimili ukame na mabadiliko ya tabianchi ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kuimarisha usalama wa chakula kwa familia zao.

Wakizungumza Mei 22, 2026 katika Kijiji cha Giriku kwenye sherehe za mavuno zilizoambatana na ngoma za asili za Kisukuma, mbina, wakulima hao wamesema mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha mvua kutotabirika yamekuwa chanzo cha hasara kubwa kwa wanaotumia mbegu za kawaida au za asili zisizohimili ukame.

Magasha Malimi, mkulima katika Kijiji cha Majahida wilayani Bariadi, amesema wanahitaji mbegu zinazoendana na mazingira ya sasa ili kuongeza tija mashambani.

“Hali ya hewa imebadilika sana. Zamani mvua zilikuwa zinajulikana, lakini sasa hazitabiriki. Tunahitaji mbegu bora zinazowahi kukomaa na zinazohimili ukame ili tusipate hasara kila msimu,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bayer Tanzania, Mwinyi Sango, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika kijiji cha Giriku, mkoani Simiyu, kuhusu uzalishaji wa mbegu bora za mahindi kwa ajili ya kuimarisha kilimo cha zao hilo. Picha na Samwel Mwanga.

Naye Neema Daud kutoka Kijiji cha Lugulu wilayani Itilima amesema gharama za kilimo zimeongezeka, hivyo ni muhimu wakulima kupata mbegu bora zinazoweza kuongeza mavuno hata katika maeneo madogo.

“Tunatumia fedha nyingi kulima, lakini wakati mwingine tunavuna kidogo kutokana na ukame. Tukipata mbegu bora tunaweza kuvuna zaidi hata kwa ekari chache,” amesema.

Kwa upande wake, Shitebo Jiganga kutoka Kijiji cha Malita wilayani Maswa amesema pamoja na kuwepo kwa aina mbalimbali za mbegu bora, bado changamoto ya upatikanaji na gharama zake inaendelea kuwaathiri wakulima wengi vijijini.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bayer Tanzania, Mwinyi Sango amesema kampuni hiyo inaendelea kuzalisha mbegu bora za mahindi zinazolenga kumsaidia mkulima kupata mavuno mengi licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Ofisa ugani wa Bayer Life Science Tanzania, Sylivesta Mihayo, akitoa elimu ya kilimo bora cha mahindi katika shamba darasa kwa wakulima (hawapo pichani) katika kijiji cha Giriku, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu. Picha na Samwel Mwanga.

“Sisi tupo hapa kusherehekea na wakulima wetu baada ya mavuno. Tunaamini kilimo bora kinaanza na mbegu bora. Pia, maofisa ugani wetu kwa kushirikiana na wale wa Serikali wanaendelea kuwa karibu na wakulima ili kuhakikisha wanalima kwa tija,” amesema.

Amesema ubora wa mbegu wanazozalisha una uhakika wa kuota vizuri na kumpatia mkulima mavuno bora na mengi.

Kwa upande wake, mtafiti wa Bayer Tanzania, Maduka Joseph amesema matumizi ya mbegu zilizoboreshwa ni njia muhimu ya kuongeza uzalishaji wa mahindi na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

“Sisi tunazalisha mbegu zinazoendana na mazingira yaliyobadilika. Kuna mbegu zinazokomaa mapema na zinazostahimili ukame, hivyo mkulima akifuata kanuni za kilimo anaweza kupata mavuno makubwa zaidi,” amesema.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa baadhi ya mbegu zilizoboreshwa zina uwezo wa kuhimili ukame, magonjwa pamoja na kuongeza mavuno kwa hekta, huku aina kadhaa zilizofanyiwa utafiti nchini zikionyesha uwezo mkubwa wa kustahimili mazingira magumu ya uzalishaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *