Mgodi wazindua kliniki kutatua changamoto za wanakijijiMgodi wazindua kliniki kutatua changamoto za wanakijiji

Tarime. Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara umezindua kliniki maalumu ya kusikiliza na kutatua malalamiko pamoja na migogoro ya wananchi kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mahusiano na jamii.

Kliniki hiyo inayohusisha wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, mgodi pamoja na wadau wengine, inalenga kupata suluhisho la kudumu la changamoto mbalimbali zinazojitokeza kati ya wananchi na mgodi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kliniki hiyo uliofanyika Nyamongo leo Jumanne Mei 26, 2026, Meneja Uhusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi amesema licha ya mahusiano kati ya mgodi na wananchi kuimarika kwa kiasi kikubwa, bado zipo changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa kudumu.

Ametaja changamoto ya fidia kuwa miongoni mwa masuala yanayoendelea kujitokeza, akisema baadhi ya wananchi wamegoma kupokea malipo wakidai kutoridhishwa na kiwango walichopangiwa.

 “Wananchi 728 walifanyiwa tathmini katika eneo la Nyabirama na malipo yao yapo tayari. Kati yao, 667 wamepokea fidia na kupisha shughuli za mgodi, huku 61 wakiendelea kusubiri, ambapo watu 44 ni wa familia moja,” amesema.

Uhadi amesema mgodi huo umeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambapo miradi 103 imepangwa kutekelezwa mwaka huu, huku 70 ikiwa tayari imekamilika na mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Amesema kliniki hiyo itazunguka katika vijiji vyote 11 vinavyozunguka mgodi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kusikiliza changamoto zao moja kwa moja.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wamepongeza hatua hiyo, wakisema itasaidia kupunguza migogoro na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na mgodi.

Mkazi wa Kijiji cha Kewanja, Mwita Omahe amesema pamoja na kuimarika kwa mahusiano, bado kuna changamoto ya ubovu wa barabara za mitaa inayohitaji kushughulikiwa.

Kwa upande wake, Felister Rioba amesema wananchi wanapaswa kushirikiana na mgodi huo kwa maendeleo ya jamii badala ya kuwa chanzo cha migogoro inayoweza kukwamisha uwekezaji.

Akizindua rasmi kliniki hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele amesema mpango huo utasaidia kupunguza na hatimaye kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi wanaoizunguka migodi hiyo.

Pia, amewataka watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayofadhiliwa na mgodi huo, ikiwemo ujenzi wa soko la dhahabu Nyamongo na stendi ya kisasa Nyamwaga.

“Nimeelezwa kuwa ili miradi hiyo iweze kuendelea, ni lazima hati za maeneo husika zipatikane kwa wakati. Watendaji hakikisheni mnakamilisha taratibu zote zinazohitajika bila kuchelewesha maendeleo,” amesema.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuongeza matumaini na kuimarisha mahusiano chanya kati ya wananchi na mgodi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *