
Hakuna jambo linalokera kuliko lile linalojirudia bila kuisha. Mtu yeyote huweza kufanya makosa na kusamehewa, lakini mfanyakazi huweza kupoteza ajira yake baada ya kuonywa zaidi ya mara mbili. Huku majumbani wanandoa hutalikiana kwa sababu hizohizo za kujirudia kwa makosa. Wazazi hukosana na watoto wao kwa sababu hizohizo, na hata marafiki huweza kutengana kufuatia mmoja wao kurudia makosa.
Ukiacha machungu yanayosababishwa na kosa lenyewe, kinachosumbua zaidi ni ile hali ya kujirudia. Waswahili wana tahadhari juu ya mambo yanayojirudia bila kuisha. Neno linapojirudia hupunguza umakini wake; kwa mfano “Baba analima” ni tofauti na “Baba analimalima”. Sentensi ya kwanza inaonesha umakini, lakini ya pili inaondoa umakini. Linamwonesha akifanyafanya tu, na si kufanya.
Jambo hata likiwa zuri, linapojirudia mara nyingi hukinaisha. Matokeo yake uzuri hugeuka kuwa ubaya, na ubaya unaweza kusababisha maumivu na hata msongo. Ndio maana hata uwe na kazi nzuri, inakupasa kwenda likizo kila baada ya mwaka ili isikuchoshe na kukutia msongo. Maana mchoko wa jambo moja unaweza kusababisha mengine yote yasiende. Unaweza kusababisha kuchoka maisha kwa ujumla.
Jemedari mmoja wa utawala wa Kinazi huko Ujerumani ya Mashariki alibuni njia ya mateso ya kikatili sana. Pindi alipomkamata mpinzani wa utawala wao, alimfungia kwenye handaki lenye kiza usiku na mchana. Akaweka humo chombo kinachotoa sauti endelevu. Sauti ilifanana na tone la maji lililoangukia ndoo ya bati kwa mwendo wa mshale wa sekunde. Kwa hiyo mateso ya kwanza yalikuwa kiza kisicho na mapambazuko, na ya pili ni sauti ile isiyo na ukomo.
Matokeo yalikuwa ni kifo cha kila aliyefungwa humo baada ya muda mfupi. Marehemu hawakuonekana na majeraha, sumu wala hawakufa kwa njaa. Wataalamu wanasema haya ni mateso ya kiwango cha juu zaidi ya mateso mengine yanayojulikana. Baada ya utawala wa Kinazi kusambaratishwa, Jemedari huyu alisakwa kila kona. Alipopatikana alikutwa na hatia, akahukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Kitu kimojawapo kinachowatesa sana Watanzania ni marudio ya marekebisho yanayofanyika muda wote. Huku mtaani ni aghalabu siku kupita bila umeme kukatwa. Maelezo yanasema ukarabati wa miundombinu ndiyo sababu kuu. Leo waya umekatwa na kunguru, kesho nguzo iliyoliwa na mchwa itaanguka… Inaeleweka kuwa marekebisho yanafanyika ili huduma zipatikane kwa ubora, lakini kwao imekuwa kinyume.
Umeme ni nyenzo muhimu sana ya maendeleo katika wakati huu. Asilimia kubwa ya Watanzania wanategemea ukulima wa kisasa na ujasiriamali. Hivyo kwao umeme ni kitu kisichoepukika katika umwagiliaji mazao na uzalishaji bidhaa. Lakini hata mama wa nyumbani anahitaji sana umeme katika kuunga mkono matumizi ya nishati safi ya kupikia. Wanafunzi kadhalika, hawawezi kujisomea bila nishati hii.
Tuchukulie mfano wa nyumba yenye matatizo ya umeme: Kila siku baba anakuja nyumbani na mafundi, anawakuta mama akiwa jikoni na watoto wakijisomea au kutazama TV. Mafundi wanakata umeme, wanachokoachokoa kisha kuuwasha umeme na kuondoka. Hali hii iwe inajirudia kila siku, mwaka baada ya mwaka. Nina uhakika baba ataiona familia yake ikidhoofika kiafya na kielimu.
Tatizo lingine kubwa ni matengenezo ya barabara yasiyoisha. Kila kona kuna malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara zao. Si kwamba hazijengwi, ila barabara inaanza kuchakaa muda mfupi tu baada ya kujengwa au kukarabatiwa. Uchakavu wa barabara ni sababu mojawapo ya ajali za mara kwa mara. Tatizo hili limekuwa likisababisha watu kupoteza maisha na kupata ulemavu. Wagonjwa na wajawazito wapo kwenye hali hatarishi kutokana na tatizo hili.
Hivi karibuni nilisikiliza Bunge la Bajeti. Baadhi ya wabunge walionyesha kukerwa na hali ya kujirudia kwa matengenezo ya barabara zetu. Majadiliano yaliashiria kuwapo na tatizo la ubora wa barabara hizi. Wakati tukiwa watoto tulizikuta barabara zenye afya (wenyewe tuliziita “za Mjerumani”). Tukaishi nazo kwa miaka mingi bila kuona mashimo wala viraka hadi tulipokuwa watu wazima.
Ujenzi wa sasa ni tofauti sana. Barabara iliyojengwa mwaka jana imeshaanza kuonyesha makunyanzi. Sijui tatizo ni vifaa, mkandarasi au msimamizi. Hivyo vitu vitatu vinategemeana kama mafiga, figa moja likipelea ugali utatoka mbichi. Unaweza kumlaumu mkandarasi kumbe viongozi ndio wapigaji. Wanaweza mleta mkandarasi wa kupaua majengo au kumnunulia lami ya kufanyia maigizo badala ya kujengea barabara.
Kipindi hiki tunachoelekea maridhiano baada ya mtiti wa Oktoba, ni lazima tuwe makini sana kwa kila jambo. Tume ya Jaji Chande ilibaini moja ya sababu za vurugu ilikuwa “hasira za muda mrefu”. Na hasira ni upofu, unaweza kumkasirikia mtu asiyekukosea. Unakuta mtu anagombana na mumewe, kwa hasira anakwenda kuvunja TV. Mwingine anaweza kumnunia jirani baada ya kucheleweshewa mshahara kazini kwake.
Tunaamini kuwa Serikali inaweza kuyamaliza matatizo haya. Kuna nchi ziliyoamua kujiondoa kwenye mashindano ya kombe la dunia, wakashughulika kurekebisha timu zao nje ya mashindano. Basi inawezekana kuishi bila umeme kwa muda, tukafanya marekebisho na kupata huduma iliyo bora. Na Serikali inaweza kuamua kuwashughulikia wajenzi wa barabara zinazoishi miezi miwili. Marekebisho yaishe ili tufaidi matunda ya uhuru.
