
Kampuni ya huduma za fedha kidijitali, Mixx kwa kushirikiana na kampuni ya vifaa vya kielektroniki Hisense, wametambulisha rasmi kampeni itakayowapa Watanzania nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo kwenda Kombe la Dunia.
Kampeni hiyo ambayo imezinduliwa kwa ushirikiano na Hisense, itawawezesha wateja kujishindia zawadi za fedha taslimu za kila siku zenye thamani ya Sh1 milioni, vifaa vya majumbani ikiwemo televisheni, friji na spika za PartyBox, pia kuna safari ya bure kwenda Mexico kwa washindi watano na mshindi wa jumla ambaye ataondoka na zawadi kuu ya Sh 50 milioni mwishoni mwa kampeni.
Kampeni hiyo, iliyopewa jina la “Jimixx FIFA World Cup 2026 na Hisense”, ina kauli mbiu isemayo “Kila muamala ni bao la ushindi”. Kampeni hiyo imeanza Mei hadi mwisho wa Julai 2026, ikiwa na lengo la kuadhimisha na kusherehekea Kombe la Dunia pamoja na kuhamasisha matumizi ya huduma za fedha kidijitali nchini.
Kupitia kampeni hiyo, wateja watajishindia zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu hadi shilingi 1milioni kila siku, pamoja na vifaa vya kisasa vya nyumbani kutoka Hisense.
Aidha, washindi watano watapata fursa ya safari ya kwenda Mexico kushuhudia mechi za Kombe la Dunia moja kwa moja huku gharama zote zikiwa zimelipwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, alisema kampeni hiyo inalenga kuunganisha Watanzania kupitia mchezo wa soka huku ikihamasisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali.
“Mpira wa miguu ni mchezo unaowaunganisha Watanzania na dunia kwa ujumla. Kupitia kampeni hii tunawapa wateja wetu nafasi ya kufurahia soka huku wakinufaika na urahisi wa huduma za kifedha kidijitali na kujishindia zawadi zinazoweza kubadilisha maisha yao,” alisema Pesha.
Akizungumza kwa niaba ya Hisense, Tahera Karim, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mars Communications Ltd, alisema ushirikiano huo unalenga kuongeza msisimko wa Kombe la Dunia kwa Watanzania kupitia zawadi mbalimbali.
