Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiwataka majaji wapya wa Mahakama ya Rufani kwenda kutenda haki bila upendeleo, huba na chuki, wadau mbalimbali wamepongeza kwa ujumbe huo wakisisitiza viongozi hao wa Mahakama, wafuate msingi ya Katiba.
Rais Samia amesema hayo jana Jumanne, Mei 26, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kuwaapisha majaji tisa wa Mahakama Kuu kuwa wa Mahakama ya Rufani ambao aliwateua hivi karibuni.
Majaji hao ni Imani Aboud, Rabia Mohamed, Dk Yose Mlyambina, Immaculata Banzi, Cyprian Mkeha, Yohane Masara, Dk Juliana Masabo, Abdi Kagomba na Mzee Ibrahim.
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa uapisho wa majaji uliofanyika leo Jumanne Mei 26, 2026 Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Samia amesema majaji hao wamepata uteuzi huo kutokana utumishi wao uliotukuka ndani ya Mahakama, akiwataka kwenda kuimarisha utendaji wa haki na kulinda uhuru wa mhimili huo.
“Nendeni mkaitumikie nchi kwa uzalendo, werevu bila upendeleo, huba na chuki katika kutoa maamuzi ya hukumu zenu.
“Mna dhima kubwa kwa nchi hii katika kutenda haki kuhakikisha haki za wananchi zinatimia,” amesema.
Rais Samia amesema kutimiza haki ni kutimiza kusudi la Mungu akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kutaongeza ufanisi katika mhimili wa Mahakama nchini.
“Uteuzi wenu ni kuongeza uwezo wa watu wa kufanya kazi katika kusimamia haki,” amesema Rais Samia.
Aidha, amewataka majaji hao kwenda kulinda heshima na uhuru wa mahakama, akisisitiza ufanisi na weledi katika utumishi wao ambao amesisitiza uzingatie utu, taifa na nchi.
“Uamuzi wenu uzingatie utu kwanza, Taifa kwanza, nchi kwanza,” amesisitiza.
Mwananchi limezungumza na wadau mbalimbali juu ya ujumbe huo wa Rais Samia kwa majaji. Mwanadiplomasia mkongwe, Profesa Benson Bana amesema uteuzi huo unaonesha kuzingatia ikama katika utumishi wa mahakama, akieleza kuvutiwa na wito wa haki alioutoa Rais Samia.
“Uteuzi wake naona umezingatia ikama ya utumishi wa mahakama. Wengi ukiangalia nyuso wanaonekana kuwa na umri usiopungua 50, la muhimu zaidi katika hotuba ya Rais.
“Amezungumzia neno haki ambalo kwa muda mwingi limekuwa adimu kwa wanasiasa,” amesema.
Amesema haki ndiyo inayozaa amani, akisisitiza kuteuliwa kuwa jaji wa mahakama ya rufasni ni jambo kubwa.
“Tunaamini vyombo vya uchunguzi vimefanya kazi yake wamekidhi vigezo, na matumaini ya wananchi ni kuona mhimili wa mahakama inakuwa sehemu inayotoa haki,” amesema Profesa Bana aliyewahi kuwa Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mwanahabari mkongwe, Jesse Kwayu anasema hatua ya Rais Samia kutoa wito wa haki na uhuru wa Mahakama ni wito muhimu kwa watumishi wa Mahakama nchini.
“Kuwaambia watende haki ndiyo kazi ya Mahakama. Kwahiyo amewakumbusha wajibu wao na hiyo ndiyo kazi yao. Katiba yetu inatambua katika mgawanyo wa mihili ya serikali ambapo bunge linatunga sheria,” amesema.
Kwa upande wake, Loserian Kasale wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), amesisitiza umuhimu wa sheria zinazolinda haki na uhuru wa Mahakama, katika kulinda haki za binadamu.
“Kimsingi suala uhuru wa Mahakama halipaswi kutoka kwa mtu, uhuru wa mahakama na utendaji wa haki unapaswa uundiwe mifumo ili kuondoa kwenye utashi wa mtu.
“Rais amekumbushia jambo muhimu kwa watumishi wa mhimili wa mahakama. Nami nitoe wito kwa majaji kuitenda haki kwa mujibu wa katiba na wasipofanya hivyo mifumo ya ikisheria iwawajibishe,” amesema.
