
Dar es Salaam. Katika jamii nyingi, ndoa na uhusiano huonekana kama maeneo ya wenza kujitoa bila kuuliza maswali.
Wengi hufundishwa kuwa kumpenda mtu ni kuvumilia kila kitu, hata pale utu, amani na heshima vinapokanyagwa. Mtazamo huu umechangia migogoro mingi ya ndoa, maumivu ya kihisia na uhusiano usio na afya.
Ukweli ni kwamba upendo wa kweli hauishi kwa kujikana, bali kwa kujitambua. Ndipo dhana ya mipaka inapopata nafasi yake.
Waandishi Henry Cloud na John Townsend katika kitabu chao: Boundaries in Dating wanaeleza kuwa mipaka hutusaidia kuelewa wajibu wetu unaanzia na unaishia wapi.
Bila mipaka, mtu hujikuta anaishi maisha ya mwingine badala ya yake mwenyewe. Katika ndoa au uhusiano, hali hii husababisha lawama, chuki za kimya kimya na hisia za kutothaminiwa.
Mipaka ni nini katika muktadha wa uhusiano
Mipaka si ukuta wa kuzuia upendo, bali ni mstari unaolinda utu. Ni uwezo wa mtu kusema hapana bila kujilaumu na kusema ndiyo bila kulazimishwa.
Ni uelewa wa ndani unaokusaidia kutambua unachokubali, unachohitaji na kile kinachokuvuka mipaka. Uhusiano wenye mipaka huwa na mawasiliano ya wazi, heshima ya pande zote na uwajibikaji.
Mtaalamu wa masuala ya ndoa, Dk John Gottman, anaeleza kuwa ndoa zinazodumu si zile zisizo na migogoro, bali ni zile zinazojua jinsi ya kushughulikia tofauti kwa heshima. Heshima hiyo huanza pale kila upande unapojua mipaka yake na ya mwenzake.
Changamoto ya kujitoa kupita kiasi
Katika mazingira mengi, hasa kwa wanawake, kujitoa kupita kiasi huonekana kama ishara ya upendo au utii.
Mtu anaweza kuacha ndoto zake, sauti yake na hata uamuzi wake kwa jina la ndoa. Hatua kwa hatua, anajikuta amechoka, ana hasira isiyoelezeka na anahisi kupotea.
Erich Fromm, mwandishi wa Kitabu: The Art of Loving, anaonya kuwa upendo usio na uhuru huacha kuwa upendo na kuwa utegemezi.
Kujua mipaka hakumaanishi kumpenda mwenzako kidogo, bali ni kujipenda vya kutosha ili upendo wenu uwe wa kweli. Mtu asiye na mipaka mara nyingi hubeba majukumu yasiyo yake, hutatua matatizo ya mwenzake na hatimaye humlaumu pale mambo yanapoharibika.
Mipaka katika mawasiliano
Maneno yanayotamkwa ndani ya ndoa yana nguvu kubwa. Kuna uhusiano inaovunjwa si kwa kukosa mapenzi, bali kwa lugha kali, dharau na mawasiliano yasiyo na mipaka.
Mipaka katika mawasiliano inamaanisha kukataa matusi, vitisho na maneno yanayodhalilisha utu. Inamaanisha pia kujua lini uongee na lini unahitaji nafasi ya kutulia.
Marshall Rosenberg, mwandishi wa Kitabu: Nonviolent Communication, anaeleza kuwa mawasiliano bora hutokea pale mtu anapoongea ukweli wake bila kushambulia utu wa mwingine. Ndoa yenye afya huruhusu hisia kuzungumzwa kwa uwazi bila hofu.
Mipaka ya kihisia na kiakili
Si jukumu lako kubeba hisia zote za mwenza wako. Kila mtu anapaswa kuwajibika kwa hisia na uamuzi wake. Katika uhusiano mwingi, mmoja hujiona kama mkombozi wa mwenzake. Hali hii huonekana kama upendo, lakini kwa ndani huzaa uchovu na mzigo wa kihisia.
Kujua mipaka ya kihisia kunakusaidia kutambua kwamba unaweza kusaidia, lakini huwezi kuokoa kila kitu. Unaweza kusikiliza, lakini si lazima ukubali kila lawama. Huu ni msingi wa uhusiano ulio sawa.
Mipaka ya kimwili na heshima
Mwili wa mtu ni wake, hata ndani ya ndoa. Mipaka ya kimwili inalinda heshima, usalama na ridhaa. Kulazimishana, kushinikiza au kudharau hisia za mwenzako,huacha majeraha ya ndani yasiyoonekana kwa macho. Uhusiano wenye afya hujengwa juu ya ridhaa na maelewano, si hofu au wajibu wa kulazimishwa.
Fedha na mipaka katika ndoa
Migogoro mingi ya ndoa huzunguka suala la fedha. Kukosa mipaka ya kifedha husababisha matumizi ya siri, lawama na kupotea kwa uaminifu. Uwazi, uamuzi wa pamoja na heshima katika matumizi ni sehemu ya mipaka muhimu inayolinda amani ya ndoa. Kama anavyosema mwandishi Dave Ramsey, fedha zinahitaji mpango na mazungumzo ya wazi, si hisia za ghafla.
Kwa nini watu huogopa kuweka mipaka?
Wengi huogopa kuweka mipaka kwa kuhofia kukataliwa, kuonekana wabinafsi au kuvunja uhusiano.
Lakini ukweli ni kwamba mtu anayekupenda kwa dhati ataheshimu mipaka yako. Uhusiano wenye afya unahitaji ukaribu na nafasi kwa wakati mmoja. Bila nafasi, ukaribu hukosa pumzi.
Kujua mipaka yako katika ndoa na uhusiano ni hatua ya ujasiri na hekima. Ni kitendo cha kujipenda na kumheshimu mwenzako kwa wakati mmoja.
Mipaka hujenga ndoa zilizo salama, uhusiano wenye heshima na upendo unaodumu. Upendo wa kweli hauhitaji mtu ajipoteze, bali ujitambue.
Kama wanavyosisitiza wataalamu wa uhusiano, mipaka si adui wa upendo, bali ni mlinzi wake. Ndoa yenye mipaka ni ndoa yenye amani. Uhusiano wenye mipaka ni uhusiano wenye maisha.
