
Ikiwa leo ni sikukuu ya Eid El-Adha, tunakupeleka huko Ukanda wa Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli kuona jinsi watoto badala ya kusherehekea sikukuu hii wanajihusisha na uchuuzi wa bidhaa ndogo ndogo ili waweze kukimu familia zao.
Katika mtaa wa Al-Jalaa katikati mwa Jiji la Gaza, Mohammad Ashour habebi vitu ambavyo watoto wa umri wake kwa kawaida hubeba kabla ya Eid.
Ninauza kahawa ili kusaidia familia yangu
Badala yake, ameshika birika la kahawa, amebeba mfuko mgongoni, na anatembea miongoni mwa wapita njia akitafuta wateja kabla ya sikukuu ya Eid al-Adha, ambayo mwaka huu inawadia huku Ukanda wa Gaza ukiendelea kuteseka kutokana na madhara ya vita na kuporomoka kwa uchumi.
Mohammad amemwambia mwandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa huko Gaza kuwa, “Ninauza kahawa ili kusaidia familia yangu. Zamani, wakati wa Eid, Eid ilikuwa siku ya furaha; tulikuwa tukitoka nje, kutembea, na kwenda bustanini, migahawani, na baharini. Lakini sasa, chini ya vita, Eid imekuwa siku ya kawaida kama siku nyingine yoyote.”
Zamani Eid ilikuwa fursa ya kupata nguo mpya
Katika mitaa mingine ya jiji hilo, Wasim Aliwa anaonekana akiwaita wapita njia kwa sauti yake ya kitoto wanunue chokoleti.
Kabla ya vita, Eid kwake ilikuwa fursa ya kununua nguo na kutoka pamoja na familia yake. Sasa, anasema, “Wakati wa Eid, kabla ya vita, tulikuwa tukitoka na kununua nguo. Lakini sasa, kila kitu kimekuwa kibaya.”
Wasim anaongeza kuwa, “Natumaini Eid ijayo itakuwa nzuri, kutakuwa na vinyago na kila kitu, na tutaweza kununua nguo ambazo bado hatujanunua.”
Eid ya sasa vifusi vimezingira watoto
Ingawa Eid al-Adha inapaswa kuhusishwa na mikusanyiko ya kifamilia, nguo mpya, na ugawaji wa nyama, watoto wa Gaza sasa wanasimama katikati ya vifusi vya nyumba zilizoharibiwa, wanajazana ili kupata chakula kutoka kwenye jiko la jumuiya, au kubeba madumu ya maji yanayoweza kutumika huku kukiwa na upungufu mkubwa wa huduma za msingi.
Kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), watoto 637,477 wenye umri wa kwenda shule hawana fursa endelevu ya kupata elimu rasmi ya ana kwa ana. Watoto 64,000 wenye umri wa miaka mitano hawana fursa ya kupata elimu ya awali ya utotoni.
OCHA imebainisha kuwa hali ya kibinadamu huko Gaza bado ni mbaya sana, huku familia nyingi zikiendelea kuishi katika mahema yaliyojaa watu wengi, shule, na majengo yaliyoharibiwa, katikati ya vizuizi vikubwa vya upatikanaji wa maji safi na usimamizi wa taka.
