Wabunge wajibu muswada wa maseneta Bunge la MarekaniWabunge wajibu muswada wa maseneta Bunge la Marekani

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikilieleza Bunge kuwa itatoa majibu ya kidiplomasia kufuatia hatua ya maseneta wawili wa Marekani wanaoshinikiza Tanzania iwekwe vikwazo, baadhi ya wabunge kwa upande wao wametaka heshima kwa uhuru na mamlaka ya nchi kupewa kipaumbele.

Kufuatia shinikizo la maseneta hao wawili wa Marekani, Jeanne Shaheen na Ted Cruz, Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema tayari wamemwelekeza Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dk Elsie Sia Kanza kufanyia kazi hoja za maseneta hao.

Pia, Balozi Kombo amesema kiutaratibu hoja zilizotolewa maseneta hao ndani ya Bunge lao zinatakiwa zijibiwe na wabunge wa Tanzania kama ilivyofanyika.

Hayo yameibuka bungeni leo wakati Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Mungula alipokuwa akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mungula alilieleza Bunge kuwa Mei 20, 2026,  maseneta hao wa Marekani,, waliwasilisha muswada unaoitwa Reassessing the United States-Tanzania Bilateral Relationship Act, wanapendekeza Marekani kufanya tathmini upya ya ushirikiano wake wa kiusalama, kiuchumi na kidiplomasia na Tanzania.

Mbunge wa Mtama Nape Nnauye  akizungumza wakati wa kuchangia mjadala wa makadilio na matumizi ya Bajeti ya  Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika mashariki kwa mwaka wa Fedha wa 2026/2027 jiojini Dodoma. Picha na Said Khamis

Pi, unapendekeza kuwekwa kwa vikwazo kufuatia madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa kisiasa uliotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akisoma maelezo ya seneta Cruz, katika muswada ambao upo hatua ya kujadiliwa na baraza hilo, amesema muswada huo si mzuri kwa Serikali ya Tanzania, akiitaka kuuchukulia kwa umuhimu wake.

“Kama walivyosema kuwa Tanzania tunakosa uhuru wa kuabudu na vilevile kuna unyanyasaji wa kisiasa, Tunafahamu Watanzania tunaishi kwa udugu na yaliyotokea Oktoba 29 tayari Serikali imeshachukua hatua na kuwa watakaobainika watafikishwa kwenye Tume ya Kijinai na kuwajibika,” amesema.

Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Addo Shaibu akizungumza wakati wa kuchangia mjadala wa makadilio na matumizi yaBajeti ya  Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika mashariki kwa mwaka wa Fedha wa 2026/2027 jiojini Dodoma. Picha na Said Khamis

Mungula ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje, wanadiplomasia na wataalamu wake kuwasihi Wamarekani kuenzi na kuendeleza uhusiano wa Tanzania na Marekani, akisema kupoteza uhusiano huo kuna athari mbaya kwa nchi.

“Muswada huu ukipita utaweka vikwazo takribani vinane, ikiwemo watu binafsi na viongozi wetu wa vyombo vya uhuru kuwekewa vikwazo.

“Ikiwezekana vilevile hata kuichukua kamati yetu ya mambo ya nje iende Marekani kuliongelea hili ili tutumie diplomasia kulikamilisha hili tatizo,” amesema.

Kwa upande wake mbunge wa Mtama, Nape Nauye amesema; “Tulipopitia matatizo Rais Samia (Samia Suluhu Hassan) amesimama imara, ameonyesha uzalendo na hii limepeleka salamu duniani kuwa hata tunapopitia matatizo bado tunaweza kutatua wenyewe changamoto zetu.

“Niiombe Wizara, mara kadhaa tuwakumbushe marafiki zetu, tupo tayari kusaidia nao kama marafiki, lakini nchi hii ipo huru, hatukupewa uhuru wetu kama zawadi, tulipambana tukapata uhuru wetu.

“Tupo huru, tunathamini mchango wao, lakini muhimu wakumbuke, wasitumie changamoto tulizonazo kutuumiza, kutunyanyasa, kutukandamiza, kutudhalilisha; watumie fursa tunayowapa kufanya nao kazi kwa heshima na upendo,” amesema.

Nape amesisitiza kuwa changamoto za siku na muda mfupi zisitumike kama fimbo kwao kuiadhibu nchi.

Kwa upande wake Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, amesema Tanzania ina uhusiano wa kihistoria na Marekani hivyo ameitaka Wizara kumaliza tatizo hilo kwa kuheshimu uhuru wa nchi.

“Wasitumie kigezo hicho kutukandamiza kujinufaisha kisiasa. Tulitarajia wenzetu wangewasiliana na Kamati yetu ya Bunge kabla ya kuandaa muswada huo ambao unataka kufuta viza kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi ambao wengine ni wahanga, viongozi wetu wa ulinzi ambao hawajapewa nafasi ya kusikilizwa, ni jambo linalokwenda kuharibu uhusiano wetu,” amesema.

Amesisitiza kuwa maseneta hao hawana taarifa sahihi kuhusu madai wanayoyaibua katika muswada huo.

Naye mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu amesema Tanzania ni Taifa lisilofungamana na upande wowote akisisitiza kuwa Taifa limejikita kulinda uhuru na mamlaka yake.

“Huo muswada na mimi nimebahatika kuuona. Alipoingia madarakani Rais Samia alikwenda kuwatembelea wanasiasa waliokuwa wamekimbia Taifa na kuruhusu uhuru wa vyama vya siasa Tanzania. Tusije tukaruhusu heshima ya Rais wetu na nchi yetu ikachezewa na viongozi wetu wakawa wanyonge,” amesema.

Amesisitiza kuwa Rais Samia ameendelea kuboresha mazingira ya kisiasa, uhuru wa kuabudu na kwamba Taifa halina mambo ya kutesana kidini.

Kingu ametaja hatua zilizochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani, ikiwemo kuruhusu uhuru mkubwa wa kisiasa na maridhiano, zinaonesha dhamira ya kuendelea kuimarisha demokrasia nchini.

Hata hivyo, Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Addo Shaibu ameonya kuwa sera ya kutofungamana na upande wowote isitumike kufumbia macho hoja za haki, uwajibikaji na kupinga ukandamizaji duniani.

Shaibu amesema Sera ya Taifa ya kutofungamana na upande wowote isifanye jamii kukaa kimya kwenye ukandamizaji wa haki.

Ameitaka Serikali kusimama katika kusimamia haki na uwajibikaji ikipinga dhuluma na uonevu wa mataifa makubwa, akisisitiza juu ya sera ya kutofungamana.

“Sera yetu ya kutofungamana na upande wowote, isitufanye tukae kimya pale ambapo kuna ukandamizaji wa haki, dhuluma na mwenendo usiofaa duniani,” amesema.

Msimamo wa Serikali

Akitoa msimamo wa Serikali Waziri Kombo amesema: “Baada ya Uchaguzi, Rais Samia alinipa jukumu zito sana ambalo siwezi kulisema hapa. Nawapongeza sana (wabunge) kwa hoja zenu, michango yenu yote ni mizuri nitaifanyia kazi, nitaiwasilisha kidiplomasia kwa Rais,” amesema.

Ameahidi kuwa Serikali itachukua njia za kidiplomasia katika kukabiliana na misukosuko inayoibuka ili kulinda mahusiano ya Tanzania na mataifa ya nje.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza wakati akiwasilisha Makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

“Tunawaahidi na mimi nawaahidi kama alivyosema Nape, wanaotaka kutumia udhaifu wetu mdogo uliotokezea kuonea, kuinyanyasa, kuikandamiza nchi, tutakwenda nao kwa jibu hili zuri sana la kidiplomasia,” amesema.

Ametaja juhudi za Rais Samia kujenga mridhiano, falsafa ya R4 na uhuru wa kuabudu kama hatua muhimu iliyovutia mataifa mbalimbali kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali.

Waziri Kombo amesema kuhusu muswada wa maseneta wa Marekani, wizara itachukua hatua stahiki akitoa wito kwa wanaoituhumu Tanzania kwa maovu ya ubaguzi, uonevu kuja Tanzania ili kushuhudia hali ilivyo.

“Kule wanasema tunachinjana, wote wawili hawajawahi kufika Tanzania. Tumeshatuma barua ya kuwaalika waje, tutawalipia sisi gharama zote hadi malazi waje Tanzania waweze kuona wapi tunachinjana, wapi tunapigana, waone watu wanavyokutana kwenye matatizo, Watanzania tunavyoishi. Tumeshawalika,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa kujibu hoja kwa hoja akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kutumia njia ya kidiplomasia katika kushughulikia matatizo ya kimataifa.

Hoja za maseneta

Katika muswada wao wa sheria wa vyama viwili, Jeanne Shaheen na Ted Cruz wanaitaka Serikali ya Marekani kufanya tathmini upya ya uhusiano wake na Tanzania kufuatia madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.

Muswada huo unaojulikana kama Reassessing the United States-Tanzania Bilateral Relationship Act unalenga kuchunguza kwa kina mwenendo wa demokrasia nchini Tanzania, ukandamizaji wa kisiasa na hali ya usalama kufuatia taarifa za vurugu dhidi ya waandamanaji.

Muswada huo uliowasilishwa na Jeanne Shaheen na Ted Cruz, umesomwa kwa mara ya pili na sasa umepelekwa kwenye kamati ya kwa ajili ya kutungwa sheria na Seneti na Baraza la Wawakilishi la Marekani.

Miongoni mwa mambo ambayo muswada huo umeyarejea kama mambo yanayoichafua sifa ya Tanzania ni  Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambao muswda huo unaeleza ulikuwa na mwingilio wa kisiasa, ikiwemo uchakachuaji wa kura na dosari katika uhesabuji wa kura.

Kuhusiana na kasoro za uchaguguzi huo, muswada huo unadai kuwa wakati wa mchakato wa kuelekea katika uchaguzi huo kulikuwa na matukio mbalimbali ya utekaji na kupotezwa kwa watu wenye misimamo ya kisiasa nchini Tanzania.

Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Addo Shaibu akizungumza wakati wa kuchangia mjadala wa makadilio na matumizi yaBajeti ya  Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika mashariki kwa mwaka wa Fedha wa 2026/2027 jiojini Dodoma. Picha na Said Khamis

Hivyo muswada huo unawataka Waziri wa Mambo ya Nje, kwa kushirikiana na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mwakilishi wa Biashara na wakuu wa mashirika mengine nchini humo, kufanya tathmini ya kina ya uhusiano wa Marekani na Tanzania na machafuko yaliyotokea nchini na katika nyanja mbalimbali.

Kwa mujibu wa muswada huo, matokeo ya tathimini hiyo yanapaswa kuwasilishwa katika kamati husika za Bunge si zaidi ya siku 90 baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo.

Pia, Waziri wa Mambo ya Nje anatakiwa kuwasilisha kwa kamati husika si zaidi ya siku 180 baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo; orodha viongozi wa  nafasi ya juu katika Serikali ya Tanzania, CCM, vyombo  vya ulinzi na usalama aliyehusika moja kwa moja au isivyo moja kwa moja na mambo yafuatatayo:

Kuagiza, kudhibiti au kuelekeza utekaji, upotezwaji wa kulazimishwa au vizuizi vya kiholela dhidi ya wapinzani wa kisiasa, waandishi wa habari, au wanaharakati wa asasi za kiraia;

Mbili, udhibiti wa habari, kuzimwa kwa mawasiliano, au vikwazo vingine dhidi ya vyombo vya habari, upatikanaji wa intaneti, au uhuru wa kujieleza vinavyolenga kuficha ukiukwaji wa haki za binadamu au kuzuia usambazaji wa taarifa za kuaminika, ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa dini.

Mbunge wa  Singida Magharibi , Elibariki Kingu  akizungumza wakati wa kuchangia mjadala wa makadilio na matumizi yaBajeti ya  Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika mashariki kwa mwaka wa Fedha wa 2026/2027 jiojini Dodoma. Picha na Said Khamis

Tatu, matumizi ya mbinu za ukandamizaji wa kuvuka mipaka zinazolenga raia wa kigeni, raia wa Tanzania, na wanadiaspora katika ngazi ya kikanda na kimataifa, mauaji ya kiholela nje ya sheria, mateso, au ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu zinazotambulika kimataifa.

Vikwazo vinavyopendekezwa katika muswada huo dhidi ya viongozi, au watu watakaotajwa kuhusika na matukio ya ukandamizaji wa aina yoyote wa haki za binadamu yaliyotajwa hapo juu ni pamoja na kufungia na kuzuia miamala yote inayohusu mali na masilahi ya mhusika iliyoko au inayoingia Marekani;

Mbili, kuzuiwa kuingia nchini Marekani, kutokupewa visa au nyaraka nyingine za kuingia Marekani, kufutwa kwa visa au nyaraka nyingine za kuingia za mgeni zilizokwishakutolewa kwa mhusika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *