
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameyatupilia mbali madai ya Marekani kuhusu shambulio la ndege zisizo na rubani (drone) dhidi ya kinu cha kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia cha Barakah nchini Falme za Kiarabu (UAE). Amesema kuwa Washington imetumia vibaya Baraza la Usalama ili kusambaza tuhuma za uongo dhidi ya Iran na mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani.
Katika barua zinazofanana zilizoelekezwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, na Rais wa zamu wa Baraza la Usalama, Fu Cong, Amir Saeid Iravani amesema kuwa Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, wakati wa kikao cha Baraza la Usalama kilichofanyika Mei 19 chini ya ajenda ya “Hali katika Mashariki ya Kati,” aliishutumu Iran kwa njia isiyo sahihi kuwa eti ilihusika na shambulio hilo, bila kutoa ushahidi wowote uliothibitishwa.
Barua hiyo inasema, “Iran inakataa katakata madai haya. Iran yenyewe imekuwa mwathiriwa wa mashambulizi na vitendo vya uchokozi kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vyake vya nyuklia vya amani vilivyo chini ya uangalizi wa kimataifa.”
Mwanadiplomasia huyo mwandamizi amebainisha zaidi kuwa Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza msimamo wake wa kimsingi na usio na shaka kwamba shambulio lolote au tishio dhidi ya vituo vya nyuklia vya amani ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Katiba na maazimio ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Aidha, ametoa onyo mara kwa mara kuhusu madhara mabaya ya kibinadamu, kimazingira, na ki-radiolojia yanayoweza kutokana na vitendo hivyo vya kiholela na visivyo halali.
Iravani amekumbusha kuwa Marekani ni nchi pekee kuwahi kutumia silaha za nyuklia na pia ikiwa pamoja na utawala wa Kizayuni, ilishambulia ya vituo vya nyuklia vya Iran.
Amesema kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia vituo vya nyuklia vya Iran vyenye malengo ya amani katika ameneo ya Natanz, Fordow, Isfahan, na Bushehr wakati wa vita vya kichokozi vya Juni 2025 na Februari 2026. Amesema hujuma hizo ni ukiukwaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, sheria za kimataifa za kibinadamu, Katiba ya IAEA, na maazimio husika ya IAEA.
Balozi huyo wa Iran ameisifu Jamhuri ya Kiislamu kama nchi inayoshikamana na Mkataba wa Kutoeneza Silaha za Nyuklia (NPT).